Chadema wataka Dira ya Taifa, Katiba mpya

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Uhuru maarufu kama Ujwanja wa Mayunga mjini Bukoba. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Chadema imetaja mambo matatu yanayopaswa kushughulikiwa na Serikali kwa sasa kuwa ni pamoja nan chi kuwa na Dira ya Taifa kuelekea mwaka 2050, kukamilishwa kwa mchakato wa Katiba mpya na kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Dodoma. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema Serikali inapaswa kuhakikisha nchi inakuwa na Dira ya Taifa ya miaka 50, kukamilishwa kwa mchakato wa Katiba mpya na kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura ili kuleta maendeleo ya kweli.
Mnyika ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Septemba 30, 2023 Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, vyuo vya kati na sekondari ambao ni wanachama wa Chadema (CHASO).
Ameitaka Serikali kushirikisha makundi yote muhimu kwenye mchakato wa kupata dira ya maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050.
"CHASO mshiriki kuandaa mapendekezo ya awali juu ya dira ya maendeleo ya kuelekea mwaka 2050, pamoja na Mabaraza na Chama kushiriki, kama mtendaji mkuu wa Chama tungependa sana kupata maoni ya vijana maana wengi wenu mtakuwepo mpaka mwaka 2050," amesema.
Kwa upande wa Katiba Mpya Myika amesema elimu kuhusu katiba mpya ilishatolewa kwa Watanzania kuanzia mwaka 2011 hadi 2014 hivyo kuchelewesha mchakatio siyo kwamba Watanzania hawana elimu ya katiba.
"Matatizo ya kukwama mchakato wa Katiba mwaka 2014, hayakuwa ni matokeo ya wananchi kukosa elimu, kama ni elimu ingetolewa kwa NEC ya CCM. Serikali iheshimu maoni na matakwa ya wananchi,” amesema.
Kuhusu uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Mnyika amesema ni wakati sasa wa Serikali kuboresha daftari hilo ili vijana wenye sifa wajiandikishe kupata haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Amesema mpaka sasa uboreshaji huo ungekuwa umeshafanyika, lakini bado haujatekelezwa na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuharakisha ili vijana wenye sifa wajiandikishe kupiga kura.
Katika hatua nyingine, Mnyika amegudia suala la makubaliano ya uendelezaji wa bandari akisema tangu Bunge la Jamhuri ya Muungano liliporidhia June 10 mwaka huu kinachopaswa sasa ni kuchukua hatua kuhusu maoni yaliyotolewa na Watanzania
Amesema Serikali ikishatoa kauli Chadema watatoa mwongozo juu ya jambo hilo kwani kulingana na masharti ya urekebishaji wake na kwa kinga za kimkataba zilizopo na kwa ubovu uliopo mkataba ule haurekebishiki badala yake ufumbuzi pekee ni mkataba huo kurudishwa Bungeni ufutwe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) Taifa, John Pambalu amesema lengo la mafunzo hayo kwa viajana ni kuwajengea uwezo wa kuongoza kwenye ngazi mbalimbali ikiwemo udiwani ubunge hadi ngazi ya Urais.
Naye mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Dodoma, Aisha Madoga amsema kuhusu elimu ya katiba Baraza hilo limekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa vijana kupitia mitandao ya kijamii ambayo imekuwa na mafanikio makubwa.
Amesema changamoto kubwa ya vijana ni kutopiga kura ni kukosa vitambulisho vya kupigia kura hivyo wakati wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura ni lazima serikali itoe matangazo ili vijana wegi wajitokeze kupata haki yao ya kuchagua viongozi watakaowaongoza.