Gachagua azindua chama chake, risasi zarindima

Muktasari:
- Gachagua ambaye uteuzi wake katika nafasi ya Naibu Rais wa Kenya ilitenguliwa Oktoba 2024 amejikuta kwenye misuguano na Serikali ya Rais William Ruto. Miongoni mwa hatua alizochukua ni pamoja na kuanzisha chama chake cha Democracy for the Citizens Party (DCP).
Nairobi. Shughuli ya uzinduzi wa chama kipya kilichoanzishwa na aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua imeingia dosari baada ya watu ambao bado hawajajulikana kuvamia eneo ilipokuwa inafanyika shughuli hiyo.
Baada ya watu hao kufika eneo hilo leo Alhamisi Mei 15, 2025, jijini Nairobi, walinzi wa Gachagua walilazimika kupiga risasi hewani na kulifanya kundi hilo kurudi nyuma kisha kukimbia, huku wafuasi wa Gachagua wakiwafukuza kwa kutumia mawe na silaha za jadi.
Kipande cha video kilichowekwa leo Alhamisi Mei 15, 2025, na Dail Nation kinaonyesha walinzi na wafuasi wa Gachagua wakiwashambulia watu wanaodhaniwa kuwa wavamizi wa mkutano huo.
Gachagua baada ya uteuzi wake kutenguliwa, alitangaza kuanzisha chama kipya kinachoitwa Democracy for the Citizens Party (DCP) yaani Chama cha Demokrasia ya Wananchi.
Gachagua aliondolewa katika wadhifa wake wa Naibu Rais na Bunge la nchi hiyo Oktoba 2024.
Katika hafla iliyofanyika leo Alhamisi jijini Nairobi, Mei 15, Gachagua amezindua chama hicho atakachokitumia kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao wa 2027.
Gachagua amesema kuwa amekaa kwa muda wa miezi 6 iliyopita nyumbani kwake kufanya mashauriano ya kuunda chama chake cha kisiasa.
Amebainisha kuwa DCP kimeundwa katika msingi wa kutoa uongozi bora kwa Wakenya na kuwaondoa katika matatizo ya muda mrefu ya uongozi mbaya.
"Wakenya wametuambia kwa ujasiri kwamba wana suluhu ya matatizo yanayowakabili. Wakenya wametuomba tuanzishe chama ambacho kitaunda serikali kwa ajili ya wananchi," Gahagua amesema wakati wa uzinduzi wa chama hicho.
Uongozi wa chama cha Gachagua
Chama hicho kitaongozwa na Rigathi Gachagua, huku aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala akiwa Naibu kiongozi wa chama.
Malala alifukuzwa kama Katibu Mkuu wa chama tawala cha Rais William Ruto, UDA Desemba 2023.
Aliyekuwa Seneta wa Meru na Waziri wa Kilimo Mithika Linturi atakuwa Katibu Mkuu wa Kitaifa. Linturi alifukuzwa kazi na Rais Ruto mwaka jana baada ya maandamano ya vijana maarufu kama Gen Z.
Akiwa waziri alijipata kashfa Wizara ya Kilimo kuwapa Wakenya mbolea iliyokuwa chini ya kiwango.
Gachagua amesema kuwa chama cha DCP hakina wagombea wanaopendelewa na kitatanguliza sauti za Wakenya, hivyo basi kauli mbiu ya chama "Sikza Wakenya" ambayo inamaanisha "Sikiliza Wakenya."
Amesema kuwa chama hicho kinapenda ushirikishwaji na kimejumuisha wawakilishi kutoka makundi yote nchini kote, ikiwa ni pamoja na vijana maarufu kama Gen Z.
Gachagua ni nani?
Gachagua alikuwa Naibu Rais wa Kenya kuanzia mwaka 2022 hadi Oktoba 2024. Alikuwa mshirika wa karibu wa Rais Ruto wakati wa uchaguzi wa 2022, ambapo alisaidia kushinda kura nyingi kutoka eneo la Mlima Kenya.
Oktoba 2024, Gachagua aliondolewa madarakani kupitia mchakato wa kihistoria wa kumng'oa Naibu Rais kwa mara ya kwanza nchini Kenya. Bunge la Kitaifa lilipitisha hoja ya kumtimua kwa kura 281 dhidi ya 44, likimshutumu kwa makosa 11, yakiwemo ufisadi, uchochezi wa ukabila, na kuidharau serikali. Seneti ilithibitisha mashtaka matano, ikiwemo uvunjaji wa kiapo cha ofisi na kueneza chuki za kikabila.
Gachagua alikana mashtaka hayo, akiyataja kuwa ni "propaganda ya kisiasa," na alijaribu kuzuia mchakato huo mahakamani bila mafanikio. Baada ya kuondolewa, Rais Ruto alimteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki, kuwa Naibu Rais mpya, uteuzi uliothibitishwa na Seneti.
Kuondolewa kwa Gachagua kuliibua mjadala mkubwa kuhusu siasa za ndani ya chama tawala na mustakabali wa utawala wa Rais Ruto.