Prime
Msomi alivyokwaa kisiki kortini akipigania shahada ya uzamili

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, imeyakataa maombi ya aliyekuwa mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE), Athman Kitanga aliyekuwa akipinga kunyimwa vyeti vyake baada ya kuhitimu.
Kitanga alifungua maombi mwaka 2024 dhidi ya Bodi ya Utawala (Governing Board) ya CBE na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba Mahakama ipitie upya uamuzi wa bodi hiyo wa kumnyima vyeti vyake.
Muombaji ambaye alikuwa akitetewa na wakili Faraji Ahmed, alidai uamuzi wa kukataa kumpa nakala ya matokeo ya kitaaluma (transcript) na cheti baada ya kufaulu mitihani yake, ulitolewa na bodi hiyo ya utawala Februari 27, 2024.
Kitanga alisomea shahada ya uzamili au kwa maneno mengine Shahada ya Umahiri katika Tekinolojia ya Habari (IT) katika usimamizi wa miradi na alijiunga na chuo hicho mwaka 2021.
Kulingana na hati ya kiapo chake, mwaka 2023, muombaji alifanya mitihani yake ya mwisho na matokeo yalipotolewa, alibaini kuwa alikuwa amefeli somo moja la Project Management Tools and Techniques.
Hakuridhishwa na matokeo hayo hivyo akaamua kukata rufaa na kufanikiwa kuingizwa katika orodha ya wahitimu wa shahada hiyo ya Uzamili ambapo alihudhuria mahafali yaliyofanyika Novemba 10, 2023 akiwa kama muhitimu.
Baada ya mahafali, Kitanga aliandika barua kwenda Bodi ya Utawala ya CBE, akiomba kupatiwa vyeti vyake, lakini hata hivyo ombi lake hilo lilikataliwa kwa kile alichodai kuwa ni kisingizio cha makosa katika kusahihisha mitihani yake.
Aliandika barua nyingine akipinga uamuzi huo kutokuwa na mantiki ambapo alijibiwa na kutakiwa kuhudhuria kikao cha uchunguzi kilichofanyika Januari 22,2024 na uamuzi ukatoka Februari 27,2024 ukibatilisha matokeo ya somo hilo.
Uamuzi huo ulisababisha pia kufutwa kwa “Transcript” na cheti cha kuhitimu.
Wajibu maombi hawakupinga kwa kuwasilisha kiapo kinzani hivyo Jaji Hussein Mtembwa aliyesikiliza maombi hayo, alisema kisheria watawajibika tu kujibu masuala ya kisheria na sio maelezo yaliyomo katika kiapo cha Kitanga.
Hoja za kisheria
Kuhusu kama kilichofanywa na CBE ni haki, wakili Ahmed, aliirejesha mahakama katika kifungu cha 4 cha sheria ya CBE sura ya 315, kilichoipa bodi mamlaka ya kutawala na kukisimamia chuo wakati wa kutekeleza majukumu yake ya umma.
Wakili huyo alisema mamlaka ya kisheria iliyopewa Bodi ya CBE hawakupewa tu bila kujali sheria, akisema mamlaka za umma zinapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria ikiwamo haki ya asili inayotaka uwepo wa usawa.
“Uamuzi wowote wa kiutawala unaokiuka msingi wowote wa haki ya asili, unatakiwa kufutwa na mahakama,”alisema wakili huyo na kuongeza.
“Kwa kutazama kiapo cha mleta maombi, hakuna ubishi kuwa alifaulu mitihani yake na aliidhinishwa kuhudhuria mahafali ambayo alishiriki. Lakini hata hivyo baadaye akanyimwa vyeti kwa sababu kulikuwa na makosa kwenye usahihishaji.”
“Chuo kilienda mbali zaidi hadi kubatilisha taarifa ya matokeo yake,” alieleza wakili na kuirejesha mahakama katika kifungu cha 55(1) na (2) cha kanuni za mitihani ya CBE zilizotangazwa katika gazeti la Serikali (GN) namba 926 la mwaka 2023.
Wakili huyo alisisitiza chuo hakikuwa sahihi na kilitumia vibaya mamlaka yake chini ya kanuni hizo na kusababisha kufikia uamuzi usio na mantiki na wa kimakosa, wa kubatilisha ufaulu wake na kumnyima haki yake ya vyeti.
Alisema kanuni hizo ziko wazi namna ya kushughulikia malalamiko kuhusiana na mitihani na kwamba kama mwanafunzi haridhiki na matokeo anakata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya mitihani chini ya kanuni ya 34(1)(a).
Mwanafunzi huyo naye alitumia haki hiyo kukata rufaa na kufanikiwa na kosa la usahihishaji lililokuwa limeibuliwa na chuo lilirekebishwa na bodi ya taaluma chini ya kanuni ya 34(1)(c) na mleta maombi akaingizwa kuhudhuria mahafali.
