Prime
Urembo wa Mateso: Maumivu ya nguo za kubana kwa wanawake

Muktasari:
- Wataalamu wa afya wametoa angalizo kwa wanaovaa nguo za kubana tumbo na kutengeneza shepu. Huku wakieleza matatizo ya kiafya yanayoweza kuwakumba.
Dar es Salaam. Katika sherehe nyingi siku hizi, ni nadra kukutana na wanawake walioacha maumbo yao ya asili yaonekane bila marekebisho.
Uvaaji wa nguo za kubana maarufu kama closet umekuwa mtindo unaopendwa na wengi kwa lengo la kutengeneza shepu na kubana tumbo.
Wanawake wengi wanaoyavaa huonekana wakiwa na maumbo yanayofanana, mikao yao isiyo ya kawaida, na wakati mwingine hata matiti yao yakikaribia kugusa kidevu.
Lakini je, uzuri huu wa muda mfupi una gharama gani? Licha ya mwonekano wa kuvutia, baadhi ya wanawake wanaopendelea mavazi haya wanakiri kupitia maumivu makali, shida ya kupumua, na hata matatizo ya kiafya ya muda mrefu.
Je, urembo huu unalipa au ni mateso yanayovumiliwa kwa muda mfupi?

Haya yote hutokana na aina ya nguo wanazovaa, maarufu ‘closet’ kufanya kazi ya kutengeneza maumbo yao, pale tu zinapovaliwa.
Licha ya kuwa aina hiyo ya mavazi kwa sasa inaonekana kama mkombozi kwa wanawake, wataalamu wa afya wamesema fasheni hiyo inaweza kusababisha athari za kiafya ikiwemo kushindwa kupumua vizuri.
Wamesema uvaaji wa nguo yoyote ya kubana huleta athari kiafya, kutokana na kubanwa kwa baadhi ya ogani katika mwili, hali inayosababisha ukosefu wa oksejeni katika upumuaji, hivyo kumfanya mtu ashindwe kuhema vizuri na kuharibu mfumo mzima wa upumuaji.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji katika Hopsitali ya Aga Khan, Alex Masao anasema aina hiyo ya mavazi humfanya mhusika kupunguza kasi ya upumuaji na hivyo kuyanyima mapafu kutanuka na kusinyaa kila baada ya sekunde mbili, kama ilivyo kawaida.
“Mtu anapovaa vazi hilo ni sawasawa na mtu anayeingiza tumbo ndani. Upumuaji unakuwa hauko sawa, kwani mapafu hayatanuki na kusinyaa kama inavyotakiwa. Hali hii inaweza kuleta athari kwenye ogani,” amesema.
Dk Masao amesema mhusika akikaa kwa muda mrefu katika hali hiyo, inaweza kumleta madhara lakini ikiwa ni muda wa sherehe pekee anajitesa kwa kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Mtaalamu wa fiziolojia ya homoni na mazoezi, Dk Fredrick Mashili amesema aina hizo za nguo hukaza zaidi mafuta, kwani wengi wanaopenda kuzitumia ni wale wenye vitambi.
“Kama amebanwa mpaka anashindwa kupumua, hilo ni tatizo. Lolote linaweza kutokea kwa kuwa huko anaenda kula na kunywa. Nafasi ya kupumua na chakula kuingia hilo linaweza kuzua tatizo lingine la kiafya inategemea na ukaaji wake,” amesema.
Dk Mashili ambaye pia ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS),amesema kinachokazwa ni mafuta na si misuli, hata hivyo alionya kuwa si salama kiafya.
Washonaji nguo waeleza
Akizungumza na Mwananchi, mbunifu wa mavazi ya kike, Upendo Mkonye amesema nguo za closet hutengenezwa kwa kutumia plastiki nyembamba inayowekwa ndani ya nguo katika kipande cha juu, inayoanzia sehemu ya tumbo hadi ya matiti, ili kufanya nguo isijikunje na inapovaliwa iweze kukaza na kutengeneza shepu.

