Ndege ya ATCL yakamatwa nje, Serikali yafunguka

Muktasari:
Serikali imewatoa hofu Watanzania kuhusu taarifa za kushikiliwa kwa ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) nchini Uholanzi, ikisema haiwezi kutaifishwa kutokana na rufaa ya kesi inayoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Dar es Salaam. Serikali imewatoa hofu Watanzania kuhusu taarifa za kushikiliwa kwa ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) nchini Uholanzi, ikisema haiwezi kutaifishwa kutokana na rufaa ya kesi inayoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Jana baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti kuhusu mwekezaji wa Sweden aliyeshinda tuzo ya Dola 165 milioni (Sh380 bilioni) dhidi ya Tanzania na kuishawishi Mahakama ya Uholanzi kushikilia ndege hiyo kama kigezo cha kushinikiza malipo yake, licha ya kutopata uhalali wa ICSID.
Hata hivyo, akizungumza jana na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi alikiri mwekezaji huyo kushinda tuzo hiyo na ndege imeshikiliwa.
Kituo hicho cha ICSID chini ya majaji watatu, Sir Christopher Greenwood KC wa Uingereza, Stanimir Alexandrov na Funke Adekoya SAN kilitoa tuzo kwa niaba ya Eco-Development na kuamuru Tanzania kulipa kiasi hicho cha fedha Aprili mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa katika mashirika ya kimataifa, ndege hiyo ipo uwanja wa ndege wa Maastricht, nchini humo tangu Januari mwaka huu kwa madai ya hitilafu za kiufundi katika injini yake.
“Ni kweli kwamba walienda katika mahakama ya nchini Uholanzi baada ya sisi kufanikiwa kubishana na ICSID ili kusitisha utekelezaji, lakini kila kitu kiko chini ya udhibiti,” Dk Feleshi alisema jana.
Alisema Serikali tayari imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Uholanzi na kwamba hawezi kueleza mengi juu ya suala hilo.
Kiini cha mgogoro
Septemba 20, 2017 gazeti hili liliripoti kuhusu uamuzi wa Eco Development Group kuwasilisha madai ya usuluhishi ya dola milioni 500 dhidi ya Serikali juu ya uamuzi wake wa kufuta umiliki wa ardhi wa mradi wa mabilioni ya sukari wa Bagamoyo.
Kamishna wa Ardhi aliieleza Kampuni ya Bagamoyo Eco Development Novemba 2017 kuwa Serikali iliazimia kufuta hati miliki ya hekta 20,400 na kuweka jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uamuzi huo ulichagizwa na madai ya Eco Development, inayomilikiwa na raia 18 wa Sweden na viongozi wa biashara kuwasilisha madai yake ICSID mwaka 2017 chini ya mkataba wa uwekezaji baina ya Sweden na Tanzania, ikilalamika uamuzi wa Serikali kuvunja mkataba wa kuendeleza mradi wa miwa Bagamoyo.
Mradi huo ulikusudiwa kuzalisha sukari kwa ajili ya kuuza nje ya nchi pamoja na kemikali ya ethanol kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme. Mwekezaji aliilalamikia pia Serikali kutoanzisha udhibiti mpya wa sekta ya sukari na kutoa ardhi bila kazi.
ATCL ina jumla ya ndege 11, inamiliki ndege nne aina ya Airbus A220-300, huku A220 moja pekee ikiruka hadi sasa na nyingine zikitajwa kuwa na hitilafu.
Mikasa ya ndege
Mwaka 2017, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho aliibua tuhuma za kushikiliwa kwa ndege aina ya Dash 8-Q 400 iliyotakiwa kuwasili nchini Julai mwaka huo kwa madai ya Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd kuidai Serikali Dola 38.7 milioni, sawa na Sh87 bilioni.
Kampuni hiyo ilifungua kesi katika ICSID na ilipofika Juni 2010, mahakama hiyo iliipatia tuzo ya ushindi huo kabla ya Juni 30, mwaka 2017 kukabidhiwa kibali kwa Kampuni hiyo cha kukamata mali zote za Tanzania zitakazokuwa katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.
Madai ilikuwa kuvunja mkataba wa kampuni hiyo ya Canada iliyokuwa ikijenga barabara ya kutoka Tegeta Wazo-Bagamoyo.