Mtanzania aliyepotea Israel afariki dunia

Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha wizara hiyo imesema marehemu Clemence alikuwa ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema yathibitisha kupokea taarifa za kifo cha Clemence Mtenga, Kijana Mtanzania ambaye ni miongoni mwa Watanzania wawili ambao pamoja na raia wa mataifa mengine walikuwa hawajulikani.
Watanzania hao ni wale waliopotea tnagu tangu yaliyopotokea mapigano Oktoba 7, 2023, nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina hususan Gaza.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha wizara hiyo imesema marehemu Clemence alikuwa ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.
“Tayari Wizara imechukua hatua stahiki ikiwemo kuijulisha familia na inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Israel kuhakikisha kwamba taratibu za kuurejesha mwili wa Marehemu nchini kwa ajili ya mazishi zinakamilika kwa wakati. Aidha, Wizara inaendelea kufuatilia taarifa za Mtanzania mwingine Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo tangu yalipotokea mashambulizi hayo,” sehemu ya taarifa hiyo inaeleza.
Wizara inatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huu.
Vilevile, Wizara inapenda kuuhakikishia umma pamoja na Diaspora wa Kitanzania ikiwemo wanafunzi waliopo masomoni nchini Israel kuwa, Serikali kupitia Ubalozi wake uliopo Tel Aviv, Israel, itaendelea kuwasiliana na Mamlaka za Israel ili kuhakikisha Watanzania wote waliopo nchini humo wanakuwa salama wa kati wote.