Prime
Ukomo, elimu nafasi ya ubunge mjadala mzito

Moshi/Dar. Mjadala wa ukomo kwa nafasi ya ubunge wa jimbo, umeanza kupamba moto huku baadhi ya wasomi na wananchi wakiikumbuka Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Joseph Warioba iliyoweka ukomo wa miaka 15 katika nafasi hiyo.
Wanaochagiza uwepo wa ukomo, wanaenda mbali na kutaka pia kuwepo kwa kiwango cha chini cha elimu kutokana na kiwango cha uelewa kupanda nchini, kulinganisha na miaka 48 iliyopita wakati Katiba ikitungwa mwaka 1977.
Akitoa maoni juu ya hoja hiyo, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi anasema ukomo ni njia mojawapo ya kukomesha udikteta wa wachache dhidi ya wengi na kuzuia umiliki wa madaraka kwa muda mrefu.
Wenye maoni hayo, wanaona katika mazingira ya chaguzi za Tanzania, upo uwezekano wa Mbunge kuendelea kuongoza kwa kipindi kirefu ama kwa kukubalika, kutumia rushwa au njia zingine za hila kubaki madarakani.
Justina Aloyce ambaye ni mjasiriamali anayeuza bidhaa za mitumba mjini Moshi, anasema ukomo katika nafasi ya ubunge ni muhimu ili kutoa nafasi kwa damu changa kuonyesha uwezo wao katika uongozi wa kisiasa.
“Lakini mimi naona bado ni kichekesho. Yaani unamchagua mbunge kwa sifa ya kujua kusoma na kuandika halafu anaenda kutunga sheria. Kweli? Hivi Tanzania hii kwa mageuzi makubwa ya elimu tunahitaji mtu mwenye sifa hiyo?” amehoji.
Mwananchi huyo anasema kwa mazingira ya sasa, angetamani kuona sifa mojawapo ya udiwani iwe mtu aliyefikia elimu ya sekondari ya kidato cha nne na ubunge astashahada au Shahada na ukomo vipindi vitatu.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi hawakubaliani na suala hilo la ukomo katika nafasi ya ubunge kama ilivyo kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakitaka wanaochagiza ukomo watofautishe nafasi za uwakilishi na kiutawala.
Mjadala huo unakuja mwezi mmoja tangu Chama cha Mapinduzi (CCM), kipitishe ukomo wa miaka 10 kwa viti maalum katika nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani, lakini mabadiliko hayo yataanza kutumika uchaguzi mkuu wa 2030.
Ukiacha CCM, uongozi mpya wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwenyekiti wake, Tundu Lissu na makamu wake, John Heche ndio wa kwanza kuibua hoja ya uwepo wa ukomo katika nafasi ya viti maalum.
Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 40(2), imeweka ukomo wa vipindi viwili vya urais lakini katika nafasi ya ubunge wa majimbo na wale wa viti maalum, mtu anaweza kushikilia nafasi hiyo ilimradi anakubalika na kuchaguliwa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Katiba, pamoja na sifa nyingine, ili mtu achaguliwe kuwa Rais, anapaswa kuwa na sifa za kuchaguliwa mbunge zinazopatikana ibara ya 67(1)(a) ambazo ni raia wa Tanzania na anajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza.
Lakini rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014, ilipendekeza Mbunge lazima ajue kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili na awe na elimu isiyopungua ya kidato cha nne.
Hata hivyo, wajumbe wa Bunge hilo ambao wengi walitoka CCM, walikataa mapendekezo hayo na kuondoa kigezo cha elimu katika nafasi ya ubunge na kubakiza moja ya sifa ni kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.
Hata hivyo, akizungumza Mwananchi, wakili Mwabukusi alisema suala la ukomo wa madaraka kwa wabunge wa majimbo na madiwani imejijenga katika msingi wa demokrasia, utawala bora na uwakilishi.
“Ukomo ni njia mojawapo ya kukomesha udikteta wa wachache dhidi ya wengi. Ni njia mojawapo ya kuzuia kujenga ukiritimba na umiliki wa madaraka kwa kikundi cha watu wachache baada ya kupata access katika mfumo wa kiutawala,”aamesema Mwabukusi.
“Kiongozi anaweza kutumia nafasi yake katika uwakilishi wa Umma kuimarisha nguvu zake binafsi au watu fulani katika tabaka husika na kusahau uwajibikaji kwa wananchi lakini kuingiza watu wapya ni kuchochea mawazo mapya na mabadiliko.
“Ukomo unaweza kuleta mawazo mapya na nguvu mpya za kuleta maendeleo. Viongozi wanaobakia madarakani kwa muda mrefu mara nyingi wanakuwa na mtazamo wa kizamani na hupunguza kasi ya maendeleo,”alieleza Mwabukusi.
“Hii hutokana na kuamini kuwa wana uzoefu mkubwa na ni mabingwa wa siasa. Hii hupelekea kukuza kujivuna na kuondoa uwajibikaji kwa Umma. Lakini ukomo utazuia uzembe,wizi,Ufisadi na matumizi mabaya ya Madaraka,”alisisitiza.
“Wakati mwingine, wabunge au madiwani wanapokuwa madarakani kwa muda mrefu, wanaweza kuanza kutumia vibaya ofisi zao kwa maslahi binafsi. Sio wote nasema baadhi. Ukomo unaweza kupunguza hatari ya tabia hizi,”alisema.
Lakini pia amesema kuimarisha demokrasia ya uwakilishi ni muhimu kulinda haki ya msingi ya wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka kwani itakuwa haina maana kuweka ukomo kama madiwani na wabunge hawapatikani kwa haki.
