Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwenyekiti wa AGN asisitiza umoja wa Afrika majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi

Ujerumani. Mwenyekiti wa Jopo la Wajadiliani wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN), Dk Richard Muyungi, amesisitiza umuhimu wa umoja wa bara la Afrika katika majadiliano ya kimataifa kuhusu tabianchi.

Akizungumza Juni 12, 2025 wakati wa ufunguzi wa kikao cha maandalizi cha AGN kabla ya kuanza kwa mkutano wa 62 wa Bodi Shirikishi za Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC - SB62), unaofanyika Bonn, Ujerumani, Dk Muyungi alisema “umoja ni kipengele muhimu katika majadiliano ”.

Akinukuu mchambuzi Florian Weiler, Dk Muyungi alieleza kuwa nguvu ya nchi katika majadiliano ya UNFCCC hupimwa kwa ukubwa wa uchumi, hadhi ya kimataifa, na kiwango cha uzalishaji wa gesijoto. Alibainisha kuwa nchi za Afrika kwa kujitegemea zina nguvu ndogo katika vipengele hivyo, hivyo AGN imeundwa kuleta msimamo wa pamoja ili kuimarisha ushawishi wa bara zima.

“Umoja huu hutusaidia kuepuka misimamo inayokinzana, kupunguza nafasi ya mataifa ya nje kuyachochea baadhi ya nchi za Afrika kwa maslahi yao binafsi, na kuwezesha Afrika kuwa na sauti moja yenye nguvu kwenye majadiliano ya kimataifa,” alisema Dk Muyungi.

Aliongeza kuwa AGN imekuwa chombo muhimu cha kiufundi kinachowasiliana na Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira wa Afrika (AMCEN) hadi Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC). Kwa kupitia jopo hili, Afrika imefanikiwa kushinikiza ajenda kama fedha za tabianchi, uhimilivu, na ujenzi wa uwezo kwa nchi zinazoendelea.

Dk Muyungi pia alisisitiza msimamo wa AGN wa kutilia mkazo hatua za uhimilivu (adaptation) kama njia kuu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema msimamo huu umechangia kwa kiasi kikubwa kuipa kipaumbele ajenda ya uhimilivu katika mazungumzo ya UNFCCC, ikiwa ni pamoja na kutambuliwa kwa lengo la kimataifa la uhimilivu kupitia Mkataba wa Paris.

Kuhusu vipaumbele vya Afrika katika kikao cha SB62, AGN imeweka mbele masuala ya uhimilivu, fedha za tabianchi, mpito wa haki (Just Transition), kupunguza uzalishaji, upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, na utekelezaji wa Mission 300.

“Ukosefu wa nishati Afrika umechangia changamoto katika afya, kilimo, uzalishaji viwandani, na hata uwezo wetu wa kukabiliana na athari za tabianchi. Hivyo, tunapaswa kusisitiza miradi yetu ya upatikanaji wa nishati safi kama sehemu ya mjadala wa maendeleo endelevu na hatua dhidi ya tabianchi,” alieleza Dk Muyungi.

Mission 300 ni mpango wa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika unaolenga kuwafikishia umeme watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030. Mradi wa nishati safi ya kupikia unalenga kuboresha sekta ya kupikia kwa nishati safi kwa kushirikisha sekta binafsi na kuongeza upatikanaji wa suluhisho nafuu za kupikia, hasa maeneo yasiyohudumiwa ipasavyo. Miradi hii ilipitishwa rasmi na Umoja wa Afrika Februari 2025 chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

“Katika mkutano wetu wa kimkakati uliofanyika Zanzibar Aprili, tuliamua kuhakikisha miradi hii miwili inaingizwa kikamilifu katika programu za mpito wa haki na kupunguza uzalishaji,” alihitimisha Dk Muyungi.

Vipaumbele vingine vinavyojadiliwa ni pamoja na  Kukamilisha mkakati wa Afrika kwa awamu ya tatu ya Mchango wa Kitaifa (NDCs 3.0),  Utekelezaji wa lengo jipya la kifedha la kimataifa kuhusu tabianchi na Kupiga hatua kwenye utekelezaji wa lengo la kimataifa la uhimilivu (Global Goal on Adaptation).

Vilevile kulinda msimamo wa haki wa Afrika katika maeneo kama hasara na uharibifu (loss and damage), uhamishaji teknolojia, na mfumo wa uwazi (transparency framework) na kutambua rasilimali za asili za Afrika kama fursa ya kuchochea maendeleo ya kijani na kupunguza gesijoto kwa kiwango cha kimataifa.

Mkutano huu unatarajiwa kuanza 16 Juni hadi 26, 2025 ikiwa ni maandalizi ya mkutano mkubwa wa COP30 utakaofanyika Novemba mwaka huu.