Mwananchi yaandaa mdahalo wa ubunifu kidigitali

Muktasari:
- Mdahalo huo wa siku tatu utaanza kesho kwa njia ya mtandao kuanzia saa 8 hadi saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) kupitia idara yake ya ubunifu ya HabariHub imeandaa mdahalo kuhusu ubunifu wa kidigitali na tasnia ya habari kwa siku zijazo.
Waandaaji wengine wa kongamano hilo ni Mfuko wa Ubunifu na Maendeleo ya Binadamu (HDIF), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (UKaid), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo(UNDP) na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Mdahalo huo wa siku tatu utaanza kesho kwa njia ya mtandao kuanzia saa 8 hadi saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Litafanyika kwa njia ya mtandao. Wataalamu mbalimbali kutoka Marekani, Uingereza, Zambia, Kenya, Uganda na Tanzania watatoa na kuchangia mada.
Akizungumzia mdahalo huo uliodhaminiwa na Benki ya Absa na Kampuni ya Epiroc Mkuu wa Idara ya HabariHub Wilmore Mihayo amesema kutakuwa na mada tatu ambapo kila siku itakuwa ni mada moja kwa muda wa masaa mawili.
Mihayo amesema zitakuwa ni siku tatu kwa ajili ya tasnia ya habari kwani yataangaziwa mabadiliko ya tasnia hiyo katika suala la teknolojia, biashara na mahitaji ya mlaji sanjari na athari zake katika biashara, uendeshaji wa kila siku na mlaji wa maudhui hayo.
“Tutaanza na mabadiliko ya kimtazamo, elimu na mfumo wa ajira unavyohitaji kuvutia talanta katika karne ya 21, siku inayofuata itakuwa juu ya ukusanyaji wa habari kwa ajili ya majukwaa tofauti na stadi za muhimu kwa mwandishi wa habari wa karne ya 21 na siku ya tatu ni juu ya teknolojia muhimu katika mapinduzi ya viwanda ya awamu ya nne na athari zake kwa dunia ya sasa,” alisema.
Kwa yeyote atakayependa kushiriki ni bure lakini ni lazima kujisajili kupitia kiunganishi hiki https://events.habarihub.co.tz