NEMC yaingia mkataba na kampuni kukusanya taka za plastiki

Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Dk Immaculate Semesi (kulia) na Mjumbe wa Menejimenti ya Kampuni Gaia Climate, Gediz Kaya wakiwa wameshika mkataba wa makubaliano waliyoingia
Muktasari:
- Nemc yasaini mkataba na kampuni ya Kituruki ya Gaia Climate kwa ajili ya ukusanyaji taka za plastiki Tanzania, huku ikielezwa mpango huo utaongeza fursa ya ajira kwa vijana.
Dar es Salaam. Katika kuimarisha na kuweka misingi madhubuti ya ukusanywaji taka Tanzania, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), limeingia mkataba wa makubaliano ya ukusanyaji taka za plastiki na kampuni ya Gaia Climate ya Uturuki.
mpango huo unaolenga kuchochea na kukuza ajira kwa vijana kwa kukusanya taka za plastiki, urejelezaji na usafishaji wa mazingira kwa kukusanya taka za plastiki ulisaniwa na Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Dk Immaculate Semesi na uongozi wa taasisi hiyo ya Kituruki.
Makubaliano hayo yalifikiwa na pande hizo mbili Dar es Salaam leo Machi 12, 2025 katika Ofisi za Nemc baada ya kufanya kikao na Mjumbe wa Menejimenti ya Kampuni hiyo Gediz Kaya na Viongozi mbalimbali wa Baraza hilo huku wakigusia mipango na njia madhubuti zitakazo tumika kufanikisha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mazingira Mkuu, Fredrick Mulinda amesema ulimwengu wa usimamizi wa mazingira umeibua jambo jipya litakaloongeza tija katika usimamizi wa mazingira.
"Jambo hilo ni biashara ya plastiki (Plastic Credits) itaongeza ajira kwa vijana kwa kukusanya taka za plastiki, Urejelezaji na Usafishaji wa Mazingira kwa kukusanya taka za plastiki," amesema Mulinda.

Kulingana na Mulinda amesisitiza kuwa hiyo ni fursa ya kiuchumi kwa watu mbalimbali nchini kwani itahusisha malipo kwa watu wote watakaohusika kukusanya taka za plastiki katika maeneo mbalimbali nchini, huku ikipunguza athari za kimazingira na kiafya zinazotokana na uchafuzi wa plastiki.
"Suala hili litaisaidia Nemc kufikia lengo lililoagizwa na Serikali la kupunguza asilimia tano ya taka za plastiki nchini na litaongeza nguvu katika kupunguza uchafuzi wa plastiki katika miji mbalimbali nchini," amesema.
Naye mwakilishi kutoka kampuni ya Gaia Climate ya nchini Uturuki Gediz Kaya amepongeza juhudi za Nemc kufanya mashirikiano na kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kushirikiana katika kutunza mazingira kupitia mradi wa kupunguza matumizi ya plastiki ulitokana na mazungumzo kwenye mkutano wa 29 wa mabadiliko ya tabianchi (COP29) Jijini Baku nchini Azerbaijan.