Ndege yapata hitilafu angani, TCAA yaizuia kuruka

Ndege ya Shirika la Precision Air yenye namba za usajili 5H PWD. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeizuia ndege Shirika la Precision Air kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma yenye namba za usajili 5H PWD kuruka tena angani baada ya kupata hitilafu ikiwa angani jana Februari 15, 2023.

Dar es Salaam. Wakati abiria waliokuwamo ndani ya ndege ya Shirika la Precision Air kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma wakipata taharuki jana asubuhi Februari 15, 2023 baada ya kupata hitilafu na rubani kulazimika kuzima injini moja, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeizuia ndege hiyo yenye namba za usajili 5H PWD kuruka tena angani.

Changamoto hiyo ilijitokeza kilomita chache tangu ndege hiyo iliporuka, hali iliyomlazimu rubani kuirudisha Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Meneja Masoko wa Precision Air, Hilary Mremi amesema injini hiyo haikuzimika ghafla, bali ilizimwa na rubani baada ya kupata taarifa kwenye mifumo ya uendeshaji ikimwonyesha tahadhari katika mfumo wa injini.

Amesema, aliizima injini hiyo ili kuitunza kisha aligeuza kurudi Dar es Salaam kwa kutumia injini moja, kwa sababu ndege hiyo ina injini mbili.

Mremi amesema kwa taratibu za kiusalama, rubani akipata taarifa kwenye mifumo ya uendeshaji, huchukua tahadhari kulingana na taratibu zilizowekwa.

“Hivyo aliizima injini moja ili kuitunza, kwa sababu taratibu zinaelekeza ikitokea kitu kama hicho, rubani analazimika kutua kwenye kiwanja kilichopo karibu kwa ukaguzi zaidi. Na kwa wakati huo uwanja uliokuwa karibu ni uliokuwa Dar es Salaam na si Dodoma kama inavyoripotiwa mitandaoni,” amesema ofisa huyo.

“Tunapenda kuwatoa hofu wateja na umma kwa jumla kwamba ndege zetu ziko salama. Hizi ndege zimetengenezwa kwa injini mbili na endapo moja ikipata changamoto, nyingine inaweza kufidia upungufu na kuiwezesha ndege kutua salama.”

“Ndege zetu zinafanyiwa matengenezo kwa mujibu wa taratibu za kiusalama za hapa nchini na kimataifa. Zinakaguliwa mara kwa mara na mamlaka husika za ndani na kimataifa,”amesema Mremi.


Kauli ya TCAA

Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema ndege hiyo ilipata hitilafu umbali wa kilomita 125 usawa wa Morogoro, kabla rubani hajazima injini moja na kurudi kituo cha karibu kilichopo Dar es Salaam.

“Ndege imetengenezwa katika namna ambavyo inatoa ishara nyingi, pale mbele kwenye dashboard taa yoyote ikiwaka lazima uahirishe safari, alipofika usawa wa kilomita 125 aliona taa ya injini imewaka, hivyo kiutaratibu lazima urudi chini usiendelee na safari, hivyo aliizima injini moja akarudi chini akatua,” amesema Johari.

“Hii ni mara ya pili inatokea, Januari ndege hii ilileta hitilafu hiyohiyo, kwa hiyo imetulazimu kuizuia mpaka ichunguzwe kwa kina kwa nini imejirudia, pamoja na kwamba rubani ameishusha salama. Ila ndege zingine ziko salama,” amesema Hamza.


Kilichojiri ndani ya ndege angani

Wakati Precision na TCAA wakitoa ufafanuzi huo, abiria waliokuwamo ndani ya ndege walidai kuwa walikuwa wameshajiandaa kutua kabla ya injini kuzima na rubani kuwataarifu changamoto iliyotokea kisha kurudi tena jijini Dar es Salaam kwa kutumia injini moja.

Mmoja wa abiria aliyekuwamo ndani ya ndege, Joseph Rwegasira alidai, “ndege iliondoka saa 11 (alfajiri) kwenda Dodoma, lakini wakati tunakaribia kutua ndipo changamoto ikatokea nikaona injini imezima, tupo hewani tulikaa kwa muda. Rubani akatangaza kurudi Dar es Salaam kwa dharura kwa kutumia injini moja, ndege ikageuza kurudi.

“Wakati huo wote kulikuwa na taharuki ndani ya ndege, abiria wanahama siti wanarudi kukaa siti za nyuma, wengine wanalia kwa lugha zao, wengine wanasali kama mwisho umefika, kiufupi hali ilikuwa mbaya. Binafsi nampongeza rubani kwa kutupatia ujasiri na kutushusha salama.”

Licha ya kurudi jijini Dar es Salaam, Rwegasira ni miongoni mwa abiria waliofanikiwa kusafiri kwa ndege nyingine ya Precision jana hiyo hiyo saa sita mchana kuelekea Dodoma.

Rwegasira alizitaka mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kuzikagua ndege hizo ili kuepusha madhara yanayoweza kuwapata abiria siku za mbeleni.