Kwa mujibu wa wakili huyo, kulikuwa hakuna sababu za kutosha za kufuta “transcript” kulingana na Kanuni ya 55(1) na 38(2)(b) inayohusu mitihani ambazo zinataka kuwepo kwa sababu za kutosha kabla ya kufikia uamuzi huo.
“Uamuzi ungekuwa halali kama sababu zingehusu makosa ya mwanafunzi mwenyewe. Kwa mfano kuwasilisha taarifa za uongo kwa chuo, kufanya udanganyifu kwenye mitihani na sababu zinazofanana na hizo,”alisema wakili Ahmed.
Wakili huyo alimalizia hoja zake kwa kusema mteja wake alikuwa na matumaini ya kupewa vyeti vyake na ukweli kuwa chuo kilimhakikishia amefaulu, akapewa joho na akashiriki katika mahafali ya chuo.
Hoja za majibu ya CBE, AG
Akijibu hoja hizo kwa niaba ya bodi ya CBE na AG, wakili wa Serikali, Erigh Rumisha alisema maombi hayo hayana mantiki na yamekosa sifa hivyo akaiomba Mahakama isiyakubali na badala yake iyatupilie mbali.
Wakili huyo alieleza CBE ilimwandikisha Kitanga kwa ajili ya kusomea shahada hiyo ua uzamili lakini matokeo ya somo la BAM09117 ilionyesha mapungufu makubwa ya kitaaluma yanayoathiri uadilifu na ubora wa mitihani yake.
Ni kutokana na mapungufu hayo, bodi ya CBE inayo mamlaka ya kisheria ya kuchunguza dosari hizo, bila kujali chanzo chake au muda gani umepita tangu mwanafunzi amalize chuo au bado anaendelea na masomo.
“Lengo ni kudumisha uadilifu na ubora wa elimu inayotolewa mahsusi na CBE. Katika kuheshimu misingi ya haki ya asili, muombaji alipewa nafasi ya kuelezea kwa maandishi kuhusiana na mapungufu yaliyogundulika,” alieleza wakili.
“Zaidi ni kuwa Januari 22,2024 mleta maombi alialikwa na alifika mbele ya timu ya uchunguzi kwa ajili ya usikilizwaji wa wazi. Alishirikishwa katika hatua zote za uchunguzi na matokeo ya uchunguzi huo kwa barua ya Februari 27,2024,” amesema.
Wakili huyo alisema CBE ilifanya hivyo kwa dhamira njema na ili kuipima dhamira hiyo njema, waliiunda timu ya uchunguzi, wakamwalika mleta maombi, akaruhusiwa kuwasilisha utetezi na alijulishwa sababu ya kufuta matokeo.
“Muombaji alishirikishwa katika mchakato mzima. Misingi ya haki ya asili haikukiukwa kama anavyodai na matokeo ya uchunguzi na sababu za kufuta matokeo ziliwasilishwa kwake kwa barua ya Februari 27,2024,” alieleza.
Wakili huyo alipinga hoja kuwa kufutwa kwa matokeo hayo kulifanyika baada ya kuwa ameshahudhuria mahafali, akisisitiza kuwa hakuna muda maalumu kwa chuo chochote kufuta cheti endapo tu kutatolewa sababu zinazojitosheleza.
Hukumu ya Jaji
Katika hukumu yake aliyoitoa Mei 8,2025 na nakala kuwekwa katika mtandao wa mahakama jana Jumatano Mei 14,2025, Jaji Mtembwa alisema hoja za wakili wa mleta maombi kuwa hakukuwa na sababu za msingi kufuta matokeo hazina mashiko.
“Kwa maoni yangu, makosa yaliyoonyeshwa katika barua ya Januari 5,2024 yalitosha kuishawishi timu ya uchunguzi kuwa matokeo ya somo moja yalikuwa si sahihi na yalihitaji kufuta hadi nakala yenye matokeo ya kitaaluma,” alisema Jaji.
“Moja ya kosa ni kupewa alama 10 kwa swali ambalo jumla ya alama ilipaswa kuwa 5. Katika eneo lingine, msahihishaji wa ndani aligoma kutoa alama hususan katika swali la 3B na C na swali la 4,”alieleza Jaji katika hukumu hiyo.
“Kwa sababu hiyo, sikubaliani na wakili wa mleta maombi kwamba kulikuwa hakuna sababu za msingi za kufuta matokeo ya mtihani huo. Dosari hizo zilielezwa katika barua ya chuo ya Januari 5,2024,”amesisitiza Jaji Mtembwa.
“Wakili wa mleta maombi alijenga hoja kuwa makosa yaliyofanywa na chuo hayawezi kuhesabika kama yalifanywa kwa dhamira njema. Kama ingekuwa hivyo basi vyuo vitakuwa vinashindwa kufuta vyeti vinapogundua makosa.”
Jaji alisema baada ya kupitia sababu hizo na nyingine kwa ujumla wake, ameona maombi hayo hayana mashiko hivyo hawezi kuyaruhusu na kulingana na mazingira ya shauri lenyewe, kila upande utabeba gharama zake za kesi.