Tozo za miamala, mikopo ya wanafunzi ilivyotokisa bajeti

Muktasari:

Ukiacha moto aliouwasha Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alipohoji kwa nini kesi 1,097 za kodi zenye thamani ya Sh360 trilioni na dola 181.4 milioni za Marekani hazijaamuriwa hadi Septemba 2022, tozo za miamala ya kielektroniki na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ni hoja zilizolisimamisha Bunge mwaka 2022.

  

Ukiacha moto aliouwasha Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alipohoji kwa nini kesi 1,097 za kodi zenye thamani ya Sh360 trilioni na dola 181.4 milioni za Marekani hazijaamuriwa hadi Septemba 2022, tozo za miamala ya kielektroniki na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ni hoja zilizolisimamisha Bunge mwaka 2022.

Swali la Mpina liliwagonganisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na naibu wake, Hamad Hassan Chande ambao hawakuwa na majibu ya uhakika kuhusu kesi zilizopo mahakamani kuhusiana na madai ya kodi.

Utata huo umejitokeza katika kipindi cha maswali na majibu Septemba 22 ambapo Naibu Waziri Hamad alisema hadi Agosti kulikuwa na mashauri 854 yenye thamani ya Sh4.21 trilioni na dola 3.48 milioni, majibu ambayo hayakumridhisha Mpina.

“Nasikitika kwamba swali limeuliza Sh360 trilioni lakini nimejibiwa Sh4.21 trilioni,” alisema Mpina.

Swali hilo ambalo lilikuja kujibiwa vyema kwenye Bunge la Novemba ni kati ya hoja zilizofuatiliwa na wananchi wengi nje ya Bunge kutokana na jinsi mawaziri husika walivyojichanganya wakati wa kulijibu, huku Dk Mwigulu akipata kigugumizi kueleza maana ya Trab (Bodi ya Rufaa za Kodi) na Trat (Mahakama ya Rufaa za Kodi).

Tozo za miamala

Tangu zilipoanzishwa mwaka wa fedha uliopita, wananchi wamekuwa wakizipinga kiasi cha kutaka ziondolewe ili kuwapunguzia ugumu wa maisha.

Tozo hizo ambazo mwaka jana zilikuwa zikitozwa kuanzia Sh10 mpaka Sh10,000 kwa kila muamala wa simu, wigo wake ulitanuliwa zaidi na kuhusisha miamala yote ya kielektroniki, ingawa ukomo ulipunguzwa mpaka Sh4,000 kwa miamala yenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni.

Ilikuwa siku mbili kabla Mpina hajajibu hoja yake, yaani Septemba 20 ndipo Serikali ilipotangaza kufuta na kupunguza viwango vya tozo za miamala ya kielektroniki.

Waziri Mwigulu alisema Serikali imefanya hivyo ili kuchochea malipo ya kidijitali ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu, kurahisisha utozaji na kuzuia kutoza mara mbili.

“Marekebisho yaliyofanyika ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote),” alisema Dk Mwigulu.

Marekebisho mengine yalikuwa kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine (pande zote) huku gharama za makato hayo zikipunguzwa kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kulingana na kundi la muamala husika.

Hii ilikuwa ni mara ya tatu viwango hivyo vinapunguzwa. Mwanzo ilikuwa Septemba 2021 viliposhuka kutoka ukomo wa Sh10,000 mpaka Sh7,000 kisha Sh4,000 ya sasa.

Mikopo ya wanafunzi

Awali, Serikali iliitengea Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) Sh570 bilioni kwa ajili ya wanafunzi wapya 71,000 ambazo baada ya kutolewa zikaonekana hazitoshi.

Tathmini mpya iliyofanywa ilibaini mahitaji ya ziada ya Sh84 milioni, sawa na asilimia 14.7 na kufika Sh654 bilioni. Ongezeko hilo litapaswa kuidhinishwa na Bunge litakapokutana tena mwezi ujao.

Kiasi kilichoongezwa, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru anasema kitawatosha wanafunzi 28,000 na tayari fedha hizo zimeshapelekwa kwenye vyuo husika waweze kuanza masomo.

“Bajeti isingeongezwa ni wazi wanafunzi 28,000 wangekosa mikopo, lakini kutokana na hatua hii iliyochukuliwa wataweza kupata ufadhili huu. Hawa waliopata walikuwa tayari wameshafanyiwa tathmini na kuonekana mahitaji yao ni makubwa,” alisema Badru.

Ushiriki wa wananchi katika bajeti

Ingawa Tanzania inaelezwa kuwa na mchakato bora wa bajeti, lakini ushirikishaji mdogo wa wananchi ndio unaoleta changamoto zinazosababisha ama kupunguza baadhi ya vyanzo vilivyoidhinishwa au kuongeza matumizi kwenye uhitaji mkubwa zaidi.

Mhadhiri wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Mutahyoba Baisi anasema kwa jinsi ilivyoandikwa, hana wasiwasi kabisa na mchakato wa bajeti Tanzania, ingawa utekelezaji wa kilichoandikwa ndio kitu muhimu zaidi.

“Iwapo budget process (mchakato wa bajeti) haifuatwi, basi kitakachopitishwa hakitaungwa mkono na wananchi. Kwa utaratibu, bajeti inatakiwa kuwashirikisha wananchi watakaoeleza vipaumbele vyao, hicho kisipofanyika wataikataa kama ilivyotokea kwenye tozo za miamala ya kielektroniki,” anasema Dk Baisi.

