Mwenyekiti Chaumma Kilimanjaro ahojiwa na Takukuru

Gervas Mgonja akiwa katika Ofisi za Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro.
Muktasari:
- Mwenyekiti huyo amethibitisha kuitwa na Takukuru na kueleza kuwa alitoa maelezo kuhusu kauli yake, aliyodai inalenga kuibua mjadala wa maadili katika siasa.
Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Mkoa wa Kilimanjaro, Gervas Mgonja amehojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, kufuatia kauli aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara akimtuhumu Mbunge wa Same Magharibi, Dk David Mathayo kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kauli hiyo, ambayo video yake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, inadaiwa kutolewa na Mgonja Juni 14, 2025, katika viwanja vya Kwasakwasa, Same Mjini, wakati wa mkutano wa operesheni ya Chaumma ya C4C.
Akizungumza baada ya kuhojiwa leo Juni 27, 2025, Mgonja amethibitisha kuitwa na Takukuru na kueleza kuwa alitoa maelezo kuhusu kauli yake, aliyodai inalenga kuibua mjadala wa maadili katika siasa.
“Ni kweli nilipokea wito wa kuhojiwa kutoka kwa Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Same, nikielekezwa kukutana na maofisa kutoka Dodoma. Nilifika katika ofisi za Takukuru hapa Moshi na tumezungumza kuhusu kauli yangu ya Juni 14, nilipotaja kuwepo kwa vitendo vinavyoashiria rushwa vinavyofanywa na Mbunge wa Same Magharibi,” amesema Mgonja.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Mussa Chaulo amesema hatua ya kumuhoji Mgonja ililenga kupata ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo alizotoa kwenye mkutano wa hadhara.
“Ni kweli tumemuita Mgonja kwa ajili ya kumhoji kuhusu kauli yake aliyotoa kwenye mkutano wa hadhara, ambapo alimhusisha Dk David Mathayo na madai ya kutoa rushwa ya Sh50,000 kwa wajumbe wa kura za maoni katika mchakato wa ndani wa CCM,” amesema Chaulo.
Kwa sasa, haijajulikana iwapo hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa kufuatia mahojiano hayo, lakini Takukuru imeeleza kuwa inafuatilia kwa karibu taarifa zote za tuhuma za rushwa zinazoibuliwa na viongozi wa kisiasa.
Tukio hilo limekuja wakati ambapo siasa za ndani ya vyama vya siasa nchini zikipamba moto kuelekea uchaguzi mkuu ujao, huku viongozi mbalimbali wa kisiasa wakionekana kuchukua hatua za mapema kujipanga ili kuhakikisha wanapata ushindi.