Prime
Chanzo miamala ya simu kupungua miaka mitano mfululizo

Muktasari:
- Idadi ya miamala kwa watumiaji wa simu kwa mwaka imeshuka katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kutoka wastani wa miamala 117 mwaka 2019 hadi 100 mwaka 2023, wachumi wataja sababu.
Dar es Salaam. Wastani wa miamala inayofanywa kupitia mitandao ya simu imezidi kupungua kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kutoka 2019 hadi 2023, wachumi na wananchi wabainisha sababu.
Ripoti ya Takwimu za Mawasiliano ya Robo ya mwisho ya mwaka 2023 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha wastani wa miamala 17 imepungua kwa kila mtumiaji wa huduma hiyo ndani ya miaka mitano.
Ripoti ya TCRA inaonyesha mwaka 2019 wastani wa kila mtumiaji wa huduma hii alifanya miamala 117 kwa mwaka.
Mwaka 2020 ilipungua hadi miamala 106, mwaka 2021 ilisalia 106, mwaka 2022 ilishuka hadi kufikia 102 na mwaka 2023 ilishuka tena hadi 100.
Wakati wastani ukishuka, idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100, huku thamani ya miamala pia imeongezeka.
Ripoti hiyo inaonyesha mwaka 2019 watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu walikuwa 25,864,318. Mwaka 2020 (32,268,630), mwaka 2021 (35,285,767), mwaka 2022 (40,953,496) na mwaka 2023 (52,875,129).
Kwa mujibu wa ripoti, mwenendo wa thamani za miamala ya fedha kwa njia ya simu ndani ya miaka mitano imeongezeka kutoka Sh3 bilioni mwaka 2019 hadi Sh5.3 bilioni mwaka 2023, ambayo ni sawa na asilimia 19 ya ukuaji kwa kila mwaka.
Wasemavyo watumia huduma
Mkazi wa Igoma jijini Mwanza, Alicia Rugemalila, ambaye ni mfanyabiashara wa vinywaji vikali amesema tozo zilizopo katika miamala ya simu zinamfanya afanye malipo kwa fedha taslimu.
“Ninafanya biashara, hivyo inanilazimu kufanya miamala lakini ninajitahidi kuipunguza niwezavyo kwa sababu ya makato bado si rafiki, mara nyingi napendelea ‘cash’ (fedha taslimu)” amesema.
Kwa upande wake, Said Chiemba, mkazi wa Mabibo Mwembeni jijini Dar es Salaam amesema hutumia zaidi huduma za kibenki kupitia simu.
“Hivi sasa namalizia miamala yangu mingi kwa njia ya simu, naona wamerahisisha, pia kwangu ni salama zaidi fedha zangu kukaa benki,” amesema Said.
Mchumi mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema kupungua kwa wastani wa miamala kunatokana na tozo, pia majanga mengine yaliyotokea katika miaka hiyo.
“Hata hivyo, kuna faida za kiuchumi kama miamala imehamia benki, tusihuzunike kama miamala hii inahamia benki kwa sababu huko kuna faida zaidi, itarudi tena kwa wananchi kwa njia ya mkopo, lakini pia usalama wake ni mkubwa zaidi,” amesema.
“Miamala ni sehemu ya kipato na mzunguko wa fedha (velocity of money), katika kipindi ambacho wastani wa idadi ya miamala unapungua utagundua ni wakati ambao tozo ziliwekwa na pia kulikuwa na vita vya Ukraine na Russia na athari za ugonjwa wa Uviko-19,” amesema.
Profesa Kinyondo amesema, “Hizo zote ni sababu za kufanya watu waache kutumia huduma za kifedha za simu, kumbuka watu wanakimbilia huduma huko kwa ajili ya urahisi wa upatikanaji wake, sasa kukiwa na changamoto kama hizo inakuwa ngumu.”
Amesema maendeleo ya Tehama katika benki ikiwamo uanzishwaji wa huduma za kibenki kwa njia ya simu inaweza kuwa sababu ya kuwahamisha wateja kutoka kwenye huduma za simu hadi za kibenki.
Hoja ya huduma za kibenki kwa njia ya simu kuwa chanzo cha wastani wa miamala kupungua imeungwa mkono na Mchumi Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora anayesema:“Kupungua kwa miamala ya fedha ya simu kunasababishwa na sababu nyingi, lakini kubwa ni benki kuingia katika dijitali nako wateja wao wanaweza kurushiana fedha kutoka benki moja kwenda nyingine, hii lazima itaathiri huduma za kifedha za simu.
“Pia bado saikolojia ya Watanzania inaamini njia salama ya kutuma fedha ni benki, kwa hiyo nao walivyokuja na huduma ya kutuma fedha kidijitali wateja wengi wa simu wamehamia huko, bado kuna haja ya utafiti zaidi eneo hili.”
Naima Omari, ambaye ni mwanasaikolojia amesema binadamu huamini na kujenga mazoea ya maarifa aliyoyapata awali kabla ya mapya, hivyo kama benki iliyoanza awali imetengeneza mfumo rafiki wa fedha ni rahisi kwa watumiaji kurudi huko.
“Unajua kuna dhana inaitwa Cognitive Dissonance (maarifa ya awali kuaminika zaidi), hapa benki inaaminika zaidi nchini kwa sababu ndiyo mfumo wa kwanza wa kifedha, kwa hiyo saikolojia za watu lazima wawe na imani kubwa kwao,” amesema.
Amesema, “Wanapoanzisha huduma inayorahisisha utumiaji ni rahisi kuwapata watu wengi na ikibidi watu hao huhama kutoka sehemu nyingine.”
Utafiti wa GSMA
Vilevile utafiti uliofanywa na Shirikisho la Kampuni za Simu (GSMA), Desemba 2021, ulioitwa ‘Uchambuzi wa Athari ya Tozo kwenye Miamala ya Simu Tanzania’ ulionyesha watumiaji wengi wa huduma za kifedha za kielektroniki wamepungua kwa sababu ya tozo kupanda.
Sehemu ya ripoti hiyo imesema wapo watumiaji wa huduma za kifedha kielektroniki wameacha kutumia njia hizo tangu kuanzishwa kwa tozo, licha ya jitihada za watoa huduma kufanya maboresho ya viwango siku hadi siku.
Maoni ya mitandaoni