Profesa Kabudi aeleza sababu za kuandikwa kitabu cha Nyerere

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi.
Muktasari:
- Profesa Palamagamba Kabudi amesema kitabu cha Julius Nyerere kiliandikwa ili kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, kutokana na kukosekana kitabu cha kusisimulia maisha yake kupitia picha.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kukosekana kitabu cha kusisimua kupitia picha na maisha, ndiyo sababu iliyofanya kuandikwa kitabu cha Julius Nyerere ili kuenzi mchango wa mwasisi huyo wa Taifa.
Profesa Kabudi ameeleza hayo leo Jumamosi, Aprili 26, 2025, wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Mwalimu Julius Nyerere chenye simulizi na picha, shughuli iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Uzinduzi uliofanyika Ikulu Chamwino, jijini Dodoma, ulikwenda sambamba na Rais Samia Suluhu Hassan kuwavisha nishani ya kumbukumbu ya Muungano daraja la pili na tatu, viongozi mbalimbali wastaafu, akiwemo Rais wa zamani wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
"Kitabu hiki si tu mkusanyiko wa picha, bali ni alama ya heshima ya Baba wa Taifa (Nyerere) kikienzi jitihada zake na wenzake, Sheikh Aman Abeid Karume, Rashid Kawawa, Thabit Kombo Jecha waliokuwa na maono ya kujenga Taifa moja, lenye umoja, amani na mshikamano,” amesema Kabudi.
"Taifa lenye kujali utu na heshima ya binadamu, usawa kwa watu wote na linaloimiza maendeleo na ustawi wa wananchi wa Tanzania," amesema Profesa Kabudi.
Amesema wazo la kuandika na kuchapisha kitabu hicho lilianza mwaka 2014, baada ya kubaini hakuna cha mezani chenye kusimulia kupitia picha maisha na mchango wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kwa Taifa letu, Afrika na Ulimwengu.
"Pengo hilo ndilo lililotusukuma kuandaa na kuandika kitabu hiki ili kuzifanya picha hizo kueleweka, na zimeendana na simulizi fupi zinazoipa pumzi na uhai ili kumfanya msomaji kuzielewa, ili kitabu hiki kuwa na mvuto wa kipekee," amesema Profesa Kabudi.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, kitabu hicho hakielezei maisha na mchango wa Nyerere tu bali kinaelezea historia na mapito ya Tanzania.
"Lengo la kitabu hicho ni kuhifadhi kumbukumbu kwa vizazi vijavyo, ili kumuona Baba wa Taifa kwa picha na kumfahamu kwa simulizi zilizosheheni katika kitabu hicho, ili kuwa sehemu ya urithi," amesema.
Wazo lilipoanza
Kabudi amesema wazo la kuandika kitabu lilipelekwa kwake kwa mara ya kwanza mwaka 2014 akiwa na Japhet Jafech, katika mazungumzo yao walikubaliana kuandika kitabu cha kwanza wakishirikiana na Dk John Jingu, Profesa Alexander Makulilo na Dk Richard Sambaiga.
"Baada ya hapo ilifuata kazi ya kutafuta picha za viwango na ubora wa hali ya juu kutoka maktaba, makavazi na taasisi mbalimbali za ndani na watu binafsi duniani. Baada ya kukamilisha rasimu ya kwanza, ilichukua muda mrefu kuendelea na uandishi wa kitabu," amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, Rais Samia ndiye aliyeweka msukumo mpya wa kukamilisha uandishi wa kitabu hicho, baada ya kukaa kwa miaka 10 bila kumalizika.
Waziri Kabudi amesema hawajaishia hapo, bali wapo mbioni kuandaa vitabu vingine vya aina hiyo vitakavyomhusu Aman Abeid Karume ambaye ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar.