Mganga mfawidhi, muuguzi wahukumiwa kwa matumizi mabaya ya nyaraka, malipo hewa

Muktasari:
- Ubadhirifu wa Sh586, 200 za mwajiri wawaponza muuguzi na mganga mfawidhi, wafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kulipa faini pamoja na kurejesha fedha walizotumia kinyume cha sheria.
Kigoma. Mahakama ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, imewahukumu kulipa faini muuguzi na mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Mtendeni baada ya kupatikana na hatia ya kutumia vibaya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wao.
Waliohukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh1,000,000 ni muuguzi Onesmo Janks (34) na aliyekuwa mganga mfawidhi Annie Newton (37) wa kituo hicho.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 19, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko, Ambilike Kyamba, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kyamba alisema kuwa watuhumiwa wamehukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh1,000,000, ambapo mshtakiwa wa kwanza, Newton, anatakiwa kulipa Sh700,000, na mshtakiwa wa pili, Janks, anatakiwa kulipa Sh300,000.
Aidha, Mahakama iliagiza kuwa kiasi cha Sh586,200 kilichohusiana na ubadhirifu huo kirejeshwe na kuingizwa katika akaunti ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).
Watuhumiwa wote walitekeleza maagizo hayo kwa kulipa faini ya Sh1,000,000 mahakamani hapo, pamoja na kurejesha kiasi cha Sh586,200 katika akaunti ya DPP, na hivyo wakaachiwa huru mara baada ya kutimiza masharti ya hukumu hiyo.
Awali, ilidaiwa kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo Desemba 2023, wakati wakitekeleza majukumu yao katika Kituo cha Afya Mtendeli, kwa kufanya malipo hewa.
Walitengeneza hati ya malipo iliyoonyesha kuwa wamenunua betri ya sola aina ya N200 yenye thamani ya Sh586,200, ilhali fedha hizo walizitumia kwa matumizi yao binafsi.
Shauri hilo la Uhujumu Uchumi namba ECO 9652 la mwaka 2025, liliwasilishwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kigoma, Jackson Lyimo ambapo ilielezwa kuwa watuhumiwa walikabiliwa na makosa mawili ya jinai.
Mashtaka hayo ni pamoja na matumizi mabaya ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kwa kufanya ubadhirifu na ufujaji wa mali za umma, kinyume na vifungu vya 22 na 28(1) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329.
Aidha, walikabiliwa na shtaka la kughushi nyaraka, kinyume na vifungu vya 333, 335(a), na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, toleo la mwaka 2022.