Prime
Mwanzo, mwisho wa Papa Francis

Muktasari:
- Papa Francis amefariki dunia leo Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88. Kwa mujibu wa mtandao wa kijamii wa Vatican News, Papa Francis amefariki dunia akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta.
Dar es Salaam. Alipochaguliwa kuwa Papa Jumatano Machi 13, 2013 akiwa na umri wa miaka 76, Papa Francis alikuwa na afya njema.
Madaktari walisema tishu katika mapafu zilizoondolewa akiwa mdogo hazina athari kubwa kwa afya yake. Wasiwasi pekee ungekuwa kupungua kwa uwezo wa kupumua endapo angepata maambukizi ya njia ya hewa.
Papa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kudumu ya mapafu, jambo ambalo kwa sehemu limechangia afya yake kuzorota.

Katika miaka ya hivi karibuni amekuwa akipata matatizo ya mafua, kikohozi, maumivu ya koo na kifua wakati wa baridi.
Maumivu ya magoti na mishipa ya nyonga pia yamesababisha mara kwa mara atumie kitimwendo au mkongojo.
Mwaka 2021, matatizo ya afya ya Papa yalisababisha kuwapo uvumi huenda angejiuzulu, jambo alilolikanusha.
Juni 2022 baada ya matibabu ya magoti, Papa Francis aliahirisha ziara zilizokuwa zimepangwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini.
Katika mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) mwezi huo, alisema hakuwahi kufikiria kujiuzulu, lakini angeweza kufanya hivyo ikiwa hali yake ya afya ingemzuia kuongoza kanisa.
Wakati wa ziara DRC Februari 2023, alisema kujiuzulu haikuwa ajenda yake kwa wakati huo.

Machi 2023, alipelekwa hospitalini Roma kutokana na matatizo ya kupumua. Alirejea na kuadhimisha misa ya mkesha wa Pasaka. Juni mwaka huo, alifanyiwa upasuaji kutokana na uvimbe tumboni.
Tangu mwaka 2022, amekuwa akitumia kitimwendo kutokana na maumivu ya magoti yaliyohitaji upasuaji.
Maradhi ya mara kwa mara yalikuwa mwanzo wa kile alichoeleza: "Awamu mpya ya taratibu ya utawala wake."
Februari 14, 2025 alipelekwa Hospitali ya Gemelli, mjini Roma kwa matibabu yaliyotokana na athari kwenye mapafu (kichomi) kutokana na maambukizi ya bakteria.
Uchunguzi wa CT Scan ulionyesha kuanza kwa nimonia. Februari 21, afya yake ilianza kuimarika, kabla ya kuzorota tena kutokana na tatizo la muda mrefu la mapafu.
Habari zilizowekwa hadharani kutoka Vatican kuhusu hali ya Papa, zilielezea alikuwa amewekewa oksijeni kwa kiwango cha juu.
Februari 23, 2025 ilitangazwa kuwa Papa Francis alikuwa na tatizo katika mapafu, ingawa hali yake ilikuwa ikiendelea kudhibitiwa.
Siku ya 10 tangu alipofikishwa hospitalini, Februari 24, ilielezwa hali yake bado ilikuwa tete, ingawa iliimarika kidogo akiweza kula mwenyewe na alirejea kazini.
Februari 25, maofisa wa Vatican walisema alifanyiwa uchunguzi wa CT Scan.
Jioni ya Jumatatu, Machi 3, ofisi ya vyombo vya habari vya Vatican ilitoa taarifa kuhusu hali ya afya ya Papa Francis, ikieleza alikumbwa na vipindi viwili vya upungufu mkubwa wa hewa, hivyo kupatiwa huduma kwa msaada wa mashine.
Licha ya changamoto hizo, ilielezwa Papa alibaki mwenye fahamu, akitambua mazingira yake na kushirikiana na madaktari.
Vipimo vya damu havikuonyesha ongezeko la seli nyeupe, ishara kuwa hakuna maambukizo mapya, bali mkusanyiko wa kamasi ni matokeo ya ugonjwa wa mapafu aliokuwa nao awali. Machi 23, 2025 aliruhusiwa kutoka hospitali.
Papa Francis na Kanisa
Kiongozi huyu wa Kanisa Katoliki na Askofu wa Roma, alizaliwa Desemba 17, 1936 mjini Buenos Aires, Argentina na kubatizwa jina la Jorge Mario Bergoglio.
Ni Papa wa kwanza kutoka Shirika la Jesuit (Jumuiya ya Yesu), ni wa kwanza kutoka Amerika Kusini na wa pili kutoka nje ya Bara la Ulaya, akitanguliwa na Papa Gregori III, mzaliwa wa Syria aliyeshika wadhifa huo katika karne ya nane.

