Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hali ilivyo uchaguzi Chadema Mlimani City, shangwe zatawala

Muktasari:

  • Leo Jumanne, Januari 21, 2025 mkutano mkuu wa Chadema unafanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Maandalizi ya ukumbi watakapokaa wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), watakaoamua hatima ya mafahali watatu wanaowania kukiongoza chama hicho, yamekamilika.

Ni ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Januari 21, 2025, utakaopokea wajumbe 1,360 wa mkutano mkuu wa Chadema, ambao kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, ndio wataamua mustakabali wa uongozi wa juu wa chama hicho.

Tayari baadhi ya wajumbe wameanza kuingia ukumbini na watakuwa na kazi ya kukata majina mawili na kubaki na jina moja kati ya matatu yanayowania nafasi ya uenyekit---Charles Odero, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.

Makamu mwenyekiti wa Chadema(bara), Tundu Lissu akiingia maeneo ya Mlimani City jijini Dar es Salaam leo wanachama wakiwa wamezunguka gari lake. Picha na Sunday George

Mbowe, ambaye anawania nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21, anakutana na upinzani wa karibu kutoka kwa makamu wake Bara, Lissu.

Kalamu za wajumbe ndizo zitaamua hatima ya Mbowe kuendelea na wadhifa wa uenyekiti au nafasi hiyo ikabidhiwe makamu wake, Lissu, ambaye amejinasibu kuahidi kukijenga upya chama hicho, au Odero.

Yeyote kati ya viongozi hao watakaoaminiwa na wajumbe atakuwa na kazi ya kukirejesha chama katika mstari kutokana na mgawanyiko uliopo sasa baina ya upande unaomuunga mkono Lissu na Mbowe.

Pande hizo mbili zimekuwa na mvutano baada ya Lissu kuibua shutuma za rushwa ndani ya chama, akisema zipo fedha zinazotumika katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho ambazo hazijulikani zinatoka wapi.

Januari 17, 2025, akiwa kwenye mdahalo wa kisiasa uliofanyika kupitia Star TV, Lissu alisema:

"Mimi ndiye niliyekuwa wa kwanza kupuliza filimbi kwamba kuna rushwa kwenye chaguzi zetu (Chadema). Tuna tatizo, muda huu tunapozungumza, kuna wajumbe wanasafirishwa, wanawekwa kwenye mahoteli, makambi, wanapewa pesa, wanalishwa na wagombea. Kuna uchafuzi wa aina hiyo unaofanywa na wagombea na wapambe wao," alidai.

Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, ambaye mara kwa mara ameeleza kuwa hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa, akisisitiza mwenye ushahidi aupeleke hatua zichukuliwe.

Shutuma hizo zimezidisha minyukano baina ya wafuasi wa Lissu na Mbowe, ambapo mara kadhaa kila upande umekuwa ukivutia upande wake, ukijinadi kwamba ni zamu yao kukiongoza chama hicho, huku mivutano hiyo ikijitokeza kupitia vyombo vya habari.

Mbali na hayo, uchaguzi wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha), Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), na Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) uligubikwa na dosari, ikiwemo madai kwamba baadhi ya wajumbe wamepewa hongo, hali inayotajwa kama hujuma za upande mmoja kujitengenezea nafasi ya uongozi.

Pamoja na hayo yote, leo ni swali moja tu litakalojibiwa: nani atakuwa Mwenyekiti wa Chadema? Wakati tunasubiri wajumbe kutegua kitendawili hicho, kibao cha muziki "One Love" cha Bob Marley na wimbo wa Profesa Jay "Zali la Mentali" vinatamba ukumbini.

Nje ya viunga vya ukumbi wa Mlimani City, wapambe wa wagombea wote watatu – Odero, Lissu, na Mbowe – wanaimba nyimbo na kushangilia huku wakiwa na mabango na picha za wagombea wao.

Saa 4:15 asubuhi, Lissu amewasili katika viunga vya ukumbi huo, akipokelewa kwa shangwe na wapambe wake waliomuunga mkono. Gari alilokuwa amepanda limesukumwa na wafuasi wake hadi kwenye maegesho.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, chini ya Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro, wameimarisha ulinzi kwa askari wenye silaha waliopo katika magari na kutanda viunga vya ukumbi huo.


Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali.