Serikali yaanza kushughulikia changamoto ya kukatika Daraja la Somanga

Dar es Salaam. Wakati Daraja la Somanga likikatika na kukata mawasiliano ya Barabara ya Somangafungu, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema Serikali inafanya jitihada za kuyarejesha kabla ya mchana.
Jana Jumapili Machi 24, 2024 daraja hilo linalounganisha barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam na mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara lilikatika na kusababisha magari yanayotoka maeneo hayo kukwama njiani.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwapo eneo hilo wamesema daraja hilo limekatika juzi Jumamosi Machi 23, 2024 saa 2 usiku na kusababisha adha kwa watumiaji.
Hata hivyo, Waziri Bashugwa amewapa matumiani watumiaji wa barabara hizo akisema, “jitihada kubwa zinaendelea la kurudisha mawasiliano ya barabara eneo la Somangafungu, Lindi.”
“Teams za Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) mikoa ya Lindi na Pwani zimeungana kuongeza nguvu ili kabla ya mchana safari ziweze kuendelea, tunawapa pole wasafiri wote kwa changamoto iliyojitokeza,” amesema Waziri Bashungwa kupitia ujumbe wake wa mtandao wa Instagram.