Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mrema aihoji Chadema maswali matano kupigwa kigogo wa Bawacha

Muktasari:

  • Sigrada anadaiwa kupigwa Machi 25, 2025 na mmoja wa walinzi wa Chadema kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche.

Dar es Salaam. Sakata la tuhuma za kupigwa kwa Mratibu wa Uenezi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Sigrada Mligo limechukua sura mpya baada ya kuibuka kwa mjadala mkali mtandaoni.

Mjadala huo umetokana na maelezo ya Mkurugenzi wa zamani wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema kuhoji maswali matano juu ya tukio hilo na uamuzi wa chama uliouchukuliwa.

Mrema ameibua maswali hayo baada ya taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia kueleza kuwa chama kinachunguza tukio hilo na kumuonya Mligo kuwa makini na asitumiwe kisiasa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika maelezo yake, Mrema anasema ametumia Katiba ya Chadema, Ibara ya 5.3.5, inayoeleza "kuwa tayari kupambana na namna yoyote ya uonevu, ukandamizaji, udhalilishaji na ubaguzi" juu ya kuhoji kilichompata Mligo.

Sigrada (34) anadaiwa kupigwa Machi 25, 2025 na mmoja wa walinzi wa Chadema kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche, mkoani Njombe.

Siku iliyofuata, Machi 26, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, alimtaja Noel Olevale, anayedaiwa kuwa mlinzi wa Chadema, kuwa ndiye anayetuhumiwa kufanya shambulio hilo la mwili.

Banga alisema tukio hilo lilitokea wakati viongozi wa Taifa wa Chadema walipokuwa kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Heche.

Leo Jumatatu, Machi 31, 2025, Chadema imetoa taarifa kwa umma ikisema inafanya uchunguzi wa kina, ili kubaini ukweli wa jambo hilo na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa katiba, kanuni na miongozo yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, chama hicho pia kinafuatilia “kwa makini kile kinachodaiwa kuwa njama za CCM za kutumia tukio hilo kwa manufaa yao binafsi.”

“Tunatoa wito kwa Sigrada Mligo kuwa makini na mahusiano yake na CCM ili kuepuka kutumiwa kwa malengo yasiyo na nia njema, ambayo yanaweza kuathiri si tu hadhi ya chama bali ya kwake pia kama kiongozi na usalama wake binafsi,” imeeleza taarifa hiyo

Chadema pia imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua inayochukuliwa kwa kushirikiana na vyombo husika vya ndani na nje ya chama na baadaye watatoa kauli rasmi kuhusu suala hilo kadri itakavyofaa.


Mrema aibua maswali matano

Baada ya taarifa hiyo, Mrema ametumia akaunti yake ya kijamii ya X kuzungumzia taarifa hiyo ya Chadema. Hatua yake imeibua mjadala kwa baadhi ya wachangiaji wa hoja hiyo, huku Mrema akijibu hoja zao.

Mrema ameanza kwa kusema: “Nimesikitishwa na taarifa hii ya chama, pamoja na kutolewa kwa kuchelewa sana,” akisema masikitiko yake yanatokana na mambo matano ambayo ni:

Mosi, chama hakikuona haja ya kulaani tukio la kiongozi wa wanawake taifa kupigwa na kuumizwa, kipigo kilichotolewa na mwanaume, bali kinasema ni taarifa zinazosambazwa mtandaoni.

Pili, chama hakikutoa pole kwa mgonjwa, mbona kinatoa pole hata kwa viongozi wa CCM wanapopatwa na majanga? Huu uadui wa kushindwa kumpa pole kiongozi umeanza lini?

Tatu, chama kinamtishia mgonjwa na kumpangia nani wa kumpa faraja na nani hatakiwi kwenda kumpa faraja. Nani amchangie, wakati huohuo hakijaonyesha kuwa kipo tayari kuwezesha matibabu yake.


Nne, chama kinasema kinaendelea na uchunguzi, sasa kama kinachunguza, kwa nini kinatoa vitisho kwa mgonjwa? Hivi mgonjwa anayetishiwa atatoa ushirikiano kwenye huo uchunguzi? Kinachunguza jambo ambalo kinasema ni 'tuhuma za mtandaoni'.

