Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mnyika, Kamati ya Bunge wavutana uwasilishwaji maoni sheria za uchaguzi

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeendelea na upokeaji wa maoni ya wadau mbalimbali juu ya marekebisho ya sheria za uchaguzi, huku mvutano ukiibuka baina ya kamati hiyo na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akiwasilisha mapendekezo ya chama hicho.

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema chama hicho kimependekezwa kufutwa kwa miswada ya sheria za uchaguzi inayotolewa maoni sasa, badala yake upelekwe muswada wa marekebisho ya Katiba.

Miswada aliyopendekeza ifutwe ni ule wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na muswada wa sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi

Mnyika aliliibua pendekezo hilo leo Jumatano, Januari 10, 2024 jijini Dodoma alipopewa nafasi ya kutoa maoni kuhusu miswada pendekezwa, jambo lililosababisha Mwenyekiti wa kamati hiyo Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama amkatishe.

Sababu za kumkatisha ni kilichoelezwa na Dk Mhagama, kamati hiyo haina mamlaka ya kubadilisha Katiba.

“Mheshimiwa John naomba uende kwenye vifungu vya sheria, unajua majukumu ya kamati yetu kwa sababu na wewe ulishawahi kuwa mbunge na kama hauko tayari naomba tutakupa nafasi siku nyingine utakapokuwa tayari kutoa maoni," amesema Dk Mhagama.

Hii si mara ya kwanza kwa Chadema kutaka marekebisho ya Katiba na msingi wa mapendekezo yao ni kuweka mazingira mazuri ya sheria mama, kabla ya kuziendea sheria nyingine.

Kabla ya Chadema, wadau wengine wametoa mapendekezo yao wakitaka marekebisho mbalimbali katika miswada hiyo, ikiwemo uchaguzi hasa wa Serikali za mitaa usisimamiwe na wakurugenzi wa halmashauri.

Baada ya kukatishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Mnyika aliachana na hoja hiyo na kuibuka na suala la wakurugenzi wa halmashauri kutosimamia uchaguzi.

Katika hoja yake hiyo, Mnyika ametaka watumishi hao wa umma wasipewe nafasi hiyo kwa kuwa si waadilifu.

"Wakurugenzi wengi ndiyo hao ambao kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wanafanya ubadhirifu wa fedha za umma halafu mnataka wasimamie uchaguzi na watende haki," amehoji Mnyika.

Ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuajiri watumishi watakaokuwa wasimamizi wa uchaguzi na si wakurugenzi wanaoteuliwa na Rais ambaye naye ni mgombea.

Hata hivyo, amependekeza watumishi hao watakaoteuliwa wanapaswa wawepo wa kudumu kwa ngazi ya halmashauri, huku wengine wakiwa wa mikataba.

Pendekezo lingine, amesema ni uwepo wa kifungu kinachotoa kigezo cha ushindi wa kura za Rais ziwe zaidi ya asilimia 50, na kuwe na mwanya wa matokeo yake kupingwa mahakamani.

“Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki ni Tanzania pekee ambayo matokeo ya urais hayapingwi mahakamani,” amesema.

Katika muswada wa sheria ya vyama vya siasa, amependekeza marekebisho katika kifungu kinachokataza vyama vya siasa kuingiza vifaa vya uchaguzi kutoka nje siku 90 kabla ya uchaguzi mkuu.

“Kama chama kinataka kukodi helikopta kwa ajili ya kampeni ni lazima wazikodi kabla ya siku hizo ambayo ni gharama kubwa,” amesema.

Mbali na Mnyika mwingine aliyetoa maoni ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi aliyetaka kuondolewa kwa gharama za kuchukua fomu, ili kuwapa fursa wanawake wengi washiriki mchakato wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Amependekeza wagombea waliowahi kushitakiwa kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia au kufanya ukatili wowote wasiruhusiwe kugombea.

Ametaka usawa wa kijinsia katika vyama vya siasa kwa kuonyesha umri, jinsia na aina ya ulemavu ili kuwa na taarifa sahihi ya watakaopitishwa kuwania nafasi mbalimbali.

Naye mwakilishi wa Chama cha Demokrasia (DP), Abdul Mluya ameitaka Serikali itoe ruzuku kwa vyama vyote vya siasa nchini, hasa vile vilivyoshiriki uchaguzi kwa miaka kuanzia mitatu hadi mitano mfululizo.

Amesema kama vyama vitashindwa kushiriki uchaguzi basi vitakuwa vimejiondoa vyenyewe kwenye ruzuku na kuondoa utitiri wa vyama vya siasa nchini.

Naye katibu Mkuu wa Chama cha UDP, Swaumu Rashidi ameitaka Serikali kutoa ruzuku kwa vyama vyote vya siasa, ili wasishawishike na fedha za magaidi na mafisadi ambao wana lengo la kuhatarisha usalama wa Taifa.

Malalamiko ya vyama

Akifafanua malalamiko ya baadhi ya vyama vya siasa kuhusu kunyimwa haki ya kutoa maoni, Dk Mhagama amesema nafasi ilitolewa kwa wote bila upendeleo na hadi jana vyama 10, taasisi za kidini na wadau mbalimbali wameshatoa maoni yao.

"Hakuna chama cha siasa ambacho kina umuhimu kuliko kingine na ndiyo maana vyama vyote vimetoa maoni yao kwa siku hizi nne bila upendeleo wa aina yoyote," amesema.

Amesema jumla ya vyama vya siasa 18 vyenye usajili na Asasi za kiraia 400, zimetoa maoni.

“Pia, taasisi za dini na watu binafsi wametoa maoni yao moja kwa moja na wengine kwa njia ya maandishi kwa siku nne ambazo kamati hiyo ilikuwa inakusanya maoni,” amesema.