Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwabukusi, Mpoki ngoma nzito kutetewa na mawakili nane

Dar es Salaam. Sakata la Wakili Boniface Mwabukusi limeendelea kuibua mapya baada ya juzi kulazimika kujitetea mwenyewe mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili iliyoketi chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Ntemi Kilekamajenga, baada ya wakili wake, Mpale Mpoki kusimamishwa uwakili kwa miezi sita.

Mbali na Mpoki, mawakili wengine sita waliokuwa wakimtetea waliamua kujitoa kwenye shauri hilo wakipinga mwenendo mzima wa kesi na kitendo cha mwenzao kusimamishwa katikati ya shauri.

Mpoki alisimamishwa uwakili Novemba 20 kwa kile kilichoelezwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kuwa “alikuwa akiweka mapingamizi,” jambo ambalo kamati ililikataa.

Mbali ya kukataa mapingamizi, TLS imedai kuwa mawakili hao walinyanyaswa kwa kupekuliwa wakati wanaingia kwenye ukumbi wa mahojiano, ilhali mawakili wa Serikali hawakukaguliwa.

Kesi hiyo imekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi kumshtaki Mwabukusi kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili kwa kile kilichodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu kupitia kauli zake za kupinga makubaliano ya uwekezaji katika bandari alizozitoa hivi karibuni.

Akizungumza jana na Mwananchi, Mwabukusi alisema alijitetea kwa saa 10, kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa moja kasoro usiku.

“Nimelazimika kujitetea mwenyewe, jana (juzi) sikupata wakili wa kunitetea. Nimewasilisha hoja zangu kuonyesha kuwa tuhuma hizo ni uongo na uzushi na kwamba mimi nilizungumza jambo ambalo lipo kisheria na wala si makosa. Ndiyo mambo ya msingi niliyowasilisha katika kamati hiyo yenye jopo la mawakili sita wa Serikali.

“Hakuna kanuni yoyote niliyovunja kuhusiana na kile nilichozungumza," alisema Mwambukusi.

Alisema mara baada ya kumaliza kujitetea walifunga ushahidi na uamuzi unatarajiwa kutolewa Januari, mwakani.


Wanane kumtetea Mpoki

Kwa upande mwingine, wakili Mpoki ameiomba Kamati ya Maadili ya Mawakili impatie nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi yake na pia amewasilisha notisi ya kukata rufaa dhidi ya adhabu aliyopewa ya kufungiwa kwa miezi sita.

Awali, alizungumza na Mwananchi akisema anashauriana na mawakili wake wanane watakaomtetea katika kesi hiyo.

“Kwa sasa bado nashauriana na mawakili wangu wanane ambao watasimamia kwenye jambo langu, hivyo vitu vingine nitaongea kesho (leo) na waandishi wa habari,” alisema Wakili Mpoki.

Juzi, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kilieleza kutoridhishwa na uamuzi wa kamati ya maadili ya mawakili ya kumsimamishi kazi Wakili Mpoki.

Kutokana na hali hiyo, taarifa iliyotolewa na TLS ilisema baraza lake la uongozi limemteua Wakili Mwandamizi Stephen Mwakibolwa kumwakilisha Wakili Mpoki katika kuandaa rufaa kupinga kusimamishwa uwakili.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Makamu wa Rais wa TLS, Deus Nyabiri alisema Mpoki hakupewa nafasi ya kujitetea katika kamati ya maadili ya mawakili kama sheria zinavyotaka.

“Sisi Chama cha Mawakili Tanganyika(TLS) hatukuridhika na ule uamuzi wa Jaji Ntime wa kumsimamisha wakili mwenzetu Mpoki kwa sababu yeye alichokuwa anaongea ni kwamba hakuridhika na uamuzi ambao jaji alikuwa ameutoa na kwamba alikuwa amepewa maelekezo na mteja wake (Mwabukusi) kukata rufaa.

“Sasa Jaji akamwambia wakili Mpoki kuwa unajua huu ni uamuzi ambao haumalizi kesi, lakini Mpoki alimwambia jaji kuwa anajua hivyo, lakini sheria inaruhusu kukata rufaa, sasa jaji akaona kwamba labda maelezo yamemuudhi au yamemkosea heshima, hivyo akaandika uamuzi wa kumsimamisha uwakili kwa kupindi cha miezi sita,” alisema.

Alisema taarifa waliyopewa na Wakili Mpoki ni kuwa hakupewa nafasi ya kujitetea ili kamati hiyo ione namna ya kutoa adhabu.

“Ubishi wa kisheria mahakamani ni jambo la kawaida, Jaji anaweza kukuambia umekosea hiki na wewe ukamwambia ‘mheshimwa jaji asijakosea kwa sababu nimesoma sheria hii na hii au nimesoma pia maamuzi ya mahakama nyingine haya na haya, hivyo mimi naona msimamo wangu huu upo sawa awa’, sasa mnavyofika hapo, jaji anaweza kusema kuwa sawa, nitatoa maamuzi,” alisema wakili Nyabiri.

Wakati Nyabiri akieleza hayo, Mwenyekiti wa Mawakili Vijana ndani ya TLS, Edward Heche alisema sheria hazikufuatwa kikamilifu kwa sababu wakati maamuzi yanafanyika aliyefanya maamuzi alifanya kama mwenyekiti, mwenyekiti wa kamati hana nguvu ya kumsimamisha wakili huyo.

Hii si mara ya kwanza kwa mawakili kufikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili wakilalamikiwa na Serikali.

Septemba 20, 2019 Fatma Karume alisimamishwa uwakili kwa madai ya kuishambulia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Fatma, aliyekuwa akimwakilisha Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu katika kesi ya kupinga kuteuliwa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adeladius Kilangi, alidaiwa kutoa maneno ya kuishambulia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, Juni 21, 2021 Mahakama Kuu Masjala kuu ilitengua uamuzi huo, baada ya Fatma kukata rufaa akipinga uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Mawakili.


Chadema yajitosa, yalaani

Katika taarifa yake iliyotolewa juzi jioni na kusainiwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, Chadema imeeleza kusikitishwa na hatua ya kusimamishwa kwa wakili Mpale Mpoki, aliyekuwa kiongozi katika jopo la utetezi wa Mwabukusi.

Chadema imesema hatua hiyo inaashiria kuwepo kwa nia ovu ya Serikali kupitia kwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika sakata hilo.

“Chama kinaona hilo si tishio tu dhidi ya Wakili Mwabukusi au Mpoki na jopo lote, bali ni tishio dhidi ya taaluma ya sheria na mawakili wote nchini na tishio dhidi ya vyombo vya otoaji haki nchini,” ilisema.