Mwenge wa Uhuru waweka jiwe na msingi Daraja la Upinde wa Mawe Siha

Wakazi wa Kijiji cha Munge, Wilaya ya Siha wakishuhudia uwekaji wa jiwe la msingi katika daraja. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Wakazi wa Kijiji cha Munge, wilayani Siha wameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja
Siha. Zikiwa zimepita siku mbili tangu Mwenge wa Uhuru uzinduliwe, wakazi wa Kijiji cha Munge wilayani Siha Mkoa wa Kilimanjaro waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara katika Daraja la Upinde wa Mawe kwa muda mrefu, wameshukuru njia hiyo kuanza kufanya kazi.
Daraja hilo lililokamilika kwa asilimia 96, limewekwa jiwe la msingi leo Aprili 4, 2024 na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mzava wakati alipokwenda kutembelea mradi huo uliojengwa na Serikali ambao ujenzi wake umegharimu Sh35 milioni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao, wamesema wakati wa msimu wa mvua, shughuli za kiuchumi zilikuwa zikisimama kijijini humo, huku wanafunzi wanaosoma Shule Msingi Munge wakikosa masomo kwa kukosekana kwa kivuko cha daraja.
Wakazi hao wamesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo ni neema ya pekee kwa kuwa wakati wa kipindi cha mvua walikuwa wakitaabika kwa kukosa huduma muhimu.
Florah Naimanlatayo, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, ameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja hilo.
Amesema ni faraja kubwa kwao kwa kuwa wanafunzi hawatakosa tena masomo kama ilivyokuwa hapo awali pindi mvua inaponyesha.
“Wakati wa kipindi cha nyuma, mvua ikinyesha watoto wetu walikuwa wanashindwa kwenda shule, walikuwa wanashindwa kuvuka upande wa pili kutokana na maji kufurika kwenye daraja, wakati mwingine mvua zikinyesha mfululizo tulikuwa tukilala njaa kwa kushindwa kwenda kununua mahitaji,” amesema Florah.
Dereva bodaboda, Abel Saruni amesema msimu wa masika alikuwa akishindwa kufanya shughuli yake ya bodaboda kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya barabara na daraja.
“Hii ni neema ya pekee kwetu, hili daraja tulilopata, tulikuwa tukipata changamoto ambayo hakuna mawasiliano ya upande mmoja na mwingine, watoto wetu walikuwa hawaendi shule kabisa wakati wa kipindi cha masika,” amesema Saruni.
“Hata mteja akikupigia ukamchukue, nilikuwa nashindwa kwa sababu maji yalikuwa ni mengi kwenye daraja hili.”
Diwani wa Viti Maalumu Siha Kusini, Lilian Mollel amesema ilifika mahali kutokana kukosekana kwa daraja, wanafunzi walikuwa wakishindwa kwenda shule na kukaa nyumbani kwa wiki nzima hadi maji yapungue.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuhakikisha wananchi wetu wa Munge wanapata daraja hili kwa ajili ya kurahisisha shughuli zao za kila siku,” amesema.
Awali, akisoma taarifa ya mradi huo wa daraja, mtendaji wa kijiji hicho, Winie Muro amesema mradi huo ambao umefikia asimilia 96, unatarajiwa kukamilika Aprili 30, 2024 ili kurahisisha shughuli za kijamii kwa wananchi.
“Mradi huu ulianza Septemba 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili 30, 2024, utakapokamilika utasaidia kuunganisha mawasiliano ya Kijiji cha Munge na Shule ya Msingi Munge ili kurahisisha huduma za kijamii kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Christopher Timbuka amesema Mwenge wa Uhuru ambao umekabidhiwa leo, Aprili 4 wilayani humo utakagua, kuweka mawe ya msingi na utazindua miradi sita yenye thamani ya Sh6.9 bilioni.
Amesema Mwenge huo utakaokimbizwa kilometa 196 wilayani humo, utakagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji na sekta nyingine.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mzava amesema ameridhishwa na mradi huo na kwamba wananchi watapata huduma nzuri kwa kuwa changamoto iliyokuwepo Serikali imeitatua.
Amesema azma ya Serikali ni kuona wananchi wake wanapatiwa huduma muhimu katika jamii ili waweze kufanya shughuli zao kwa ajili ya kujipatia kipato.
“Mkuu wa wilaya hapa pamefanyika kazi nzuri, asilimia 4 hii iliyobaki naomba imaliziwe ili wananchi hawa waendelee kupata huduma na waondokane na changamoto waliyokuwa nayo,” amesema.