NBS yasema sensa imefanikishwa na Watanzania wenyewe

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa
Muktasari:
Mtakwimu Mkuu wa Serikali amesema sensa imefanyika kwa urahisi na asilimia 98 ya waliofanikisha kazi hiyo ni Watanzania wenyewe.
Dar es Salaam. Asilimia 98 ya watalaam waliohusika katika Sensa ya Watu na Makazi ni Watanzania na wasomi wa hapa nchini.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 31 na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alipokuwa akitoa tathmini ya Sensa ya Watu na Makazi 2022 katika uzinduzi wa ripoti ya sensa iliyofanyika jijini Dodoma.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu kazi ambayo umetutaka tufanye mheshimiwa Rais, imefanyika kwa ufanisi wa hali ya juu.
“Kazi hii imekwenda sanjari na miongozo ya Umoja wa Mataifa, lakini haya yamefanyika kwa ufanisi kutokana na utashi wa kisiasa kuanzia kwa Rais na watendaji wote,” amesema Dk Albina.
Mtakwimu huyo amesema kuzinduliwa kwa matokeo hayo kunaenda sambamba na uzinduzi wa mwongozo wa takwimu za sensa ili kuleta majibu ya changamoto zilizopo kulingana na idadi ya watu na kupanga maendeleo ya nchi.
“Matokeo haya yanaafiki sekta mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimazingira mfano katika mabenki yetu tunaenda kwenye mikopo hatutahitahi masharti magumu ya kutoa hati za viwanja, kupitia sensa hii tumechukua takwimu zote za wajasiriamali wadogo wadogo na tunajua biashara zao ziko sehemu gani.
“Hii inarahisisha sekta za kibenki kutoa mikopo ya kutosha kwa makundi mbalimbali ili wajikwamue kiuchumi na kuongeza kipato chao bila masharti magumu,” amesema.