Wauguzi wapaza sauti wingi wa majukumu, WHO wakitoa ripoti

Muktasari:
- Ripoti mpya ya WHO (State of the world’s nursing 2025 report) inaonyesha nchi za kipato cha chini zinaongeza idadi ya wahitimu wa uuguzi kwa kasi kubwa zaidi, kuliko zile za kipato cha juu, hali inayojitokeza pia nchini Tanzania.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wauguzi, Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna) kimepaza sauti kuhusu upungufu wa watumishi wa kada hiyo nchini kufikia asilimia 52 kutoka 47 iliyokuwapo miaka miwili iliyopita.
Wakati Tanna ikilalama kuhusu upungufu huo, Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa ripoti mpya inayoonyesha nchi masikini zinazalisha wahitimu wengi wa kada hiyo, lakini idadi yao haiakisi utoaji huduma kutokana na wingi wa watu na ukosefu wa ajira.
Pamoja na kuwapo kwa upungufu huo, nchini asilimia 80 ya huduma katika vituo vya afya na hospitali, hutolewa na kada hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 12, 2025, rais wa Tanna, Alexander Baluhya amesema upungufu wa waajiriwa kada ya uuguzi unaweza kuwa ni mkubwa kama ambavyo ripoti mpya ya WHO inaonyesha.
“Mfumo wa utoaji wa huduma za afya, taaluma nyingine angalau wao wanaweza wakaingia kazini mmoja akahudumia watu wengi, lakini muuguzi inamtaka awepo kazini kwa saa 24 kwa maana katika uchache uliopo, wanajigawa mara tatu, hii inafanya kuwe na idadi ndogo inayohudumia wagonjwa wengi,” amesema.
Kauli ya Baluhya inaungwa mkono na ripoti hiyo, iliyoeleza kutokuwepo kwa usawa katika nguvu kazi ya wauguzi duniani, namna kunavyowaacha watu wengi bila huduma muhimu za afya.
“Ripoti hii ina habari za kutia moyo, ambazo tunapongeza nchi zinazopiga hatua,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus. “Hata hivyo, hatuwezi kupuuza ukosefu wa usawa unaoikumba sekta ya wauguzi duniani. Katika maadhimisho ya siku hii muhimu, nawahimiza nchi na washirika kuitumia ripoti hii kama ramani inayoonyesha tulikotoka, tulipo sasa na tunapopaswa kuelekea, kwa haraka iwezekanavyo.”
Kwa mujibu wa Baluhya, mgonjwa mmoja anaweza akahitaji kuonwa na muuguzi mara tatu mpaka nne kwa zamu moja, hivyo kuongeza mzigo mkubwa kiutendaji.
Amesema pamoja na jitihada ya Serikali kuongeza ajira, bado upungufu ni mkubwa. Kwa sasa wanaona umeongezeka kufikia kwenye asilimia 52 kutoka asilimia 47 miaka miwili iliyopita, akifafanua kuwa hiyo imetokana ongezeko la vituo vya afya vilivyojengwa hivi karibuni.
“Serikali imejenga vituo vingi, lakini bado haijaendana na miundombinu na vituo vya afya. Changamoto kubwa ni upungufu wa wauguzi sababu zile huduma nyingi zinazoonekana kwenye vituo zinatolewa na wauguzi, anaingia asubuhi mpaka jioni anahudumia wagonjwa zaidi ya 50 mtu mmoja.
“Mfano mgonjwa anahitaji kupewa dawa mara tatu mpaka nne kwa siku, hivyo mgonjwa mmoja ni lazima aonwe mara nne na muuguzi kwa dawa pekee,” amesema.

Baluhya amesema hiyo inaathiri hata utoaji bora wa huduma za afya maana muuguzi hutoa kipaumbele kwenye huduma za msingi ili kuokoa maisha.
Hali hiyo huwafanya baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa wanahitaji huduma zaidi ya hiyo, matokeo yake ikaonekana wauguzi hawatimizi majukumu yao.
“Ndiyo sababu tunalilia mazingira yetu yaboreshwe. Tuna mazingira magumu hususan kwenye halmashauri na wilaya usalama si mzuri matukio ya kujeruhiwa na maeneo ya makazi, muuguzi anatoka mbali asafiri afike afanye kazini, atoke usiku ni changamoto Serikali iliangalie hili na wapewe kipaumbele,” amesema Bahulya.
Ripoti
Katika maadhimisho haya, WHO na washirika wake leo imezindua ripoti ya Hali ya Uuguzi Duniani 2025, na kuwasilisha matokeo makuu na vipaumbele vya sera za kimataifa.
