Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwongozo mpya wa upimaji Covid-19

Mwongozo mpya wa upimaji Covid-19

Muktasari:

  • Serikali imetoa mwongozo mpya wa tatu wa uchukuaji wa sampuli za vipimo vya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona katika hospitali na vituo maalum nchini kwa kufuata hatua tisa muhimu.

Dar es Salaam. Serikali imetoa mwongozo mpya wa tatu wa uchukuaji wa sampuli za vipimo vya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona katika hospitali na vituo maalum nchini kwa kufuata hatua tisa muhimu.

Tofauti na mwongozo wa kwanza na wa pili ambayo iliwalenga wageni kutoka nje na wale wanaosafiri nje ya nchi, mwongozo huu uliotolewa Januari 14, mwaka huu na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi, unawalenga wananchi wa kawaida ndani ya nchi.

Mwongozo huo umezungumzia kuhusu wagonjwa wanaostahili kupimwa, mapokezi ya wateja, uchukuaji, utunzaji na usafirishaji wa sampuli, chumba cha kuchukulia sampuli, malipo ya vipimo, muda wa kuchukua sampuli, uhakika wa sampuli, majibu ya vipimo na uhakiki wa majibu ya vipimo.

Profesa Makubi alisema wagonjwa wote wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo watapimwa baada ya daktari husika kuagiza na si vinginevyo.

“Wagonjwa wote wanaohisiwa kuwa na ugonjwa watapimwa baada ya daktari husika kuagiza na kipimo kitatolewa katika kituo cha kutolea huduma za matibabu anakotibiwa mgonjwa husika,” alisema.

Alisema wasafiri wote wanaokwenda nje ya nchi ambapo nchi husika inahitaji vipimo vya Covid-19 hao ndiyo watafanyiwa vipimo bila dalili yoyote ya ugonjwa huo.

Akizungumzia malipo ya kipimo hicho ambacho mgonjwa atachukuliwa sampuli mbili ya kooni na damu, Profesa Makubi alisema itakuwa ni Sh230,000 kwa kila sampuli.

Aidha, alisema majibu ya kipimo hicho yatatolewa kwa njia ya simu ya kiganjani itakayoelekeza `link’ ya kupakua majibu na cheti kitatolewa baada ya saa 24 baada ya sampuli kufika Maabara ya Taifa kwa mkoa wa Dar es Salaam.

“Nje ya mkoa wa Dar es Salaam majibu yatatolewa ndani ya saa 48, kwa mteja ambaye hatapata majibu kwa wakati, kituo husika kitatakiwa kufuatilia maabara ya taifa,” alisema Profesa Makubi.

Hospitali zinazotoa huduma ya upimaji kwa mkoa wa Dar es Salaam ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za Rufaa Mkoa za Amana, Mwananyamala na Temeke pia zinahusika kuchukua sampuli.

Nyingine ni pamoja Aga Khan, Kliniki ya IST, Hospitali ya Sinza, Hospitali ya Mbagala na Hospitali ya Kigamboni zinahusika na uchukuaji wa sampuli na kuziwasilisha Maabara ya Taifa kwa lengo la kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaosubiri huduma ili maabara ibaki na zoezi la kupima.

Mpaka kufikia jana jioni, watu milioni 95,566,768 duniani kote walikuwa wamedhibitishwa kuugua ugonjwa huo, huku 2,051,418 wakifariki dunia na wengine 69,279,554 wakipona.

Mwongozo wa upimaji toleo la pili uliotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima Januari 4 mwaka huu, ulielezea ongezeko la gharama za vipimo kufuatia kuongezeka kwa vimelea vipya vya ugonjwa wa Covid-19 na mabadiliko ya teknolojia katika upimaji.

Gharama hizo zilipaa kutoka Sh40,000 mpaka Sh230,000 (Dola za Marekani 100).

Kuongezeka kwa wagonjwa wapya wanaoripotiwa kila siku duniani na kuibuka kwa aina mpya ya vimelea vya ugonjwa huu (New Variant Strains) katika baadhi ya nchi na mabadiliko ya teknolojia katika upimaji, alivitaja kuwa chanzo cha ongezeko la gharama hizo.

“Kuna nchi zimeomba kuongezeka kwa kipimo cha IgM Antibody sanjari na PCR na kuongezeka kwa mahitaji ya vituo vya kuchukulia sampuli imesababisha maboresho ya mwongozo toleo la kwanza la Julai 20, 2020,” alisema Gwajima kwenye taarifa yake.

Julai 20, mwaka jana, Wizara ya Afya iliandaa mwongozo wa kwanza wa kuwapima virusi vya corona wanaokwenda nje ya nchi, unaolenga kuweka utaratibu wa upimaji wa wasafiri kwa hiari kwa wanaohitaji kwenda kwenye nchi ambazo zinahitaji wawe wamepima kabla ya safari zao.

Gharama za vipimo vya Covid-19 zilikuwa Sh40,000 kwa raia wa Tanzania, Sh60,000 kwa raia mkaazi wa Tanzania na Sh 230,000 kwa raia wa kigeni.