Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muliro, RPC Kitinkwi waongoza polisi ulinzi mkutano Chadema

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ni miongoni mwa askari waliokuwepo eneo la Mlimani City kuimarisha ulinzi katika mkutano wa uchaguzi wa Chadema.

Dar es Salaam. Hali ya ulinzi si suala la kutilia shaka katika viunga vya Mlimani City, Dar es Salaam, kunapofanyika mkutano wa uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) utakaoamua hatima ya nafasi ya uenyekiti na makamu wake bara na Zanzibar.

Hilo linatokana na kusambaa kwa vikosi vya ulinzi na usalama katika eneo hilo, leo Jumanne, Januari 21, 2025, vikiongozwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Sambamba na Muliro, katika eneo hilo alikuwepo pia Mtatiro Kitinkwi, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, wote wakihakikisha wanatawanya askari wa jeshi hilo ili kuimarisha ulinzi.

Magari ya askari wa jeshi hilo zaidi ya 10 yanaonekana nje ya ukumbi, na askari, akiwemo Muliro na Kitinkwi, wakiwa umbali wa takriban mita 100 kutoka walipokuwepo wafuasi wa Chadema.

Kwa hali ilivyokuwa katika viunga hivyo, ungedhani kuna tukio kubwa la kustaajabisha, kutokana na namna polisi walivyokuwa wamejipanga, huku wanachama nao wakizunguka huku na kule.

Maandamano ya vikundi vya wafuasi wa Chadema, yameshuhudiwa yakishajihisha na nyimbo za kumnadi mgombea wa uenyekiti, Tundu Lissu, na anayeutaka umakamu bara, John Heche.

Usingeamini kama katika eneo hilo kulikuwa na wafuasi wanaomuunga mkono Mbowe, kwa kuwa kelele na nyimbo zilizoimbwa zilimtaja Lissu na Heche.

Hata hivyo, nyimbo na kelele zilizopigwa hazikutosha kuthibitisha ushindi wa Lissu, kutokana na kile kilichoelezwa na baadhi ya wajumbe wa upande wa Mbowe kuwa, maneno ya washindani wao ni kama ngoma ya watoto ambayo aghalabu haikeshi.

"Hiyo ni ngoma ya watoto haikeshi, waache wapige kelele, tutaenda kuwapigia (kushinda) ndani," amesikika mmoja wa wafuasi wa Mbowe.

Lakini, kulikuwepo na vikundi vya wafuasi wa chama hicho vinavyovishania ubora wa wagombea wa uenyekiti kati ya Lissu na Mbowe.

Kadhalika, wengine walihoji kulikuwa na haja gani ya kuwepo kwa vikosi vya jeshi la polisi katika uchaguzi wa chama kimoja.

Shangwe ziliongezeka ilipofika saa 4:11 asubuhi baada ya Lissu kuwasili ukumbini hapo, akisindikizwa na gari mbili pamoja na yake.

Lissu aliwasili ukumbini hapo akiwa na wasaidizi zaidi ya watano, nyimbo za 'Lissu, Lissu, Lissu' ziliimbwa kama ishara ya kupokea kwa furaha.

Idadi kubwa ya wajumbe walibeba mabango yenye jina la Tundu Lissu na John Heche.

Wafuasi wakimpokea Heche alipowasili viwanja vya Mlimani City ambapo mkutano mkuu utafanyika leo.

"Wewe unalalamika unafilisika unatoa fedha zako za mfukoni, wametokea wa kukupokea unalalamika, waachie na wengine wafilisike," maneno ya mmoja wa wajumbe waliosikika nje ya ukumbi huo.

Wanaogombea nafasi ya makamu mwenyekiti bara ni John Heche anayemuunga mkono Lissu, Ezekia Wenje anayemuunga mkono Mbowe, na Mathayo Gekul.

Kwa upande wa makamu mwenyekiti Zanzibar, ni Hafidh Ali Saleh, Said Issa Mohammed, Said Mzee Said, na Suleiman Makame Issa.


Endelea kufuatilia Mwananchi