Mvua yaharibu mkongo wa mawasiliano

Muktasari:
- Ni mkongo wa njia tatu unaotumiwa na kampuni ya simu ya Tigo.
Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za simu ya Tigo imesema mvua zilizonyesha mwishoni mwa wiki iliyopita zimesababisha kukatika kwa huduma na kusababisha hasara kwa kampuni hiyo baada ya mawasiliano kukatika.
Kampuni hiyo imesema mvua hizo zimeharibu njia tatu za mkongo wa mawasiliano, hivyo kubakia na njia moja huku nyingine zikiwa zimesombwa na mafuriko yaliyotokea sehemu tofauti.
“Sisi tuna njia nne za mkongo, tatu ziliathirika tukabakia na moja, huduma za kupika simu ziliathirika kwa dakika 30 lakini huduma nyingine zilizopotea saa tatu usiku na kurejea mapema kesho yake,” amesema Emmanuel Malya, ofisa mkuu wa teknolojia na ufundi Tigo,
Hata hivyo, amesema changamoto hiyo ni funzo kwao kuendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kuwa na njia mbadala, ili kutoathirika pindi yanapotokea majanga yakiwemo ya asili.
Kwa upande wa uwekezaji katika miundombinu, Malya anasema ndani ya takribani miaka miwili kampuni hiyo imewekeza karibu Sh500 bilioni kwa ajili ya kuongeza ubora wa huduma na kufikisha huduma maeneo ambayo awali hazikuwepo.
“Malengo ni kuwekeza Sh1 trilioni ndani ya miaka mitano lakini mpaka sasa tumewekeza karibu nusu ndiyo maana ubora wa huduma zetu umepaa mpaka tumepata tuzo ya mtandao wenye kasi Zaidi ya intaneti Tanzania mwaka 2023,” amesema Malya.
Tuzo ya Tigo kuwa mtandao wenye kasi zaidi nchini ilitolewa na taasisi ya Ookla ambayo hupima ubora wa mtandao kimataifa kwa kuangalia kasi ya kupakia na kupakua data.