Gachagua amtuhumu IGP kuhusika majaribio ya kumuua, ampa masharti sita

Aliyekuwa makamu wa rais wa Kenya, Rigathi Gachagua
Muktasari:
- Rigathi Gachagua alikuwa makamu wa rais wa Kenya kabla ya bunge la nchi hiyo kupiga kura ya kumng’oa katika wadhifa huo. Gachagua amemtaka IGP kutekeleza mambo sita ili kuimarisha ulinzi wake.
Nairobi. Aliyekuwa makamu wa rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amemwandikia barua Mkuu wa Polisi nchini humo (IGP), Douglas Kanja akilalamika kuwepo majaribio kadhaa ya kumuua, huku mamlaka nchini humo zikishindwa kuchukua hatua dhidi ya wahusika.
Katika barua hiyo aliyoichapisha kwenye akaunti yake ya Mtandao wa X leo Jumanne Aprili 15, 2025, Gachagua ametaja majaribio kadhaa yaliyolenga kuondoa uhai wake, familia yake, watu wake wa karibu na uharibifu wa mali zake.
“Kama unavyofahamu, una jukumu la kikatiba la kulinda maisha na mali ya kila Mkenya kama ilivyoainishwa katika katiba ya Kenya ya mwaka 2010. Hata hivyo, katika hali hii, Kanja (IGP) unaendeleza uhalifu na ukatili kwa makusudi,” ameandika Gachagua.
Huku akitaja Kifungu cha 245 cha Katiba ya Kenya, hasa 245(2)(b) Gachagua amesema ni wajibu wa Jeshi la Polisi nchini humo kulinda usalama raia na mali zao, jambo ambalo anadai IGP huyo halitekelezi badala yake anaukingia kifua uovu unaotendwa na Serikali iliyoko madarakani.
“Iwapo umesahau, IG (Kanja) nilihudumu kama Mbunge wa Jimbo la Mathira kuanzia mwaka 2017 hadi 2022, kisha nikachaguliwa kwa tiketi ya pamoja na Rais William Ruto kuhudumu kama naibu rais wa pili wa Jamhuri ya Kenya kuanzia Septemba 13, 2022 hadi kufukuzwa madarakani kwa njia ya aibu mwaka 2024 kwa madai ya uongo yaliyoandaliwa na watu unaowafahamu vizuri.”
“Unafahamu vyema na ni jambo linalojulikana wazi kwamba suala hili bado liko mahakamani ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Kenya,”
Gachagua ameenda mbali na kudai kuwa uamuzi wa kumuondolea ulinzi uliofanywa na IGP huyo, ulikuwa wa makusudi na wenye njama za kumfanya awe katika hatari ya kushambuliwa na magenge ya kihalifu kwa kushirikiana na maofisa Polisi na vyombo vingine vya usalama, chini ya uratibu wa mkuu huyo wa polisi.
“Unafahamu kwamba; Novemba 28, 2024, katika ibada ya mazishi huko Limuru, Kaunti ya Kiambu, nilishambuliwa na magenge yaliyoandaliwa, magari yangu yakaharibiwa vibaya, wanawake na watoto wakapigwa, mali isiyojulikana ikaharibiwa, waombolezaji wakapigwa huku polisi wakitazama tu, hili lilikuwa jaribio la kuniua lililoshindikana.”
“Washambuliaji ambao picha zao na taarifa zao zilisambazwa mtandaoni kwa zaidi ya mwezi mmoja hawajachukuliwa hatua yoyote. Badala yake, wanasiasa na viongozi wanaonihusisha nao akiwemo Seneta Karungo Wa Thang’wa na aliyekuwa mbunge wa Limuru, Peter Mwathi wamekuwa wakiteswa na vyombo vya usalama kuhusu tukio ambalo unawajua vilivyo wahusika wake.”
“Desemba 28, 2024 huko Shamata, Kaunti ya Nyandarua, Ofisa wa Polisi akiwa ameandamana na magenge ya kihalifu alinirushia gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya wafuasi wangu na kutengeneza mazingira ya kunishambulia kwa nia ya kuniua. Ofisa huyo wa polisi unamfahamu vyema na bado hajachukuliwa hatua yoyote licha ya kusababisha taharuki na kujaribu kuniua,” ameandika Gachagua.
Katika jaribio lingine Gachagua, ametaja tukio la Januari 18, 2025 katika uwanja wa Kamukunji mjini Nyeri, wakati wa mkutano wa maombi ulioandaliwa na Mchungaji maarufu Maina wa OTC, ambapo mke wake, Mchungaji Dorcas Rigathi alipokuwa akihubiri, genge la wahalifu lilivamia mkutano huo wa maombi.
