Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyongeza, kodi kilio cha wafanyakazi nchini

Dar es Salaam. Wakati ulimwengu unaelekea kuadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi “Mei Mosi”, Tanzania imetajwa kuwa na viwango vikubwa vya kodi ya mishahara ‘PAYE’.
Licha ya kodi hiyo inayojulikana “Paye” imepunguzwa mara kadhaa, hata hivyo bado inaonekana kuwa juu, jambo linaloelezwa ni mzigo kwa wafanyakazi licha ya kupata nyongeza ya mshahara ambayo nayo inadaiwa bado ndogo kwa hali ya maisha ya sasa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mtanzania anayepokea mshahara chini ya Sh270,000 hakatwi kodi lakini anayepokea kuanzia Sh270,000 hadi Sh520,000, anakatwa kodi ya asilimia 8 ya kiasi kinachoongezeka baada ya Sh270,000.
Wafanyakazi wanaolipwa kuanzia Sh520,000 hadi Sh760,000 wanakatwa Sh20,000 ukiongeza na asilimia 20 kwa kiasi kinachozidi baada ya Sh520,000.

Vilevile, kwa wafanyakazi wanaopokea mshahara kuanzia Sh760,000 hadi Sh1 milioni, wanakatwa Sh68,000 ukiongeza na asilimia 25 ya kiasi kinachozidi baada ya Sh760,000.
Wanaopokea mshahara wa zaidi ya Sh1 milioni, wanakatwa kodi ya Sh128,000 ukiongeza na asilimia 30 ya kiasi kichoongezeka baada ya hiyo Sh1 milioni.

Itakumbukwa tangu mwaka 2016 hadi mwaka 2021, watumishi wa umma hawakuwahi kuongezwa mishahara, mara ya mwisho Rais Samia aliongeza mishahara hiyo mwaka jana hata hivyo wafanyakazi walilalamikia ongezeko hilo kuwa ni dogo.

Baadhi ya wafanyakazi wanasema wanakatwa kiasi kikubwa cha kodi ya mshahara, jambo ambalo linawafanya wasione unafuu wa nyongeza ya mshahara inayotolewa na Serikali ukilinganisha na kupanda kwa gharama za maisha.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Ko`siryamu, Clinton Weston, alisema kodi hiyo ni muhimu kwani fedha zinazopatikana zinasaidia kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii lakini zimekuwa zikileta maumivu kwa wafanyakazi kutokana na makato yake kuwa makubwa.

Weston ameiomba Serikali kuangalia namna ya kupunguza asilimia za makato katika kodi hiyo ili ziwe rafiki kwa wafanyakazi na kuwafanya wafurahie kulipa kodi zitakazosaidia shughuli za maendeleo.

“Kodi inapokuwa kubwa bado mfanyakazi huyo anakatwa makato mengine kama malipo ya Heslb kwa wale waliosomeshwa kwa mkopo na makato mengine ambapo mwisho wa siku muhusika anajikuta amebaki na kipato kidogo ambacho hakitoshelezi mahitaji yake kwa mwezi,”alisema.

Kwa upande wake, Suzana Kashube, alisema ukubwa wa kodi hiyo na makato mengine unafanya baadhi ya wafanyakazi kuvunjika moyo kwani inafanya wanachokipata baada ya makato hayo kuwa kidogo na wakati mwingine hakitoshelezi mahitaji.

“Wakati mwingine tunaingia kwenye madeni ili kukidhi mahitaji kwa sababu kipato ni kidogo, maisha yamepanda na tuna makato mengine pia. Hapo kuna NSSF naPSSSF, kuna wale wa bodi ya mikopo, kuna vyama vya kitaaluma, hapo unabaki na nini?” alihoji mfanyakazi huyo.

Hata hivyo jitihada za Mwananchi, kutaka ufafanuzi wa kilio cha wafanyakazi hao kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene hazikuweza kuzaa matunda kutokana na simu yake kutopokelewa.

Vilevile, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa naye hakupatikana kuzungumzia madai hayo ya wafanyakazi.
 

Tucta wafunguka

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limebainisha kwamba limekuwa likipiga kelele kuomba kupunguziwa kodi ya mshahara na Serikali imekuwa sikivu katika kutekeleza jambo hilo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Herry Mkunda alisema wameomba mara nyingi kupunguziwa kodi ya Paye ambapo wakati Rais John Magufuli anaingia madarakani, alipunguza kutoka asilimia 11 hadi tisa na mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan alipunguza hadi asilimia nane.

“Mimi naona Serikali ina hiyo feeling (hisia) kwamba ni vizuri wakapunguza kodi kwa mazingira waliyonayo. Lakini kwenye kodi au vyanzo va mapato vinatofautiana kati ya nchi na nchi, inawezekana sisi kwenye hili tukawa juu kwenye maeneo mengine tukawa chini,” alisema.

Alisema wanaona kwamba Serikali imekuwa na utayari wa kupunguza kodi hiyo na kwamba kama mfanyakazi angefurahi ikipungua zaidi, lakini hadi sasa bado iko pazuri na anaishukuru Serikali kwa hilo.

Mkunda alisema karibu asilimia 90 ya mambo waliowasilisha kwa Serikali Mei Mosi ya mwaka jana kwenye sherehe hizo yalipatiwa ufumbuzi.

Katika sherehe za mwaka jana, Tucta walikuwa na maombi ya kutaka nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali inayolingana na hali halisi ya maisha ya Watanzania na kanuni mpya za kikotoo cha mafao ya mkupuo.

Mengine ni upandishaji wa madaraja, wafanyakazi waliotimuliwa na vyeti feki kulipwa michango yao waliyochangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii na sakata la kuwekwa ndani kwa watumishi wa umma na wakuu wa mikoa.

“Mwaka huu tunatarajia mambo mengine yaje lakini kwa kiwango kikubwa ni hayo ni maslahi ya wafanyakazi lakini vile vile kuongeza ushirikiano kati ya wafanyakazi, waajiri na Serikali kwa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu na majukumu yake,” alisema Mkunda, alipozungumza na gazeti.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU), Dk Paul Loisilie alisema katika mataifa yote duniani, wafanyakazi hutarajia Serikali kuboresha maslahi yao ikiwemo sera, sheria na kanuni zinazowahusu wafanyakazi.

“Mishahara iko katika makundi matatu ikiwemo nyongeza ya mishahara yenyewe ambalo Rais wa awamu wa mne Jakaya Kikwete aliliweza kwa kupandisha mishahara kila mara,” alisema.

Utawala wa Kikwete ulikuwa kati ya mwaka 2005 – 2015 huku ule wa awamu ya tano kuanzia Novemba 5, 2015 hadi Machi 17, 2021 chini ya Dk John Magufuli (sasa marehemu), haukuongeza mishahara.

Rais Samia aliyeingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Dk Magufuli, tayari ameongeza mishahara mara moja huku akisisitiza, ataendelea kuboresha maisha ya wafanyakazi.

Pili, Dk Loisilie ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) alisema wafanyakazi wangetamani kusikia ni nyongeza ya mwaka ya mishahara ambayo inawezesha kutofautisha kati ya mfanyakazi anayeajiriwa leo na miaka ya nyuma na upandishaji wa madaraja.

“Mfano mwaka jana waliongeza mishahara lakini ikawa haina maana kabisa yaani watu waliongezewa Sh20,000, halafu wakikatwa inabaki Sh12,000 watu wanatamani kusikia mwaka huu nyongeza ya mshahara kuwa kubwa kuliko ya mwaka jana,”alisema Dk Loisulie.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Peter Elias na Mariam Mbwana.