Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Namna ya kulikwepa jinamizi la ajali za barabarani

Picha na AI

Muktasari:

  • Kila mtu akitimiza wajibu wake barabarani basi tutamaliza kama siyo kupunguza kabisa ajali hizo ambazo zinasababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali pamoja na umasikini.

Dar es Salaam. Wakati jinamizi la ajali likiendelea kutafuna roho za ndugu zetu barabarani, wadau wa usalama wameshauri usimamizi wa sheria, elimu, ukaguzi zaidi wa vyombo vya moto na madereva ufanyike kwa mkazo.

Kila mtu akitimiza wajibu wake barabarani basi tutamaliza kama siyo kupunguza kabisa ajali hizo ambazo zinasababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali pamoja na umasikini.

Hadi mwisho wa mwaka jana 2024, Jeshi la Polisi nchini lilisema ajali za barabarani zilizotokea katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2024 zilikuwa 1,735. Kwa mujibu wa jeshi hilo, ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo katika kipindi hicho.

Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2023, matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 1,733 katika kipindi cha Januari hadi Desemba na kusababisha vifo 1,118.

Katika hilo wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alimuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, pamoja na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali hizo za barabarani.

Hata hivyo, wakati akihitimisha Bunge jijini Dodoma Rais Samia Suluhu Hassan Juni 27, 2025 alisema ajali za barabarani ndilo eneo ambalo Jeshi la Polisi linahitaji kuongeza kasi ya udhibiti.

"Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani, lazima nazo tuendelee kuzitafutia muarobaini wake," alisema Rais Samia katika hotuba yake ya kuhitimisha Bunge la 12.

Akizungumza na Mwananchi, Balozi wa Usalama Barabarani kutoka Asasi ya RSA Tanzania, Ramadhan Msangi amesema elimu ya usalama barabarani huku kila mmoja akitimiza wajibu wake ndilo jambo linalopaswa kutiliwa mkazo sambamba na kuwa endelevu.

Msangi amesema kila mmoja akiibua changamoto za barabarani ikiwemo uendeshaji hatarishi, ulevi kutofuata sheria itakuwa ni hatua muhimu katika udhibiti wa ajali hizo.


Washauri ndugu kutosaifiri pamoja

Kwingineko kutokana na baadhi ya ajali kutokea huku zikihusisha madhara ya vifo kwa ndugu wa familia moja baadhi ya watu wameshauri ndugu wanapokuwa na safari ya pamoja basi waepuke kupanda gari moja kama kosta ama basi.

Ikirejewa ajali iliyotokea wilayani Same mkoani Kilimanjaro iliyohusisha basi na gari aina ya Coaster kugongana kisha kuwaka moto huku watu 38 kupoteza maisha, akiwamo Mzee Abdalah Kiluvia ambaye kwa upande wake alipoteza ndugu wanne na wapangaji sita katika ajali hiyo.

Kati ya ndugu wanne aliowapoteza, amesema yumo mdogo wake, shemeji yake na ndugu wengine wawili, sambamba na wapangaji sita, walioambatana katika safari hiyo ya kwenda harusini.

Majonzi hayo sio kwa Mzee Kiluvia pekee, hata mwanawe, Ramadhani Kiluvia anakabiliwa nayo, akisema amepoteza mama na mdogo wake.

Pia, ajali iliyotokea mwaka 2023 ambapo familia ilipoteza ndugu wanne waliofariki dunia katika ajali iliyotokea usiku wa Agosti 2 huko Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani wakiwa safarini kuelekea msibani wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza na Mwananchi mkazi wa Dar es Salaam, David Mathayo amesema kama ndugu wana ulazima wa kusafiri pamoja basi ni vyema kusafiri gari tofauti ili kuepusha vifo vya familia moja.

“Mnaweza mkagawana huyu apande huku yule apande kule ingawa hatuombei mabaya ajali zitokee,” amesema Mathayo.

Rosemary Richard yeye amesema kwa kuwa ajali haiepukiki unaweza ukafuata sheria, chombo kikawa kizima, kila kitu kiko sawa lakini ikaja kusababishwa na jambo lingine la nje basi ni vyema kuchukua tahadhari ya kwa kutosafiri pamoja.

Mtazamo wa Balozi Msangi unatofautiana na Mathayo na Rosemary kwani yeye amesema kitendo cha ndugu kusafiri tofauti maana yake tunatangaza tumeshindwa kudhibiti na kukabiliana na ajali za barabarani.

“Sheria taratibu na kanuni za barabarani zikifuatwa basi si kosa kwa familia kusafiri kwa pamoja. Tukifikia hatua hiyo kutakuwa hata ikiwa kuna shughuli hakutakuwa na mantiki za kifamilia kukodi gari,” amesema.

Msangi amesema mke akisafiri pekeyake, baba na watoto pamoja na ndugu wengine vivyo hivyo inakua haina maana ya kuwa na gari la familia.

“Maoni yangu ni kwamba tuwekeze kwenye kuelimisha kuhusu usalama barabarani kwakuwa sauti ya mtu mmoja inaweza kuokoa uhai wa watu wengi. Mamlaka ziendelee kutenda kwa weledi.

“Suala kama vizimia moto je, vinafanya kazi, vimekaguliwa? Madereva pia watambue wakiona ajali gari linawaka watumie vizimia moto vyao kuokoa uhai wa watu wengine,” amesisitiza.

Amesema ipo haja ya kuongeza usimamizi wa sheria kwenye gari za kukodi ili kudhibiti madereva wake ambao hawafuati sheria za barabarani.

Mkurugenzi wa kampuni ya magari ya kukodi ya Vimac Travel and Tours, Marik Assenga amesema kwa upande wake wa uzoefu wa miaka mingi barabarani wa zaidi ya miaka 25 ameona uchovu wa madereva wa magari ya kukodi ndio sababu kubwa ya ajali.

“Uchovu na usingizi unasababishwa na dereva kuwa mmoja kutokana na kipato anachopata anaona bora asafiri mwenyewe kuliko kwenda na msaidizi wake.

“Madereva wanapaswa kuwa wawili wawili ‘special hire’ zinapata ajali kwa sababu ya usingizi na uchovu, askari pia waongeze umakini barabarani madereva pia wawapatie elimu watumiaji wa barabara kwa sababu elimu inahitajika kila siku,” amesema Assenga.

Amesema yeye akiwa ni miongoni mwa waanzilishi wa gari za kukodi katika miaka ya 2000 zamani madereva walikuwa wakisafiri wawili wawili tofauti na sasa.