Ripoti inaangazia kutokuwepo kwa usawa katika nguvu kazi ya wauguzi duniani, kunawaacha watu wengi bila huduma muhimu za afya, jambo linaloweza kuhatarisha maendeleo kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, usalama wa afya duniani, na malengo ya maendeleo yanayohusiana na afya.
Ripoti hii mpya, inatoa uchambuzi wa kina na wa kisasa kuhusu nguvu kazi ya wauguzi katika ngazi ya dunia, kanda na nchi.
Kwa kutumia taarifa kutoka nchi wanachama 194 wa WHO, ushahidi unaonyesha hatua ya kupunguza uhaba wa wauguzi duniani kutoka milioni 6.2 mwaka 2020 hadi milioni 5.8 mwaka 2023, na inakadiriwa kushuka hadi milioni 4.1 kufikia mwaka 2030.
Hata hivyo, maendeleo haya kwa ujumla yanaficha tofauti kubwa za kikanda, takriban asilimia 78 ya wauguzi wote duniani wako katika nchi zinazowakilisha asilimia 49 tu ya idadi ya watu duniani.
Nchi za kipato cha chini na cha kati zinakumbwa na changamoto ya kuhitimu, kuajiri na kuwahifadhi wauguzi katika mifumo ya afya, na zitahitaji kuongeza uwekezaji wa ndani ili kuunda na kudumisha ajira.
Wakati huohuo, nchi za kipato cha juu zinapaswa kujiandaa kushughulikia viwango vya juu vya wauguzi wanaostaafu na kutathmini utegemezi wao kwa wauguzi waliopata mafunzo nje ya nchi, kwa kuimarisha mikataba ya pande mbili na nchi wanazowachukua wauguzi.
Ripoti ya State of the World’s Nursing 2025 (SoWN), inaonyesha tofauti tata kati ya nchi, kanda na mazingira ya kijamii na kiuchumi. Data na ushahidi uliokusanywa vinakusudiwa kusaidia mazungumzo ya nchi binafsi ili kutafsiri matokeo hayo kuwa sera na vitendo.
“Tunaikaribisha ripoti ya SoWN 2025 kama hatua muhimu ya kufuatilia maendeleo ya kuimarisha na kusaidia sekta ya wauguzi kuelekea malengo ya afya ya dunia,” anasema Pam Cipriano, Rais wa Baraza la Kimataifa la Wauguzi. “Ripoti hii inaonyesha wazi ukosefu wa usawa unaokwamisha taaluma ya uuguzi na kuwa kikwazo kwa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.”
Uzinduzi huo rasmi umeambatana na mijadala ya kitaifa na kikanda inayolenga kuangazia takwimu na maarifa katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa UN, idadi ya wauguzi duniani imeongezeka kutoka milioni 27.9 mwaka 2018 hadi milioni 29.8 mwaka 2023, lakini kuna tofauti kubwa katika upatikanaji wa wauguzi kati ya maeneo na nchi mbalimbali.
“Masuala ya jinsia na usawa bado ni ya msingi katika sekta ya wauguzi. Wanawake wanaendelea kutawala taaluma hii, wakiwa ni asilimia 85 ya wauguzi wote duniani.” imeeleza ripoti hiyo.
Takwimu zinaonyesha kuwa mmoja kati ya kila wauguzi saba duniani na asilimia 23 katika nchi za kipato cha juu wamezaliwa nje ya nchi wanazofanyia kazi, hali inayoonesha utegemezi wa uhamiaji wa kimataifa. Kinyume chake, asilimia ni ndogo zaidi katika nchi za kipato cha juu (asilimia 8), kipato cha kati cha chini (asilimia 1), na kipato cha chini (asilimia 3).
Nchi za kipato cha chini zinaongeza idadi ya wahitimu wa uuguzi kwa kasi kubwa zaidi kuliko zile za kipato cha juu. Hata hivyo, katika nchi nyingi, mafanikio hayo hayajaweza kubadilika utoaji huduma, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu na fursa chache za ajira.
Ili kushughulikia hili, nchi zinapaswa kuwaajiri ili kuhakikisha wahitimu wanapata kazi, wanaunganishwa kwenye mfumo wa afya na kuboresha mazingira ya kazi.
Julai 6, 2024 akitoa maoni kwenye kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Profesa Abel Makubi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), iliyopo jijini Dodoma alisema wauguzi wengi wanazalishwa lakini wanaishia mtaani.
"Ajira ni changamoto kubwa sekta ya afya, tunao zaidi ya madaktari 3,000 na manesi 25,000 hawana ajira, hili suala linaniogopesha sana. Lazima tuweke mikakati katika dira ijayo, hawa watu wasiendelee kuzagaa katika jamii yetu hii ionekane kwenye dira yetu," alisema.