“Mke wangu alilazimika kuondolewa kwa haraka na walinzi wake binafsi. Polisi waliokuwa wamevaa kiraia walijiunga na wahalifu hao na hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa. Unafahamu kuwa nilikuwa niwepo kwenye mkutano huo na kutokana na taarifa ya kiintelijensia nilijiepusha kwa uamuzi wa busara ili kuzuia mzozo ambao unajua ungesababisha vurugu kwa taifa letu,” amedai mwanasiasa huyo.
Katika tukio lingine, Gachagua amesema Machi 23, 2025, katika Kanisa Kuu la ACK Mtakatifu Peters’ mjini Nyeri, magenge ya kihalifu yaliyoandaliwa na watu anaowafahamu IGP huyo yalivamia waumini wa Kikristo ambapo alihudhuria ibada ya Jumapili.
“Polisi walitazama tu vurugu hizo huku waumini wakidhalilishwa na magari kupigwa mawe ndani ya eneo la kanisa na nje. Tena, umekaa kimya kana kwamba hakuna kilichotokea,” ameandika Gachagua.
Mbali na hayo, Gachagua ametaja jaribio la kumuua la Machi 29, 2025 mjini Naivasha, ambapo amedai kikosi cha polisi chini ya uongozi wa Keter ambaye ni OCPD wa Naivasha, kikiwa kimejihami vikali, kilipiga na kudhalilisha wakazi wa Naivasha waliokusanyika kumpokea.
“Maofisa haohao wa polisi walinifuatilia hadi kituo cha biashara cha Mai Mahiu ambapo walishambulia wakazi kwa virungu na kurusha mabomu ya machozi kwa wananchi waliokuwa wakitaka kuzungumza nami. Bwana Douglas Kanja, kimya chako ni kikubwa mno,” ameeleza.
Pia, amedai Aprili 6, 2025, katika ibada ya kanisa la PCEA Kasarani East Parish, Mwihoko, Kaunti ya Nairobi, kundi kubwa la watu anaodai ni wahalifu waliojihami kwa silaha za jadi ikiwemo mapanga walivamia kanisani na kuwajeruhi waumini.
“Wanawake, watoto na waumini walikumbwa na ukatili mkubwa na hakuna hata ofisa mmoja wa polisi aliyefika licha ya kituo cha polisi kuwa mita chache kutoka kanisani. Unafahamu kuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi alikuwa ametoa maagizo kuwa hakuna ulinzi utakaotolewa.”
“Unajua vyema kuwa kumekuwa na mipango ya makusudi ya kuvamia nyumba zangu jijini Nairobi, Nyeri na mali yangu nchini kote na watu unaowafahamu au ambapo wewe mwenyewe ni mshirika wa njama hiyo. Utafanyaje hatua wakati ni wewe mwenyewe mshiriki?” amehoji Gachagua.
Ameenda mbali na kudai kuwa kuna maofisa usalama wanaomfuatilia kwa magari yenye namba za siri ama zisizosajiliwa ambapo ametaja tukio la Desemba 19, 2024 kuwa Ofisa wa NIS kwa namba ya gari feki alimfuatilia umbali wa zaidi ya kilomita 150 huko Makueni.
“Tafadhali elewa kuwa maofisa hawa wa NIS wamekuwa wakinifuatilia mimi na familia yangu kwa magari yasiyotambulika. Hili ni kosa dhidi ya haki ya faragha. Ni dhahiri kuwa ufuatiliaji huu wa NIS ni kiashiria kuwa wanashirikiana na magenge ya kihalifu ili kufuatilia mienendo yangu na kuniua,” ameandika Gachagua.
Katika waraka huo, Gachagua amehitimisha kwa kumtaka IGP kutekeleza mambo sita kuimarisha ulinzi wake ambayo ni kukamatwa mara moja na kufunguliwa mashitaka kwa wote waliohusika na vitendo vya kikatili.
Pia amemtaka IGP kumpatia ulinzi katika mikusanyiko yote ya umma anayohudhuria, kumpatia ulinzi binafsi mara moja, kuacha kuingilia mikutano ya amani ya raia, kusitisha mara moja ufuatiliaji na unyanyasaji wa maofisa wa NIS dhidi yake na familia yake na kulinda nyumba na mali zake.
“Iwapo jaribio lingine la kuniua au kutumia ukatili litafanyika, utawajibika binafsi kwa wananchi wa Jamhuri ya Kenya na kwa jumuiya ya kimataifa,” ameandika Gachagua.