Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni mwendo wa kudai haki mwaka 2024

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Dodoma/Dar. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai Serikali haijasikiliza maoni ya wadau kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023.

Dodoma/Dar. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai Serikali haijasikiliza maoni ya wadau kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipokuwa akizindua ‘vuguvugu la kudai haki Tanzania 2024’ sambamba na kutoa salamu za mwaka mpya za chama hicho.

“Kamati Kuu ya Chadema ilifanya mkutano kwa njia ya kidijitali Januari 8, 2024 na kuzungumzia mambo mawili mahususi. Miswaada iliyowasilishwa bungeni na ugumu wa maisha…” alisema Mbowe.

Hata hivyo, alidai Katibu Mkuu wao, John Mnyika alikataliwa kutoa maoni kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.

“Katibu Mkuu wa chama aliongoza jopo la chama lililowasilisha maoni ya msimamo wa chama mbele ya kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.

Katibu alifanya hivyo ila alikataliwa kusoma mbele ya kamati maoni yetu ya jumla kuhusu miswada hiyo na kutakiwa kusoma uchambuzi wa vifungu kwa vifungu, jambo ambalo linaonyesha tayari kamati imeshafanya uamuzi na ndio maana haitaki kusikiliza maoni ambayo yako nje ya vifungu husika ya muswada,” alidai Mbowe.

Hata hivyo, siku ya kwanza ya utoaji maoni ya Janurari 6, 2024, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Dk Joseph Mhagama aliwaongoza washiriki waliofika mbele ya kamati hiyo kutoa maoni na kueleza kwamba jukumu lao ni kuisaidia kamati namna bora ya utungaji wa sheria.

Dk Mhagama aliwaelekeza watoa maoni ya vyama vya siasa na asasi za kiraia, kwa kuwa wao wana wataalamu mbalimbali, ikiwamo wanasheria.

Aliwataka maoni yao yajielekeze kuisaidia kamati kwa kueleza mambo matatu kwenye vifungu husika kwamba, kifungu kifutwe na mbadala wake kiwekwe kipya, kifungu kiboreshwe na mbadala wa uboreshaji na kifungu kibadilishwe na mbadala wa mabadiliko hayo.

Mwenyekiti pia aliwaeleza watoa maoni ambao ni watu binafsi waliokuwa 376 waruhusiwekutoa maoni ya jumla kwa kuwa hawana wataalamu wa kufanya uchambuzi wa kifungu kwa kifungu, tofauti na vyama vya siasa na asasi za kiraia ambao ni wadau wakubwa wa kuishauri.

Dk Mhagama akiwa na wajumbe wake ambao pia walishiriki katika kutoa elimu ya namna ya kupokea maoni kwa lengo la kuwarahisishia kazi, aliwaelekeza watoa maoni kujielekeza kwenye miswada na si vinginevyo.

Maelekezo ya Dk Mhagama yalilenga kuokoa muda na wahusika kutakiwa kuwasilisha maoni yao kwa maandishi. Vyama vya siasa vilipewa muda wa dakika 20, asasi za kiraia dakika 10 na watu binafsi dakika tano.

Alichosema Mbowe

Mbowe pia kwenye hotuba yake jana aliyoitoa mbele ya wanachama katika makao makuu mapya ya chama hicho yaliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, alitoa hoja kwamba maoni ya wadau mbalimbali, yakiwamo ya Chadema yalikataliwa na Serikali na hivyo kutangaza maandamano ya nchi nzima.

“Kwa kuwa mapendekezo yetu yote yalionekana kukataliwa, chama kinatangaza maandamano ya amani ya kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendelezo ya wadau mbalimbali wa uchaguzi nchini ambayo yataanza Dar es Salaam tarehe 24 mwezi wa kwanza mwaka 2024 siku ya Jumatano mpaka hapo Serikali itakapoondoa miswada hiyo na kusikiliza na kuheshimu maoni ya wadau,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, saa chache baadaye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alitangaza kuwa vyombo vya dola vitakuwa na shughuli ya usafi katika wilaya zote za mkoa kuanzia Januari 23 hadi 24.

