Nyerere aenziwa, wafungwa 4,887 wapata msamaha

Muktasari:
- Ni katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Dar es Salaam. Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua kitabu cha Safari ya Mwalimu Nyerere huku Serikali ikieleza ipo mbioni kuandaa vitabu vingine vya aina hiyo kumuhusu Amani Abeid Karume, ambaye ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
Mbali na hilo ametunuku nishani za Muungano kama ishara ya kutambua utumishi na mchango wa waliotunukiwa katika ujenzi wa Taifa na katika kudumisha Muungano.
Rais katika maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu yamefanyika katika ngazi ya mikoa, pia ametoa msamaha kwa wafungwa 4,887.
Rais Samia amesema katika kitabu alichozindua, watu wataona namna ambavyo hayati Julius Nyerere alivyokuwa akibeba kamera shingoni na alipenda kuitumia kupata kumbukumbu za maisha ya kawaida ya wananchi.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Madaraka Nyerere Kitabu cha “Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Photographic Journey” mara baada ya uzinduzi uliofanyika leo Jumamosi Aprili 26, 2025 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Uzinduzi huo ameufanya leo Jumamosi Aprili 26, 2025 Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma ambako pia alitunuku nishani ya kumbumbuku ya Muungano daraja la pili na la tatu kwa viongozi mbalimbali.
Kuhusu kitabu
“Kitabu hiki, pia kimemuenzi Mwalimu (Nyerere) kupitia kile alichokipenda kufanya, pamoja na kueleza historia yake kitabu hiki ni sehemu ya historia ya nchi na Muungano wenyewe,” amesema.
Kutokana na sababu hizo, amesema hakusita kuandika dibaji na maneno ya mwisho ya kitabu hicho, alipoombwa kufanya hivyo.
Amesema pia hakusita kutoa msukumo kiandikwe, kichapishwe na kukigawa.
“Nimefurahi imewezekana kukizindua leo, siku yenye mnasaba na maudhui ya kitabu hiki, sambamba na utoaji wa nishani kwa viongozi waliotumikia vema Muungano wetu,” amesema.
Amesema kitabu hicho kinatumia picha na maelezo ya kina ya simulizi na historia ya Mwalimu Nyerere kuanzia kwenye milima ya Kijiji cha Mwitongo (Butiama-Mara), takribani miaka 103 iliyopita.

Rais Samia amesema kitabu hicho chenye kurasa 362 kinapitisha hatua mbalimbali za safari ya Nyerere, vikwazo alivyovivuka na mafunzo aliyoyapata na kujenga mwelekeo wa maisha yake kama kiongozi.
“Kama nilivyoandika katika dibaji Mwalimu alikuwa ni mwanafalsa ya kujitegemea iliyojengwa katika misingi ya haki, utu, mshikamano wa kitaifa na maendeleo jumuishi. Kwa sehemu kubwa falsafa hiyo imeendelea kwa msingi wa uongozi wa nchi yetu tangu enzi hizo hadi sasa,” amesema.
Amesema Nyerere alisimamia kwa uthabiti mkubwa yale aliyoyaamini na kitabu hicho kinakumbusha namna alivyopambana kujenga Taifa jumuishi, lisilo la ubaguzi wa rangi, dini, ukabila au majimbo.
“Kutokana na makuzi yake, Mwalimu aliamini na kuonyesha kwa vitendo kwamba watu tofauti wanaweza kuishi pamoja na kufanya kazi kwa lengo moja,” amesema.
Kitabu hicho amesema kinaeleza mchango wa wanawake katika safari ya Mwalimu Nyerere akiwemo mama yake mzazi, Christina Mgaya ambaye alimfunza namna ya kujituma na kutumikia jamii kwa uadilifu.
Amesema kitabu kitawapa fursa hata wale wananchi wavivu kusoma, watajifunza historia kupitia njia ya picha, pia kinaeleza kuhusu uhusiano kati ya Nyerere na viongozi mbalimbali waliobahatika kufanya kazi naye.
Ameagiza kitabu hicho, kitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ili watu wengine wapate fursa ya kukisoma, lakini wahakikishe kinapatikana kwa njia ya kidijitali ili kurahisisha usomaji wa watu wengi zaidi duniani.
“Serikali ipo tayari kuendelea kuwapa nguvu ili haya yatimie,” amesema.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimkabidhi mwakilishi wa familia ya Hayati Edward Lowassa nishani ya kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili kwenye hafla iliyofanyika leo Jumamosi Aprili 26, 2025 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika uzinduzi huo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hatua hiyo ni kutambua na kuthamini mchango wa Julius Nyerere katika kuasisi Muungano ambao ndio msingi mkuu wa umoja, amani na maendeleo ya Tanzania.
“Hayati Nyerere aliamua kutafsiri kwa vitendo dhana ya umoja wa Afrika kwa wazo lake kumtaka marehemu Karume (Abeid Amani –Rais wa Kwanza wa Zanzibar) kuungania Zanzibar na Tanganyika ili kuaisisi Tanzania,” amesema.
Dk Mwinyi amesema: “Kupitia kitabu kinachozinduliwa leo kizazi kipya baada ya Muungano watapata fursa ya kujifunza zaidi malengo na faida ya Muungano wetu uliotimiza miaka 61 ukiwa na mafanikio makubwa.”
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kukosekana kitabu cha kusisimua kupitia picha na maisha, ndiyo sababu iliyofanya kuandikwa kitabu cha Julius Nyerere ili kuenzi mchango wa mwasisi huyo wa Taifa.
“Kitabu hiki si tu mkusanyiko wa picha bali ni alama ya heshima ya Baba wa Taifa (Nyerere) tukienzi jitihada zake na wenzake, Sheikh Amani Abeid Karume, Rashid Kawawa, Thabit Kombo Jecha waliokuwa na maono ya kujenga Taifa moja, lenye umoja, amani na mshikamano.
“Taifa lenye kujali utu na heshima ya binadamu, usawa kwa watu wote na linalohimiza maendeleo na ustawi wa wananchi wa Tanzania,” amesema.
Amesema wazo la kuandika na kuchapisha kitabu hicho, lilianza mwaka 2014, baada ya kubaini hakuna chenye kusimulia kupitia picha maisha na mchango wa Baba wa Taifa Nyerere kwa Taifa, Afrika na dunia.
“Pengo hilo ndilo lililotusukuma kuandaa na kuandika kitabu hiki ili kuzifanya picha hizo kuelekeweka na zimeendana na simulizi fupi zinazoipa pumzi na uhai ili kumfanya msomaji kuzielewa ili kitabu hiki, kuwa na mvuto wa kipekee,” amesema.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimtunuku nishani ya kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kwenye hafla iliyofanyika leo Jumamosi Aprili 26, 2025 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Amesema lengo la kitabu ni kuhifadhi kumbumbu kwa vizazi vijavyo ili kumuona Baba wa Taifa kwa picha na kumfahamu kiwa simulizi zilizosheheni ili kuwa sehemu ya urithi.
Amesema wazo la kuandika kitabu lilipelekwa kwake kwa mara ya kwanza mwaka 2014 akiwa na Japhet Jafech, katika mazungumzo walikubaliana kuandika kitabu cha kwanza wakishirikiana na Dk John Jingu, Profesa Alexander Makulilo na Dk Richard Sambaiga.
“Baada ya hapo ilifuata kazi ya kutafuta picha za viwango na ubora wa hali juu kutoka maktaba, makavazi na taasisi mbalimbali za ndani watu binafsi dunia. Baada ya kukamilisha rasimu ya kwanza Iilichukua muda mrefu kuendelea na uandishi wa kitabu,” amesema.
Profesa Kabudi amesema Rais Samia ndiye aliyeweka msukumo mpya wa kukamilisha uandishi wa kitabu hicho, baada ya kukaa kwa miaka 10 bila kumalizika.
Amesema wapo mbioni kuandaa vitabu vingine vya aina hiyo kumuhusu Amani Abeid Karume, ambaye ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
Kutunuku nishani
Rais Samia amewatunuku nishani za Muungano viongozi wastaafu akiwemo Rais wa zamani wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Wengine ni Balozi Seif Ali Idd (Makamu wa Pili mstaafu Zanzibar), Balozi John Kijazi, Waziri Mkuu wa mstaafu, hayati Edward Lowassa, Pandu Ameir Kificho (Spika mstaafu wa Baraza la Wawakilishi -Zanzibar), Philip Mangula (Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Mizengo Pinda (Waziri Mkuu mstaafu).

Rais Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimtunuku nishani ya kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili kwa Makamu wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk Mohamed Ali Shein kwenye hafla iliyofanyika leo Jumamosi Aprili 26, 2025 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Rais Samia pia amemtunuku nishani hiyo Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.
Aprili 5, 2025 alipozindua majengo matatu ya makao makuu ya Mahakama Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama na nyumba za majaji zilizojengwa katika eneo la Iyumbu, jijini Dodoma Rais Samia alisema Jaji Mkuu huyo amefanya mageuzi makubwa ya Mahakama.
Alisema pamoja na msukumo wa Serikali, lakini mageuzi ya fikra, kusimamia na kuleta mageuzi yaliyopo ni mabadiliko makubwa ndani ya mhimili huo.
“Sasa Katibu Mkuu Kiongozi (Dk Moses Kusiluka) nimekuona uko hapa, umenipangia kutoa nishani kwenye sherehe za Muungano, naomba uniongezee nishani moja ya Jaji Mkuu wa Tanzania,” aliagiza Rais Samia.
Msamaha kwa wafungwa
Katika maadhimisho hayo, kupitia taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Rais Samia ametoa msamaha kwa 4,887 waliokidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafungwa wote watakaopunguziwa sehemu ya vifungo vyao ni wale waliotumikia angalau miaka miwili gerezani hadi kufikia Machi 2, 2025.
Msamaha huo umewahusisha pia wafungwa waliokuwa wakikabiliwa na changamoto maalumu kama vile wanawake wenye watoto wachanga gerezani na wafungwa wenye ulemavu wa akili.
Hata hivyo, msamaha huo haujawahusu wafungwa waliopatikana na hatia ya makosa makubwa ikiwemo uhujumu uchumi, unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji ya watoto wachanga, ugaidi, ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu wa kimtandao.
Wafungwa waliopata msamaha wa awali kutoka kwa Rais lakini wakarejea kufanya makosa au kuvunja masharti ya gerezani nao hawajapata msamaha huu mpya.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kati ya wafungwa waliopata msamaha, wafungwa 42 wataachiwa huru leo Aprili 26, huku wengine 4,845 wanabaki gerezani kumaliza sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu.