Mkongo wa mawasiliano intaneti kusimikwa mlima Kilimanjaro

Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akiwa pamoja na viongozi wengine akikata utepe wakati akizindua huduma ya internet katika Mlima Kilimanjaro (Data kileleni) katika lango la Marangu Mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ni miongoni mwa timu ya watu 49 walioanza safari ya kwenda kwenye kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro, kusimika mkongo wa mawasiliano ya intaneti.
Moshi. Timu ya watu 49 imeanza safari ya kwenda kwenye kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro, kusimika mkongo wa mawasiliano ya intaneti.
Timu hiyo ambayo imeanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro leo Ijumaa Desemba 9, 2022, inaongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ambapo usimikaji rasmi utafanyika Desemba 13, 2022.
Kabla ya Waziri Nape, kuzindua mradi wa usimikaji wa mawasiliano hayo katika kilele cha Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, alishuhudia utaji saini makubaliano ya miradi huo kati ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Waziri Nape amesema mawasiliano ya intaneti katika mlima huo itasaidia kurahisisha shughuli za mawasiliano katika uhifadhi pamoja na watalii wanaopanda mlima huo ambao wataweza kuwasiliana na familia zao popote walipo duniani na mpaka sasa Serikali imepata matangazo ya bure kote duniani.
“Shirika la Mawasiliano la Taifa( TTCL ) limefanikisha kujenga miundo mbinu ya mawasiliano ya intaneti kuanzia Marangu hadi Mandara Kilomita 9.5, Marangu hadi Horombo Kilomita 13, Horombo hadi Kibo Kilomita 14, Kibo hadi Uhuru Kilomita 5.2, Kibo hadi Barafu kilomita 3 na kufanya jumla ya kilomita kuwa 44.7 ,” amesema
“Leo ni siku muhimu kwa TTCL na Taifa kwa ujumla tunapoenda kushuhudia tukio la historia la uzinduzi wa intaneti katika kilele cha cha mlima Kilimanjaro tarehe 13 Desemba,2022 ambapo safari yetu inaanza leo katika geti la Marangu tutapita Mandara, Horombo, Kibo, Gilman's, Stella na hatimaye Uhuru,” amesema
Amesema tangu kuzinduliwa kwa huduma za mawasiliano awamu ya kwanza Agosti mwaka huu katika vituo vya Mandara, Horombo na Kibo mafanikio yake yameanza kuonekana ambapo watalii wameweza kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki kuonyesha uzuri wa vivutio.
Nape amesema amesema kuzinduliwa kwa mawasilianao hayo ya intaneti katika mlima huo, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kusimika huduma ya intaneti katika kilele cha mlima Kilimanjaro.
“Niwapongeze TTCL mmefanya sana kazi nzuri ya kizalendo na imeleta sura mpya hivyo tumekusudia kuzungumza na dunia tukiwa kileleni na kuiambia dunia 'roof' ya dunia ipo mlima Kilimanjaro,"amesema Waziri Nape
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema malengo ya wizara hiyo ni kukuza matumizi ya tehama ambapo serikali inatekeleza mkakati wa kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanaunganishwa kidigitali ifikapo mwaka 2025.
"Mapinduzi ya kidigitali ambayo yametokea leo yametokana na miundombinu ya mawasiliano yakimkakati, mkongo wa taifa wa mawasiliano ambao umeongoza kasi na ubora wa mawasiliano ikiwemo intaneti ambapo mahitaji yake yamezidi kuongezeka" amesema Msigwa na kuongeza
“Huduma hii itafungua fursa za kiuchumi katika hifadhi za mlima kilimanjaro na taifa letu kwa ujumla na pia huduma hii itaimarisha usalama wa watalii na kukiza kipato cha shirila letu."
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga amesema ubunifu huo unawapa moyo kuwa Watanzania wanao uwezo mkubwa kufanya mambo makubwa yanayogusa dunia.
"Huduma hizi ambazo tunazifikisha katika mlima Kilimanjaro ni mafanikio makubwa sana na inaonyesha ni jinsi gani nchi hii imepiga hatua katika matumizi ya kutumia mkongo wa taifa na kutumia teknologia za kidigitali," amesema Upanga
"Nina imani kubwa kabisa hapa tulipo tuna uwezo wa kuiambia Tanzania na Dunia kwamba shirika la mawasiliano la TTCL linaweza kutoka hapa kwenda mbele kubadilisha sura nzima ya mawasiliano katika nchi yetu," amesema