Wadau wa siasa wafunguka
Mchambuzi wa siasa, Conrad Kabewa akizungumza na Mwananchi amesema nafasi ya Rais ni muhimu kuweka ukomo kama katiba inavyotaka, kwa sababu ni nafasi ya kiutawala na ni muhimu kuwa na damu mpya, mawazo mapya mitazamo mipya katika kuiongoza nchi.
“Udiwani na ubunge, hizi ni nafasi za kuwawakilisha watu katika maeneo maalum yaliyotambuliwa kwa mujibu wa sheria. Kama chaguzi zikiwa za wazi, za haki na huru kabisa hakuna sababu ya kuweka ukomo,”alisema mchambuzi huyo.
“Watu wakimtaka mtu awawakilishe na anafanya vizuri waachwe wamchague tu. Kinachotakiwa hapo ni utaratibu wa wazi wa namna ya kuwaondoa wawakilishi ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao bila kusubiri muhula uishe,” amesema Kabewa.
Amesema kwa hali ilivyo sasa, mbunge au diwani akichaguliwa anajua kwamba yupo pale kwa miaka mitano bila kuguswa.
“Sasa hata asipotimiza wajibu wake, wapiga kura wanamwangalia tu hadi miaka mitano iishe. Hii si sawa,”alisisitiza Kabewa.
Amesema kuna haja ya kuwa na utaratibu wa kura ya maoni pale itakapobainika mbunge huyo ameshindwa kuwajibika wakati wowote.
“Viti maalum ni tofauti kwa sababu wale sio wawakilishi wa majimbo kwa hiyo huwezi kuwapima utendaji wao kirahisi. Hawa wanaweza kuwekewa vipindi kama viongozi wa kiutawala alivyo Rais miaka 10 tu. Hiyo sawa ila sio wawakilishi,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kilimanjaro, Awadhi Lema amesema kufanya mabadiliko ya mara kwa mara katika kanuni ni jambo jema lakini kumchagua mtu inatokana na wanao mchagua.
“Mtu anaweza kuchaguliwa zaidi ya vipindi viwili au vitatu au hata zaidi kulingana na uwezo wake au uwajibikaji wake katika jamii. Ikiwa utabadilisha katiba kwa sababu tu ya kumzuia mtua asikae kwa vipindi vingi siyo sahihi kabisa,”amesema.
“Kila mgombea anachaguliwa na wananchi, kama angekuwa hafai angekataliwa na wananchi na siyo kurekebisha kanuni au katiba kumkataa mtu huyo. Kwahiyo sioni kama kuna haja ya kuweka kikomo sababu wananchi ndio waamuzi wakuu,” ameongeza.
Hata hivyo, Katibu huyo wa Bakwata aliunga mkono uwepo wa ukomo katika nafasi ya viti maalumu akisema ni vema wakawekewa ukomo ili wakapambane na wanachama wenzao kwenye majimbo baada ya kupata uzoefu wa miaka 10.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu anasema wanaunga mkono maoni ya ukomo wa ubunge ambayo ndiyo yalikuwa maoni ya Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba.
Amesema wanaamini miaka 10 inatosha kuwakilisha wananchi na kutoa fursa kwa wengine huku akisisitiza kuwa suala la ukomo kwa ubunge na udiwani ni jambo linalojadilika.
Hussein Mfinanga mtaalamu wa Kompyuta, anasema; “Tanzania hivi sasa tunaambiwa tuna shule za sekondari 5,280 na matokeo ya kidato cha nne 2024 kuna wanafunzi 477,262 walifaulu kati ya waliofanya mitihani 516,695 na tumeambiwa mwaka huu darasa la saba wote wameenda sekondari.”
“Sasa katika mazingira haya, kwa nini tunaogopa kuweka kiwango cha elimu kwenye nafasi za kisiasa. Hii ni dunia ya kidigitali na zama za utandawazi hakuhitaji ujanja ujanja. Tuna vijana milioni moja wanahitimu vyuo vikuu na vyuo vya kati.”
Mtaalamu huyo anasema Tanzania ya leo sio ile ya wakati inapata uhuru mwaka 1961, idadi ya wasomi walikuwa wachache, lakini sasa hivi kuna shule ya sekondari kila kata, kuna vyuo vikuu zaidi ya 60 na vyuo vikuu vishiriki zaidi ya 16.
Wakili Dominic Ndunguru amesema jambo hilo linaweza kuwa na matokeo chanya na hasi. Kwa baadhi ya watu wanaweza kutooana haja ya kuwatumikia wananchi kwa sababu watajua muda wao wa ubunge unakwisha huku wanaofanya kazi vizuri wanaweza kukosa nafasi ya kuwatumikia vizuri wananchi.
“Ifanyiwe utafiti tunaweza kuangalia matokeo yake pia kujifunza kutoka nchi nyingine kuona miaka michache faida yake na miaka mingi faida yake ni ipi ili sheria inapotungwa iguse pande zote kuanzia nafasi ya madiwani na wabunge,” amesema Ndunguru.
Mratibu wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa, aliunga mkono hoja ya ukomo kwenye nafasi ya ubunge lakini akasema hilo liwe kwenye Katiba ya nchi na lisiishie kwenye vyama vya siasa.
“Ukomo Viti maalum ni haki kabisa. Miaka 10 inatosha. Inapokuja kwenye suala la ukomo kwenye wabunge wa majimbo, nadhani na yenyewe inaweza kuangaliwa kwa kuwa na ukomo wake lakini isiwe kwa miaka 10 inaweza ikawa miaka 15, atoe nafasi kwa mtu mwingine,” amesema.