Chadema na maoni

Siku ya kwanza, kamati ya Bunge ilipoanza kupokea maoni, Chadema kilicho ongozwa na katibu wa chama hicho Kanda ya Kati, Emmanuel Masonga alifika mbele ya kamati na kutamka anamwakilisha Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kutoa maoni ya chama.

Masonga alisema suala la mgombea pekee kupigiwa kura ya ndiyo au hapana, ni vema kiongezwe kifungu ambacho kitasema; ‘atangazwe kushinda kwa zaidi ya asilimia 50.

Pia, alisema sheria iweke wazi kuhusu uundaji wa majimbo kwa sababu uzoefu unaonyesha majimbo huundwa kwa sababu za kisiasa badala ya uhitaji wa wananchi wa eneo husika.

Uwasilishaji wa Masonga wa kifungu kwa kifungu ulipongezwa na Dk Mhagama, aliyevitaka vyama vingine na asasi za kiraia kuiga mtiririko huo.

Pia, siku ya pili ya utoaji wa maoni mbele ya kamati ya Bunge, Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) lilitoa maoni yake likitaka matokeo ya urais katika majimbo ya uchaguzi yatangazwe kwenye gazeti la Serikali ndani ya mwezi mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu.

Bawacha kwenye utoaji wa maoni iliwakilishwa na wajumbe wawili ambao ni Susan Lyimo ambaye ni Mwenyekiti wake na Makamu Mwenyekiti wa Bawacha, Sharifa Suleiman.

Susan Lyimo katika utoaji wake wa maoni alitumia dakika 25 badala ya dakika 20 za vyama vya siasa na alipotaka mwenzake, Sharifa Suleiman naye atoe maoni, aliambiwa dakika zao zimekwisha.

Hata hivyo, kamati iliwaongeza dakika tano na Sharifa akatoa maoni na kuifanya Chadema kupata dakika 30 badala ya dakika 20.

Akitoa maoni ya Bawacha, Susan Lyimo alisema hadi sasa matokeo ya urais ya majimbo hayajatangazwa kwenye gazeti la Serikali.

“Niko tayari kusahihishwa hapa, matokeo ya urais kwenye majimbo hadi sasa hayajawekwa kwenye gazeti la Serikali. Sisi Bawacha tunapendekeza matokeo ya kura za urais kwa ngazi ya majimbo zitangazwe kwenye gazeti la Serikali ndani ya mwezi mmoja,” alisema.

Lyimo pia alizungumzia suala la wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi kwamba siyo sahihi, kwa kuwa ni watumishi wa umma na wamekuwa wakisimamia masilahi ya aliowateua.

“Mfano, Rais Magufi (John) ambaye amefariki dunia aliwahi kutamka kwa kuwaeleza wakurugenzi kwamba hawezi kuwalipa mshahara waje kumtangaza mgombea wa upinza ameshinda,” alisema Lyimo.

Pia, alisema wakurugenzi wako chini ya Waziri wa Wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi) na ndio wanawajibika huko na si kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema sheria inaelekeza mgombea akienguliwa na mkurugenzi akate rufaa kwa mkurugenzi wa uchaguzi wa Nec, lakini aliongeza kuna waliokata rufaa na mkurugenzi wa Nec akawarejesha, lakini mkurugenzi wa halmashauri aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi akakataa.

Ilichokisema TEC, Bakwata

Kuhusu kauli ya Mbowe kwamba maoni ya wadau mbalimbali yamekataliwa na Serikali na sasa wataitisha maandamano kuishinikiza Serikali ipokee maoni ya wadau, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema taasisi yao inaangalia utaratibu uliowekwa na Serikali wa kukusanya maoni ya miswada hiyo, uliohusisha watu wengi na wao walipeleka maoni yao.

