Mwili wa Mtanzania aliyeuawa vitani Israel kurejeshwa Jumamosi, mahafali yake leo

Kijana Clemence Mtenga enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Mtenga alikuwa miongoni mwa Watanzania wawili na raia wa mataifa mengine waliokuwa hawajulikani tangu yalipotokea mapigano kati ya Israel na Palestina, hususan eneo la Gaza.
Dar es Salaam. Jina la Clemence Mtenga aliyefariki dunia nchini Israel ni miongoni mwa wahitimu katika Mahafali ya 42 ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro.
Wakati mahafali hayo yanafanyika leo Alhamisi, Novemba 23, 2023 chuoni hapo, mwili wa Mtenga uliagwa jana usiku, Jumatano Tel Aviv, Israel ambapo baadhi ya Watanzania walihudhuria ibada hiyo fupi.
Mtenga alikuwa miongoni mwa Watanzania wawili na raia wa mataifa mengine waliokuwa hawajulikani tangu yalipotokea mapigano kati ya Israel na Palestina, hususan eneo la Gaza.
Katika kitabu cha orodha ya majina ya wahitimu wa SUA wa Shahada ya Sayansi ya Kilimo cha Matunda na Mbogamboga (Bachelor of Science ina Hortculture), jina la Mtenga ni la 18 akiwa amesajiliwa kwa namba HOT/D/2020/0045.
Mara baara ya kuhitimukozi hiyo Mtenga alikuwa sehemu ya wahitimu 260 waliokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.
Taarifa za kifo chake, zilitolewa na Serikali ya Tanzania, Novemba 17, 2023 na kueleza kuwa ilikuwa inaendelea kufuatilia taarifa za Mtanzania mwingine, Joshua Mollel.
Mwili wa Mtenga unatarajiwa kuwasilia nchini Jumamosi ya Novemba 25, 2023.