NEC yachochea madai ya Katiba Mpya

Muktasari:
- Mjadala wa madai ya Katiba mpya unazidi kushika kasi kila kukicha, licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kuomba apewe muda ili aimarishe uchumi kwanza, ripoti ya Uchaguzi Mkuu 2020 ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imechochea madai hayo.
Dar es Salaam. Mjadala wa madai ya Katiba mpya unazidi kushika kasi kila kukicha, licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kuomba apewe muda ili aimarishe uchumi kwanza, ripoti ya Uchaguzi Mkuu 2020 ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imechochea madai hayo.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, Agosti 21 aliwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia na kutoa mapendekezo saba ya kufanyiwa kazi, likiwemo la kuanzishwa kwa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo itawapa meno zaidi.
Miongoni mwa hoja za wanaotaka Katiba mpya ni uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, uwepo wake unatajwa utasaidia chaguzi kuendeshwa kwa uhuru na haki.
Tume iliyopo imekuwa ikilalamikiwa kutotenda haki kwa sababu ya muundo wake, uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu hufanywa na Rais ambaye wakati mwingine huwa ni mgombea urais.
Muundo huo umekuwa ukiifanya Tume kutoaminika kwa wananchi na chaguzi ambazo wanazisimamia zimekosa mvuto na kuaminika kama ilivyo kwenye baadhi ya mataifa ambayo Tume zao zinafanya kazi kwa uhuru.
Mapendekezo ya NEC ya kutaka ianzishwe sheria inayowatambua na kuwapa mamlaka zaidi imetoa tafsiri kuwa wanataka wajiendeshe kwa uhuru na ufanisi zaidi pasi hofu ya kuingiliwa na viongozi, yanaipa nguvu hoja ya wanaotaka tume huru ya uchaguzi.
Licha ya NEC na viongozi wa Serikali mara kwa mara kupinga kutoa au kupokea maelekezo ya uendeshaji wa uchaguzi, lakini ukweli unabaki kuwa kuna mkanganyiko wa kisheria na tume hiyo haiko huru.
Baadhi ya mapendekezo yanaonyesha wanalenga kuboresha utendaji, kuongeza kuaminika kwa wadau na kupata uhuru zaidi.
Tume imekuwa ikilalamikiwa kuwatumia wakurugenzi wa halmashauri ambao ni makada wa chama tawala na huteuliwa na Rais wa chama tawala kusimamia chaguzi, sasa inapendekeza kuwe na watendaji wake hadi ngazi ya halmashauri.
Soma zaidi: Warioba ashindilia msumari Katiba Mpya
Kama pendekezo hili litapitishwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika 2025, ingawa inaonekana gharama ndizo zitakuwa kikwazo cha utekelezwaji wake kama alivyodokeza Rais Samia.
Pendekezo jingine ni kuunganishwa sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura namba 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, sura ya 292 ili kurahisisha utekelezaji wa sheria hizo.
Vilevile, NEC inapendekeza uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu usimamiwe na mamlaka moja.
Kimsingi mapendekezo ya NEC yanaonyesha taasisi hiyo inavyofanya kazi katika mazingira magumu ambayo pia yanawafanya wasipate uungwaji mkono wa baadhi ya wadau pindi wanapotangaza matokeo ya kuendesha uchaguzi.
Wanaodai Katiba mpya wanataka iweke wazi juu ya Tume huru ya uchaguzi kama ilivyokuwemo kwenye rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2014 ambayo ilipendekeza Bunge lichuje na kupitisha majina ya wateule wa Rais kwenye nafasi husika.
Ipo mifano ya nchi kadhaa za Afrika ambazo Tume zao za uchaguzi zinafanya kazi kwa uhuru. Hilo limewezekana kwa sababu mamlaka ya uteuzi haijaachwa kwa Rais pekee, bali na Bunge limepewa mamlaka ya kuwathibitisha.
Mfano wa Tume hizo ni ile ya Zambia (ECZ) ambayo ilianzishwa mwaka 1996 chini ya Ibara ya 76 ya Katiba ya Zambia, inaundwa na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine wasiozidi watatu ambao wanateuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge.