“Kusema mrejesho umepatikana, bado hadi pale Bunge litakaposema tunapitisha hiki au hatupitishi hiki, msimamo wetu tunasubiri mhimili huo utakapojadili miswada ile ili kuona kama maoni yetu yamezingatiwa au la.

“Hivi siwezi kuzisemea taasisi zingine zikiwemo za kiraia au vyama vya siasa, kwa sababu kila taasisi ina namna zake za kupambania na kusimamia kile wanachokiamini, siwezi kuwasemea au kuwashauri Chadema kwa hatua hii maana TEC imeshatimiza wajibu wake kama taasisi ya kidini,” alisema Padri Kitima.

Alisema kwa sasa wanachosubiri ni kuona sheria gani itatengenezwa na wao watatoa maoni au ushauri, lakini kwa sasa hawawezi kwa sababu Serikali bado haijatoa mrejesho wa maoni ya wadau.
“Binafsi hatuwezi kutoa ushauri au maoni yoyote kwa taasisi nyingine, kwa sababu viongozi wangu wa TEC wanasubiri mrejesho,” alisema.

Wakati Kitima akisema hayo, Mbowe alisema kamati kuu ya chama hicho imeitisha maandamano ya nchi nzima kuanzia Januari 24 yatakayoanzia Dar es Salaam wakilenga kuishinikiza Serikali ikubali kupokea maoni ya wadau.

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma alipozungumzia hilo alisema maandamano sio njia sahihi ya kutengeneza mwafaka wa jambo fulani.
Hata hivyo, Mruma alisema hawezi kuzungumza kwa undani kuhusu kauli za Mbowe kwa sababu hajamsikiliza.

“Lakini ninachojua tupo katika kipindi cha kukusanya maoni kuhusu miswada mitatu, viongozi wa dini na taasisi nyingine wametoa maoni yao, bado tunahisi nafasi yetu ipo juu, yale tuliyoyashauri tunaamini yatapewa uzito unaostahili. Huu si wakati sahihi wa kufanya uamuzi au kuhamasisha watu kuandamana, sio jambo bora la kudai haki na amani kwenye masuala ya demokrasia,” alisema Mruma.

Alisema changamoto ya ugumu wa maisha haiwezi kutatuliwa kwa watu kuandamana isipokuwa kutoa uchambuzi wa kitaalamu utakaoishauri Serikali njia bora zitakazotumika ili kujikwamua kiuchumi.

Miswada ya uchaguzi

Novemba 10, 2023 Serikali iliwasilisha bungeni miswada minne na kusomwa kwa mara ya kwanza.

Miswada hiyo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023; Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2023 na muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.

Kabla kamati ya Bunge haijaanza kupokea maoni ya wadau, Baraza la Vyama vya Siasa nchini Januari 3, 2024 liliitisha mkutano wa utoaji maoni jijini Dar es Salaam ambao ulihudhuriwa kwa mara ya kwanza na Chadema na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kinachoongozwa na mwenyekiti wake Hashim Spunda Rungwe, baada ya kususa mikutano ya baraza hilo tangu mwaka 2020.

Maoni ya Serikali kwenye miswada

Miongoni mwa mambo ambayo Serikali imefanya mabadiliko kwenye masuala ya demokrasia ni makamishna wa tume ya uchaguzi kufanyiwa usaili badala ya kuteuliwa kama zamani.

Mapendekezo mengine ni kuviwekea sheria vyama vya siasa kuzingatia suala la jinsia.
Muswada huo ambao ni marekebisho yanayotokana na mawazo ya wanasiasa na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, unapendekeza vyama viruhusiwe kufanya uteuzi wa mgombea wa urais wa Zanzibar kwenye mkutano wa halmashauri kuu ya chama.
Kabla ya mapendekezo hayo kifungu cha 6A(3)(a) kwenye sheria hiyo kimeweka sharti kwamba, uteuzi wa mgombea urais lazima ufanywe na mkutano mkuu wa Taifa wa chama cha siasa, lakini kuna baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vina utaratibu wa kumteua mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia halmashauri kuu ya chama Taifa.

