Mume adaiwa kumuua mkewe

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo.

Muktasari:

  • Inadaiwa baaada ya mauaji hayo mtuhumiwa alitoroka na kujificha lakini kwa ushirikiano wa wananchi na Polisi walimbaini akiwa amekunywa vitu vinavyodhaniwa ni sumu ili kujidhuru.

Geita. Watu wanne wamepoteza maisha mkoani Geita katika matukio mawili tofauti, likiwemo la mume kudaiwa kumuua mkewe kwa kumpiga na kitu kizito kichwani, lililotokea katika Kitongoji cha Msasa, Kata ya Nyarugusu, wilayani Geita.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita imesema Juni 17, 2024 saa 11 jioni, Ndaki Shabani (35), mchimbaji wa madini Msasa – Nyarugusu anadaiwa kumuua mke wake, Pili James (37).

Baaada ya mauaji hayo, mtuhumiwa alitoroka na kujificha lakini kwa ushirikiano wa wananchi na jeshi la polisi walibaini alipo na kumkuta amekunywa vitu vinavyodhaniwa ni sumu, hivyo kupelekwa hospitali kunusuru uhai wake.

Katika taarifa iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo inaeleza uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Katika tukio lingine, watu watatu wakiwemo watumishi wawili wa sekta ya afya wilayani Chato mkoani Geita wamepoteza maisha baada ya pikipiki waliyokuwa wamepanda kugongwa na gari.

Katika ajali hiyo iliyotokea Juni 17, 2024 saa 12:15 jioni katika katika kijiji cha Mlimani Kata ya Muungano, waliofariki dunia ni Egidia Aron (30) mtaalamu wa maabara katika Hospitali ya Bwina aliyekuwa anaendesha pikipiki na Diana John (32), muuguzi katika Hospitali ya Chato.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Polisi, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva kwenye makazi ya watu na uzembe wa kutozingatia watumiaji wengine wa barabara.

Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka dereva wa gari hilo ambaye hajafahamika, ambaye alitoroka baada ya ajali kutokea.

Ajali nyingine ilitokea wilayani Bukombe na kusababisha kifo na majeruhi baada aina ya Toyota Prado mali ya mali ya China Civil Engeneering and Constraction Ltd likiendeshwa na Daimon Charles (31) kugonga pikipiki na kusababisha kifo cha Florencia Mhana (35), mwalimu wa Shule ya Msingi Ishololo na kusababisha majeruhi kwa dereva mwingine wa pikipiki, Zacharia (32) mkazi wa Ushirombo.

Polisi wamesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari kutochukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.