Bergoglio alipata msukumo wa kujiunga na shirika hilo mwaka 1958 baada ya kupona maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Alipadirishwa mwaka 1969. Kati ya mwaka 1973 hadi 1979 alihudumu akiwa mkuu wa Shirika la Jesuit nchini Argentina.
Mwaka 1998, aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires na baadaye mwaka 2001 aliteuliwa na Papa Yohane Paulo II (sasa Mtakatifu Papa Yohane Paulo II) kuwa Kardinali.
Aliongoza Kanisa Katoliki nchini Argentina wakati wa machafuko ya Desemba 2001. Utawala wa Nestor Kirchner na Cristina Fernandez de Kirchner ulimchukulia kama mpinzani wa kisiasa.
Baada ya Papa Benedicto XVI kujiuzulu Februari 28, 2013, Kardinali Bergoglio alichaguliwa kuwa mrithi wake Machi 13. Alichagua jina la Fransisko kwa heshima ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi.
Katika maisha ya uongozi kiroho, amejulikana kwa unyenyekevu na msisitizo kuhusu huruma ya Mungu. Kimataifa anatambulika kwa kuwajali maskini.
Alichagua kuishi kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta (Domus Sanctae Marthae) inayotumiwa na wageni, badala ya kuhamia katika makazi ya kipapa.
Amekuwa akipinga adhabu ya hukumu ya kifo, akiitaja kuwa ni uovu kwa asili, akieleza Kanisa Katoliki limejikita katika juhudi za kuifuta.
Katika diplomasia ya kimataifa, amehusika katika kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba, ameongoza makubaliano na China kuhusu ushawishi wa Chama cha Kikomunisti katika uteuzi wa maaskofu katika Taifa hilo na mtetezi wa wakimbizi.
Bergoglio hadi Francisco
Mwaka 1960, Bergoglio alipata Shahada ya Uzamili katika falsafa. Kati ya mwaka 1964 na 1966, alifundisha fasihi na saikolojia.
Mwaka 1967, Bergoglio alianza masomo ya theolojia. Desemba 13, 1969, alipewa daraja takatifu la upadri na Askofu Mkuu Ramon Jose Castellano. Aliteuliwa kuwa mwalimu na baadaye mhadhiri wa theolojia.
Julai 1973 aliteuliwa kuwa mkuu wa Shirika la Jesuit nchini Argentina alikohudumu kwa miaka sita hadi 1979.
Mwaka 1980 aliteuliwa kuwa mkuu wa Kitivo cha Falsafa na Theolojia, Buenos Aires, Argentina.
Mwaka 1992, Bergoglio aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Buenos Aires. Alipata uaskofu Juni 27, 1992.
Baada ya kifo cha Kardinali Quarracino kilichotokea Februari 28, 1998, akateuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires.
Katika wadhifa huo, alianzisha parokia mpya, akapanga upya dayosisi, akaendesha kampeni za kupinga utoaji mimba na aliunda tume maalumu kushughulikia masuala ya talaka.
Novemba 8, 2005, Bergoglio alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kwa muhula wa miaka mitatu (2005–2008). Alichaguliwa tena Novemba 11, 2008.
Desemba 2011 alipofikisha umri wa miaka 75, Bergoglio aliwasilisha kwa Papa Benedikto wa XVI barua ya kujiuzulu uaskofu mkuu wa Buenos Aires kama inavyotakiwa na sheria za kanisa. Hata hivyo, kwa kuwa hakukuwa na askofu mkuu aliyeteuliwa, aliendelea kuhudumu, akingojea Vatican kumteua mrithi wake.
Ukardinali
Jumatano Februari 21, 2001, Papa Yohane Paulo II alimteua Askofu Mkuu Bergoglio kuwa kardinali, nafasi aliyoanza kuitumikia Oktoba 14.
Baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II Aprili 2, 2005, Bergoglio alihudhuria mazishi yake na alihesabiwa miongoni mwa wale waliokuwa na uwezekano wa kuchaguliwa kuwa Papa.
Papa Francis alichaguliwa Jumatano ya Machi 13, 2013, siku ya pili ya makutano ya makardinali. Alipata ushindi katika duru ya tano ya upigaji kura.
Mwonekano wake wa kwanza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro alivaa vazi jeupe la kawaida, akiwa na msalaba wa chuma aliouvaa tangu akiwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires.
Adhimisho la misa katika wadhifa huo alilifanya Machi 19, 2013.
Uchaguzi wa jina
Machi 16, 2013, Papa Francis aliwaambia waandishi wa habari kwamba alichagua jina hilo kwa heshima ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, hasa kutokana na kuwajali maskini.
Hadi Februari 2025, Papa Francis ameteua makardinali 163 kutoka mataifa 76 katika mabaraza 10 ya makardinali.