Hata kilichotokea kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, mchumi huyo mwandamizi anasema tatizo lipo kwenye utambuzi na upangaji wa nani apate kiasi gani matokeo yake wanaachwa wenye uhitaji mkubwa, huku wenye unafuu wakipewa kikubwa zaidi.

“Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, nadhani tatizo lipo kwenye means testing (ukadiriaji kwa wanafunzi). Utaratibu wa kuwatambua wanafunzi na mahitaji yao uzingatiwe zaidi ili kila mmoja apate anachostahili. Hii ndio namna ya kuondoa malalamiko,” anashauri Dk Baisi.

Ili kuepuka malalamiko yanayoibuliwa na wananchi ama kwenye vyanzo vya mapato au matumizi yake, Dk Baisi anashauri Serikali kupunguza matumizi yake, kwani inayo mengi yanayotokana na ahadi zilizomo kwenye ilani ya chama tawala.

Ibara ya 8 ya Katiba ya Tanzania inampa mwananchi haki ya kushiriki shughuli za maendeleo ya nchi na Sheria ya Serikali za Mitaa namba saba na nane ya mwaka 1982, inazipa Mamlaka za Serikali za Mitaa uwezo wa kuandaa mipango na bajeti ya halmashauri.

Jukumu la kwanza la Serikali katika kuandaa bajeti ya Taifa ni kukusanya maoni na mahitaji ya wananchi kisha kupanga makisio ya mapato na matumizi kwa niaba ya wananchi ambao ndiyo wamiliki wa rasilimali.

Mwananchi anashiriki kuandaa bajeti kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji na mtaa kwa kushiriki vikao vya kuibua fursa na vikwazo vya maendeleo na kupanga vipaumbele vya mwaka husika.

Maimuna Mohammed, mtumishi wa umma mkoani Iringa anasema hakuna mwananchi anayepinga kulipa kodi, lakini utaratibu wa kuwalundikia watu wachache ndilo linaloleta kilio, hivyo watendaji wanaohusika waangalie namna ya kuibua vyanzo vipya.

“Tatizo ninaloliona ni wahusika kutaka kukusanya kodi rahisi. Kuna maeneo wanayakimbia, hivyo kuelekeza nguvu zao kwa wafanyakazina wafanyabiashara wachache waliorasimisha biashara zao, matokeo yake mzigo unaenda kwa wachache,” anasema Maimuna.

Maimuna anasema kodi nzuri ni ile inayowatoza zaidi wenye nacho na kuwapa ahueni wasionacho, lakini kwenye hii ya miamala Serikali ilitaka kuweka usawa ndio maana kelele zilikuwa nyingi.

Joel Patrick, mjasiriamali wa mpunga mkoani Mbeya anasema serikalini kuna matumizi mengi yasiyo ya lazima ambayo hupaisha bajeti ya matumizi ya kawaida huku ya maendeleo ikibaki kidogo.

“Tatizo yakishapitishwa matumizi hata kama yanaweza kufutwa, hayaondolewi. Yanaachwa kama yalivyo na Serikali inaweza kukopa kwa ajili ya kulipia chai na mikutano ya idara, vitu ambavyo kama vingepunguzwa, bajeti ingekuwa inatosha muda wote,” anasema.


Utekelezaji wa bajeti

Utekelezaji wa bajeti hulenga kufanikisha malengo ya kukusanya mapato na kusimamia matumizi, ila kumekuwa na mapungufu yanayosababisha ukusanyaji wa mapato kuwa mdogo, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na uvujaji wa mapato.

Katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa mfano, Serikali ilishindwa kukusanya asilimia 10 ya bajeti iliyoidhinishwa ambayo ni Sh34.87 trilioni, zikiwamo Sh12.89 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh21.98 trilioni kwa matumizi ya kawaida.

Uchambuzi uliofanywa na taasisi ya Wajibu unaonyesha Serikali ilishindwa kukusanya kiasi kikubwa kutoka kwenye kodi ambako ilipanga kupata Sh20.32 trilioni ila ikakusanya Sh17.59 trilioni ikishindwa kwa asilimia nane ya malengo ya bajeti.

“Kushindwa kukusanya mapato kulingana na bajeti iliyoidhinishwa, kunadhihirisha kuwa bajeti iliyopangwa haikuwa na uhalisia hivyo matarajio ya wananchi kutofikiwa,” imesema Wajibu kwenye tathmini yake ya ripoti ya mapato na matumizi ya Serikali.

Kushindwa kukusanya mapato kama ilivyotarajiwa kunafanya utekelezaji wa bajeti kutofikia malengo yaliyopangwa, hivyo kero za wananchi kubaki kama zilivyo.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kipindi hicho inaonyesha Serikali za Mitaa hazikupokea Sh840 bilioni, sawa na asilimia 14 ya ruzuku iliyoidhinishwa hivyo kushusha uwezo wa kutoa na kuboresha huduma kwa wananchi.

Ili Serikali iweze kukusanya zaidi ya asilimia 95 ya bajeti yake kama inavyopendekezwa kimataifa, Taasisi ya Wajibu inapendekeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kufanya upembuzi wa kina wa aina na uwezo wa vyanzo vya mapato ili upangaji wa bajeti uwe halisia.