Tano, kauli za kikatili kama hizi nilizoea kuzisikia wakati wa mwendazake, walipopotea watu tuliambiwa tujikite kwenye maendeleo kwani wapo wanaokwamisha... Kumbuka kauli dhidi ya Ben Saanane, Azory, Kanguye na wengineo wengi.

Mrema amesema: “Nalaani kitendo cha kiongozi wa wanawake kupigwa na wanaume. Huu ni ukatili wa kijinsia na unapaswa kupingwa na kila mtu mstaarabu bila kujali nani katendewa ukatili huo.

“Ukatili huu hauna tofauti na ukatili unaofanywa kwa wanawake wengine nchini, tuungane kuupinga, kuukemea na kutokomeza matendo ya kikatili katika vyama vya siasa na nje ya vyama vya siasa. Idd Mubarak.”


Hoja kwa hoja

Baada ya maswali hayo, kumeibuka mjadala kwa wachangiaji, huku Mrema akiwajibu baadhi yao. Obrieli Aliko amemhoji Mrema kuhusu anachotaka kifanyike iwapo mgonjwa amefanywa mateka wa CCM.

“Kama wewe, bwana Mrema, unajua hospitali anakopatia matibabu, utuambie twende tukamfariji na kumpa pole. Ila kama ni drama zake, atakuwa ameharibu, na wewe utakuwa umejisogeza engo mbaya,” aliandika Aliko.

Mrema alimjibu kuwa mgonjwa yupo Hospitali ya Rufaa Dodoma, na jana Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Dodoma, Aisha Madoga, alimtembelea hapo. Alifafanua kuwa suala la kuwa mateka linawezekana ni kutokana na udhaifu wao kama chama, kwani katika siasa kila kitu ni fursa kwa mshindani wako.

Kupitia majibu ya Mrema, Joseph Maro amemtaka Mrema kukiachia chama suala hilo, kwani chama kinajua kinachopaswa kushughulikiwa.

“Wewe sasa uko nje ya mfumo wa chama, huna taarifa za ndani, na ni ngumu kujua ya ndani. Kwa sasa wewe ni mwanachama kama wengine na unasubiri maelekezo ya chama. Fanya hivyo kwa utulivu maana viongozi wanajua wanafanya nini,” ameandika.

Mrema amejibu hoja hiyo kwa kuandika: “Nimelaani kama mwanachama, au hilo nalo limekatazwa? Chama chetu si cha ‘Zidumu fikra za mwenyekiti’ bali ni chama cha kuhoji. Viongozi watimize wajibu wao na sisi wanachama tutimize wajibu wetu,” ameandika.

Prince Massawe ameandika: “Sisi si wajinga, Mrema. Niliona uhuni huu mapema, ….”

Akijibu hilo, Mrema amesema: “Matendo yake si muhimu kwangu, ila muhimu ni kwamba kafanyiwa tendo la kikatili na chama hakionekani kulaani wala kujitenga na aliyefanya ukatili huo. Kwa nini chama hakikulaani au kutoa pole?”

Joseph Mahonia amemwambia Mrema kuwa kwa sasa hana jipya, huku Mrema akihoji ikiwa kukemea maovu ndani ya chama siku hizi kumeharamishwa. Pia alieleza kuwa ikiwa chama hakiwezi kujitenga na uovu huo, maana yake ni kwamba una baraka za viongozi.

Alisisitiza kuwa demokrasia ni pamoja na kulaani na kupinga maovu ndani na nje ya chama.

Mbali na hayo, baadhi ya watu walipokea ujumbe wake kwa mitazamo tofauti, huku wengine wakishangazwa na yeye kuwa mkosoaji wa kinachofanywa na chama chake.

Gaspar Temba ameandika: “Madaraka yakiondoka upande wako, ndipo watu wanajua una busara kiasi gani, ustahimilivu kiasi gani, ukomavu kiasi gani, na akili kiasi gani. Tumewajua.”

Christian Bwaya aliandika: “Kweli kibao hubadilika! Leo umegeuka mkosoaji wa chama chako hadharani?”

Mrema akijibu hoja hizo amesema: “Kwamba kukemea maovu ndani ya chama siku hizi kumeharamishwa? Kama hatuwezi kujitenga na uovu huu, maana yake una baraka za viongozi? Demokrasia ni pamoja na kulaani na kupinga maovu ndani na nje ya chama.”