Usafiri Daraja la Mpiji warejea

Magari yakipita upande mmoja wa daraja la Mpiji linalounganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani baada ya kufungwa kwa muda kupisha matengenezo ya shimo lililotokea darajani hapo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Picha na Erick Boniphace.
Muktasari:
- Usafiri wa Daraja la Mpiji linalounganisha mikoa ya Dar es Salaam kwenda Pwani umeanza kurejea huku vyombo vya usafiri vikipita kwa zamu.
Dar es Salaam. Daraja la Mpiji linalounganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani limeanza kupitika upande mmoja, baada ya kufungwa kwa saa kadhaa kupisha matengenezo ya shimo lilojitokeza mwanzoni mwa daraja hilo.
Kurejea kwa usafiri huo kunafuatia kauli ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyoitoa jana Desemba 8 akiwa mkoani Shinyanga, akitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kukarabati daraja hilo na likamilike jioni ya leo.
Jana, video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha uwepo wa shimo upande mmoja wa barabara hiyo, hali iliyofanya Serikali kuifunga kwa muda.
Leo Desemba 9, Mwananchi limefika eneo hilo na kushuhudia polisi wakiongoza magari kuvuka upande mmoja kwa zamu, huku upande mwingine Tanroads wakimalizia ujenzi wa kuziba shimo hilo.
Taarifa iliyotolewa na Tanroads leo imesema wamerejesha mawasiliano ya daraja hilo kupitia Bagamoyo baada ya kupata changamoto ya kumomonyoka kutokana na mvua za El Nino.
“Daraja lilifungwa jana Desemba 8, 2023 kwa ajili ya usalama wa wasafiri na limefunguliwa leo saa 12 asubuhi Desemba 09, 2023 baada ya watalaamu kufanya jitihada kutengeneza hitilafu iliyojitokeza,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema wameruhusu watumiaji wa barabara kutumia upande mmoja wa daraja baada ya matengenezo kukamilika huku timu ya wataalamu wa Tanroads na makandarasi wakiendelea kufanya matengenezo mengine ya haraka kurejesha hali yake ya awali na kulifanya liwe imara zaidi.
Baadhi ya watumiaji na wakazi wa jirani na daraja hilo, hawakusita kutoa maoni na ushauri wao huku wakishauri kujengwa kingo zenye urefu kiasi kutoka usawa wa daraja hilo.
"Changamoto hii kujitokeza katika daraja hili si mara ya kwanza kipindi Rais John Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi hali hiyo ilitokea na palifungwa wiki moja baada ya upande wa pili kutitia na kujitokeza shimo," amesema Makoye Casmir mkazi wa eneo hilo kwa miaka 20 sasa.
Amesema eneo hilo kiasili ni oevu na lina mchanga zikijengwa kingo hizo zitasaidia hata maji yakiwa mengi kupita.
"Sasa hivi mto ni mkubwa na unazidi kuongezeka kutokana na mvua zinazoendelea na maji yanapokuja yanaenda moja kwa moja kugonga kwenye nguzo za daraja na kusababisha nyufa zinazoleta mashimo," amesema
Dereva wa daladala, Ramadhan Said amesema Serikali inapaswa kuweka ulinzi mkali eneo la daraja hilo na kuzuia watu kuchimba mchanga karibu kwa kuwa imekuwa chanzo cha kuendelea kupanuka mto huo.