“Nguo za closet zinakuwa kama enzi za zamani, hakukuwa na huduma ya kuweka chuma, mtu akivunjika mguu au kuteguka. Kuna tiba iliyokuwa ikitumika miti inafungwa kwa pembeni na inakazwa ili mguu usijikunje na uweze kupona haraka.
“Hivyo katika hizi nguo, plastiki zinakuwa imara ili kufanya nguo ikae mahala pake, hata wakati wa kuvaa ikikazwa. Inasaidia kubana tumbo na kutengeneza mwonekano wa kuvutia,” amesema Upendo.
Pia ameeleza namna ambavyo nguo hizo huvaliwa kwa kuvutwa kamba maalumu, inayokuwa mgongoni au kwa upande wa mbele.
“Mtu anapovaa hizi nguo hukazwa, kuna wakati hata kuhema au kukaa inakuwa kwa shida vilevile kwa sababu mtindo hupendeza zaidi ukiwa umesimama kuliko kukaa,” ameongeza Upendo.
Naye fundi wa nguo za kike na za kiume, Sinza jijini Dar es Salaam, Ally Suleiman amesema wateja wake wengi hasa wa nguo za sherehe mbalimbali hutaka nguo za closet ili kuficha matumbo na nyama za pembeni kwenye kiuno, kwa kutengeneza mtindo wa aina ya samaki nguva.
Wapo baadhi hutaka waongezewe hadi sponji ndani ya nguo, ili waonekane wana makalio makubwa na hipsi. Pia anasema licha ya gharama ya utengenezaji wa nguo hizi kuwa juu, ongezeko la wavaaji lipo kwa kiwango cha juu.
“Wanawake wengi wanaokuja kushona hizi nguo wana vitambi, wanazipenda ili waonekane wana flat tummy, yaani hawana matumbo na wana shepu iliyochongeka, jinsi ambavyo huwa tunawabana wakati wa kuwavalisha, sina uhakika kama damu inapita vizuri,” ameeleza fundi Ally.
Hali ilivyo kwa wavaaji
Mkazi wa Sinza Mugabe, Paulinah Jacob, ameeleza masaibu aliyoyapata baada ya kuhudhuria sherehe akiwa amevaa nguo ya kubana maarufu kama "closet."
Alipata maumivu makali sehemu za tumbo na mgongo, hali iliyomfanya ashindwe hata kula chakula cha kutosha. Siku iliyofuata, alihisi maumivu ya mwili na alama za damu kuvilia kiunoni, hali iliyomchukua wiki nzima kupona.
"Kiukweli, hizi nguo zinaonekana kupendeza lakini zina machungu mengi. Nilipata maumivu makali hadi nikashindwa kufurahia sherehe," anasema Paulinah.
Mwamvi Christophel, naye anasimulia jinsi alivyojaribu kuvaa nguo hiyo lakini akaishia kuivua kutokana na maumivu kwenye tumbo na maziwa, pamoja na shida ya kupumua.
"Licha ya kusifiwa nimependeza, mimi mwenyewe nilikuwa najua machungu niliyokuwa napitia," anasema.
Mzigo kwa Wanaume
Mohamed Jumanne, mkazi wa Tabata Kimanga, anaeleza kuwa mke wake ni mvaaji wa nguo hizi, na gharama zake ni kubwa, kati ya Sh100, 000 hadi Sh150, 000.

Anasema mavazi haya husababisha maumivu makali kwa mke wake, hadi wakati mwingine anashindwa hata kusimama mwenyewe. "Wanawake wanapendeza, lakini gharama na mateso ni makubwa, hata sisi wanaume tunaathirika," anasema Mohamed.
Tatizo la kisaikolojia
Mratibu wa Afya ya Akili wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Dk Pascal Kang’iria, anaeleza kuwa uvaaji wa nguo hizi ni suala la kisaikolojia.

Watu huvaa ili kubadilisha mwonekano wao kwa sababu ya kutoridhika na maumbo yao ya asili na hali hii husababisha uraibu wa mavazi ya kubana, shida ya kupumua, na madhara kwa viungo vya ndani.
Dk Kang’iria anashauri kujikubali jinsi ulivyo na kufanya mazoezi badala ya kutegemea mavazi ya kubana kwa mwonekano wa kuvutia. "Mazoezi ni njia salama zaidi kuliko kutumia njia fupi zenye athari mbaya kiafya," anasema.