Miongoni mwa vyama vyenye utaratibu wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar kupitia mkutano wa halmashauri kuu ya Taifa ni Chama cha Mapinduzi (CCM).

Muswada huo umependekeza kifungu kidogo cha (3)(a) cha kifungu cha 6A cha sheria hiyo kirekebishwe, kuruhusu uteuzi wa mgombea wa urais wa Zanzibar kufanywa na halmashauri kuu ya chama husika, kama ilivyo kawaida kwa baadhi ya vyama vya siasa.

Pia, muswada huo umependekeza kuruhusu fedha za ruzuku kugawanywa kwa vyama vya siasa kwa kuzingatia idadi ya kura za ubunge, idadi ya wabunge na madiwani ambao chama cha siasa kinao kwa wakati husika na siyo kura za ubunge, idadi ya wabunge na madiwani ambao chama kilipata wakati wa uchaguzi mkuu pekee.

Hali ilivyo sasa kwenye sheria ni kwamba kifungu cha 16(3)(b) cha sheria hiyo kinaeleza chama cha siasa kitapata ruzuku kutoka serikalini iwapo kitakuwa kina usajili wa kudumu na kina mbunge au diwani aliyepatikana katika Uchaguzi Mkuu au Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa uliopita.

“Hali hii inafanya iwe vigumu kubadili mgawo wa ruzuku baada ya Uchaguzi Mkuu, endapo katika uchaguzi mdogo chama kimeongeza au kupungukiwa idadi ya kura za ubunge, idadi ya wabunge au madiwani,” unaeleza muswada huo.

Hata hivyo, Serikali imependekeza yafanyike marekebisho ya kifungu cha 16(3)(b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kuweka sharti kwamba fedha za ruzuku zigawiwe kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa idadi ya kura za ubunge, idadi ya wabunge na madiwani ambao chama cha siasa kinao kwa wakati husika.

Utoaji maoni

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akifunga mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi waliokuwa wakijadili miswada hiyo jijini Dar es Salaam aliwataka wadau kujitokeza mbele ya kamati ya Bunge kutoa maoni.

"Nichukue nafasi hii kuwaambia muitikie wito wa Spika wa Bunge (Dk Tulia Ackson) aliyewaalika kwenda bungeni kutoa maoni yenu kuanzia Januari 6 hadi 10 bungeni jijini Dodoma, msiache kwenda, haya mlioyazungumza mmejifua vizuri na mmepata mwelekeo.

"Sisi kama Serikali tutayazingatia maoni yenu, lakini muhimu zaidi kwa ajili ya kuzingatia utawala bora basi tupate nafasi ya kwenda bungeni kutoa maoni yetu, nawashukuru wote waliotoa maoni yao," alisema Dk Biteko.

Katika ufunguzi wa mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenistar Mhagama aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa maoni yao watakayatoa watayachukua kama yalivyo bila kuchakachuliwa.

"Maoni yatakayotolewa hapa yatawekwa sawa na kuwasilishwa mahali panapo husika bila kuchakachuliwa. Hili litakuwa ni jambo jema, hata Serikali ingependa kupata nafasi ya kujifunza kwa wadau wanafikiria nini katika kuimarisha demokrasia ndani ya Taifa letu.

"Serikali inaweza ikapata nafasi nzuri kwa sababu elimu haina mwisho, tutapitia maoni ya wadau na ushauri utakaotolewa katika mkutano huu. Niwahakikishie wajumbe tutashiriki mkutano huu kwa siku zote mbili ili kuyachukua yale yote," alisema Mhagama.