Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mhagama aondoa hofu wananchi, asema Serikali ina dawa za kutosha

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama

Muktasari:

  • Serikali imesema kuna uhakika wa dawa za kutosha kwa magonjwa yote nchini, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu afya zao.

Dodoma. Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amewatoa wananchi wasiwasi kuhusu upatikanaji wa dawa za magonjwa mbalimbali nchini kutokana na kusitishwa kwa misaada ya dawa kutoka Marekani na kusema kuwa kuna dawa za kutosha, zikiwemo za malaria, Ukimwi, na magonjwa mengine.

Mhagama ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa, Aprili 25, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani, ambayo huadhimishwa Aprili 25 kila mwaka.

Amesema agizo la kusitishwa kwa misaada ya dawa iliyofanywa na serikali ya Marekani limeathiri mataifa mengi hasa kwenye sekta ya afya kwa ujumla wake.

Hata hivyo, waziri huyo amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali chini ya juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, hali ya usalama kwa maana ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini kwa magonjwa uko vizuri.

Amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wamefanya tathmini ya kina, wameangalia akiba ya dawa na vifaa tiba iliyopo, walichokiagiza na wanachotarajia kupokea, na tayari wameshaweka mpango mkakati wa muda mfupi, kati na mrefu.

Mipango hiyo inalenga kuhakikisha wagonjwa, bidhaa zote zinazohusiana na magonjwa ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yanapata ufadhili kutoka nje, hakutakuwa na tatizo lolote, ikiwemo dawa za malaria.

Amesema dawa za malaria, ikiwemo vitendanishi, vipo vya kutosha kutumika hadi Februari mwaka 2026.

"Kwa dawa nyingine kama dawa za Ukimwi na dawa nyingine, tayari tumeshachukua hatua, mpaka sasa tuna utoshelevu wa kutupelekea mpaka mwezi wa sita, na tumeshapata fedha kutoka serikalini katika mpango wetu wa muda mfupi.

"Tulishafanya tathmini ya mahitaji yetu na tayari tumeshapokea Sh93 bilioni kutoka serikalini na tumeshaagiza dawa za magonjwa mengine yote ambayo yalikuwa yanafadhiliwa na miradi hiyo," amesema Mhagama na kuongeza kuwa:

"Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwenye eneo hili muondoe shaka, tuko salama, tumejipanga na tunamshukuru Rais kwa uongozi wake, lakini tunashukuru Serikali yetu kuturuhusu kuangalia, kufanya tathmini kujua mapungufu na kuchukua hatua za haraka.

“Kwa hiyo, nawaomba wananchi watulie, hatuna upungufu, hatutapata matatizo na tunaendelea kujipanga," amesema.

Amesema watakaposoma bajeti ya Wizara ya Afya wataangalia afua zilizokuwa zinatekelezwa na taasisi za kimataifa, ambapo kazi yao kubwa itakuwa ni kuona afua ipi iunganishwe na afua zilizokuwa zinatekelezwa na serikali moja kwa moja.

Amesema kwa upande wa watumishi, wataangalia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, watafanya tathmini kuona watafanya nini, upatikanaji wa bidhaa tiba bajeti itaona watafanya nini ili waweze kujikimu.

Amesema kila siku Rais anataka kupata ripoti ya mwenendo wa wizara kwenye eneo hilo, na wamekuwa wakiandaa ripoti na kuikabidhi kuhakikisha tuko salama na hakutakuwa na matatizo yoyote.

"Kwa hiyo, yapo mambo mbalimbali ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi na kama nilivyowaambia, Ofisi ya Waziri Mkuu ilipewa kazi na Rais ya kuturatibu sekta zote na tumejiratibu vizuri nchini na taarifa hizo tumeendelea kuwa nazo, tunaendelea kuziboresha, lakini tunaendelea kufuatilia na jukumu kubwa kwa sasa ni ufuatiliaji wa siku kwa siku kuhakikisha nchi ipo salama hasa kwenye maeneo ya hizo programu tulizokuwa tunafadhiliwa na mataifa," amesema Mhagama.

Kwa upande wa hali ya ugonjwa wa malaria nchini, Mhagama amesema maambukizi yamepungua kwa asilimia 45, kutoka asilimia 14.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2024.

Amesema upungufu huo umetokana na Serikali kuweka jitihada kubwa kwenye kuthibiti na kutibu ugonjwa huo, pamoja na kupuliza dawa kwenye mazalia ya mbu.

Amesema pia vifo vitokanavyo na malaria vimepungua kutoka 2,460 mwaka 2020 hadi 1,503 mwaka 2024, ambapo ni sawa na asilimia 39, na kupunguza idadi ya wagonjwa wa malaria kutoka milioni sita mwaka 2020 hadi kufikia milioni 3.3 mwaka 2024, sawa na asilimia 45.

Aidha, ametaja mikoa inayoongoza kwa kuwa na maambukizi makubwa ya malaria kuwa ni Tabora wenye asilimia 23, Mtwara (20), Kagera (18), Shinyanga (16), na mkoa wa Mara (15), huku mikoa yenye kiwango cha maambukizi chini ya asilimia moja ikiwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Songwe, Mwanza, Dar es Salaam, Iringa na Singida.

Akizungumza katika mkutano huo, kaimu mkuu wa programu kutoka Wizara ya Afya, Samweli Lazaro, amesema dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs) zipo za kutosha hadi Desemba 2025.