Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndoa ya Bandari na TICTS yakoma rasmi

Muktasari:

Baada ya kuhudumu kwa miaka 22 katika Bandari ya Dar es Salaam, hatimaye ndoa ya kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imekoma rasmi mwaka huu.

Dar es Salaam. Baada ya kuhudumu kwa miaka 22 katika Bandari ya Dar es Salaam, hatimaye ndoa ya kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imekoma rasmi mwaka huu.

Hatua hiyo inakuja baada ya mkataba wa miaka mitano wa wawili hao uliosainiwa Julai 6, 2017 kufikia ukomo Septemba 30, mwaka huu, licha ya kuwepo kipengele cha kuuhuisha, menejimenti ya TPA imetaka kuusitisha.

TICTS imehudumu katika bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 22 sasa tangu mwaka 2000 kwa mara ya kwanza iliposaini kutoa huduma ya makontena.

Mwananchi inakuthibitishia taarifa za ndani ilizozipata kuhusu nia ya menejimenti ya TPA kusitisha mkataba huo na TICTS, kwa kile ilichokifafanua mazungumzo baina ya pande hizo mbili hayakufanikiwa, kutokana na kutokubaliana katika vigezo vya kuuhuisha kama ilivyoainishwa katika ibara ndogo ya 2.2.1 ya mkataba huo.

Kulingana na taarifa hiyo ya ndani kutoka menejimenti kwenda kwa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, mkataba kati ya wawili hao uliisha Septemba 30, 2022 na mazungumzo kati ya pande mbili hayakufanikiwa.

Chanzo chetu kilieleza tayari TPA imewasilisha taarifa kwa Bodi ya Wakurugenzi inayoongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu Ernest Mangu kusudio la kutokuendelea na TICTS.

Aidha, TPA inayoongozwa na Plasduce Mbossa imeomba baraka za bodi ili waweze kuiandikia barua kampuni hiyo kutohuisha mkataba huo, na tayari wamejipanga kusimamia wenyewe shughuli zilizokuwa zikifanywa na TICTS.

“Sina shaka hata kidogo kwamba bodi itakubali ombi hili. Na tayari tumejipanga kuhakikisha tunasimamia wenyewe wakati tunatafuta mtu mwingine ambaye atakuwa na uwezo mkubwa zaidi,” alisema kigogo mmoja wa TPA.

Gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, lilimtafuta Mbosa kujua wapi hawakuelewana kwenye mazungumzo yao na TICTS, lakini hakupatikana kwani simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita pasina kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe hakuujibu. Jitihada hizo zilifanyika pia kwa kuutafuta uongozi wa TICTS bila mafanikio.

Katika maelezo ya menejimenti ya TPA kwenda kwa bodi yanaeleza kumweka kando TICTS kunalenga mahitaji ya hatua nyingine zinazopaswa kuchukuliwa na uongozi, katika kutekeleza wajibu wake wa kusimamia mkataba ili kulinda masilahi ya mamlaka, Serikali na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, mtoa taarifa wetu alieleza kabla ya kukamilika kwa mkataba huo Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mei 16, mwaka huu iliunda timu ya wataalamu kujadiliana na TICTS kuhusu kuongeza mkataba na ilihusisha vikao vitatu.

Alisema vikao hivyo viliendelea Septemba 7, mwaka huu kutengeneza njia ya mashauriano zaidi na mamlaka za juu katika maeneo matatu ambayo hawakuwa wamefikia muafaka ambayo ni ukodishaji wa kudumu wa mwaka, ada ya mrabaha ya kila mwezi na upitishaji wa kontena.

Chanzo chetu hicho kiliendelea kueleza kuwa Septemba 23, mwaka huu bodi ya wakurugenzi ya TPA iliridhia ombi la menejimenti la nyongeza ya mkataba wa miezi mitatu kukamilisha makubaliano ambao utaisha Desemba 31.

Hata hivyo, Oktoba 21, mwaka huu TICTS iliwasilisha ombi la kuongeza mkataba ambalo halikufikia viwango vilivyotakiwa na TPA.

“Hatua ya kutohuishwa kwa mkataba huo ni muhimu kwa kuwa menejimenti itapata fursa ya kuendesha gati 8 hadi 11 ambazo zimekuwa chini ya sekta binafsi kwa muda miaka 20, ili kupata mapato yanayotarajiwa kukusanywa,” alisema

Kabla ya uamuzi wa menejimenti wadau walianza kupinga kuendelea kwa mkataba kati ya TICTS na TPA, kwa madai kuwa kampuni hiyo haina utendaji wa kuridhisha.

Julai 23, mwaka huu, msemaji wa sekta ya mawasiliano, teknolojia, habari na uchukuzi wa ACT Wazalendo, Ally Salehe alisema suala la TICTS kukodishwa tena au la, linapaswa kuchukuliwa kwa umakini na kufikiwa uamuzi wenye kujali na kulinda uzalendo.

“Serikali isitishe nyongeza ya mkataba wa kukodisha kitengo cha makasha kati yake na TICTS, kwa kuwa ni wazi imeshindwa kukidhi matarajio ya Serikali yanayolenga kuongeza tija kwenye bandari yetu,” alisema Salehe.