Tume hiyo imesimamia uchaguzi wa Agosti 12, 2021 nchini humo na kumtangaza kiongozi wa upinzani, Hakainde Hichilema kuwa mshindi katika uchaguzi huo dhidi ya Rais Edgar Lungu, ambaye alilalamikia rafu kwenye uchaguzi huo. Hichilema ameapishwa jana kuwa Rais wa saba wa Zambia.
Soma zaidi: Serikali yawajibu wanaotaka Katiba Mpya
Tume ya Uchaguzi ya Malawi nayo imeonyesha mfano wa kuigwa kwa kufanya maamuzi bila kuingiliwa na kiongozi aliye madarakani. Tume hiyo ilisimamia uchaguzi mkuu wa Juni 2020 na kumtangaza Lazarous Chakwera kuwa mshindi dhidi ya Profesa Peter Mutharika.
Vilevile, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) ina mwenyekiti na wajumbe ambao wanateuliwa na Rais, lakini wanathibitishwa na Bunge. Tume hiyo nayo imejengwa katika misingi ya kuifanya iwe huru.
Maoni ya wadau
Wakizungumzia hatua ya Tume kujitengenezea njia ya kuwa huru, wasomi na wanasiasa wamesema NEC inakabiliwa na mazingira magumu ya kisheria, ndiyo maana wanahitaji maboresho zaidi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema pendekezo la Tume la kuwa na chombo kimoja cha kusimamia chaguzi zote ni kutaka kujenga imani ya wananchi kwa chombo hicho.
Anasema Tume inabanwa sana na sheria ndiyo maana wanafanya wanayoyafanya ili kukidhi matakwa ya sheria hizo. Hata hivyo, anasema ni wakati mwafaka Serikali ikayachukua mapendekezo yao na kuyatekeleza.
“Kweli Tume yetu huwa inabanwa sana na hawapendi lakini basi tu. Sheria haiwapi ule uhuru wanaouhitaji, nadhani ni wakati mzuri wamelitoa hili, ni vizuri wakasikilizwa,” anasema mwanazuoni huyo.
Anasisitiza kwamba kwa sheria zilizopo, NEC haiwezi kuwa huru na itaendelea kukosa uhalali kwa wananchi, ndiyo maana wengi wanasusia chaguzi kwa sababu hawaoni umuhimu wake kama wanajua fulani atachaguliwa tu.
Aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha NRA kwenye uchaguzi wa 2020, Leopold Mahona anasema anaamini Tume inafanya kazi kwa kufuata sheria zilizopo, maana yake sheria hizo ni mbovu.
Mahona anasema sheria hizo zina mianya mingi ambayo imekuwa ikitumiwa na chama tawala kuwaengua wapinzani wakati wa uteuzi wa wagombea, jambo ambalo linaharibu taswira ya Tume kwa wananchi.
“Kuna mianya mingi kwenye sheria ambazo zinatumika, mara utasikia mgombea ameenguliwa kisa hakusaini fomu ya maadili mbele ya msimamizi wa uchaguzi. Kama tukitengeneza sheria zetu vizuri, sidhani kama itakuwa hivi ilivyo,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kwamba huwezi kudai Tume huru bila kufanya mabadiliko ya katiba kwa sababu katiba nzuri itaelezea muundo wa Tume huru na kuipa uhuru katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lyimo anasema mapendekezo ya NEC yanaonyesha dhahiri kwamba inatafuta kujiweka huru kutoka kwenye mazingira magumu ambayo wanafanya kazi.
Anasema suala la NEC kusimamia chaguzi zote nchini ni la muhimu kwa sababu wao ndio wana utaalamu na masuala ya uchaguzi na hawana majukumu mengine zaidi ya hilo. Hivyo, Tamisemi kuandaa uchaguzi wa Serikali za mitaa ni kupunguza ufanisi na kuongeza gharama.
“Kuna gharama kubwa katika kutenganisha uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa. Uhifadhi wa nyaraka unakuwa rahisi kama chaguzi zote zitasimamiwa na chombo kimoja. Tume wanataka urahisi wa kufanya kazi na kuongeza imani ya wananchi,” anasema Lyimo.
Hamdun Omari anasema mapendekezo ya NEC yanaonyesha uhitaji wa Katiba mpya itakayoondoa upungufu wa kisheria uliopo.