Moto uliozuka Hifadhi ya Kinapa waendelea kuthibitiwa

Muktasari:
- Moto uliozuka katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa) katika eneo la Indonet-Rongai, wilayani Rombo umeendelea kudhibitiwa ambapo tayari watu 134 kutoka vikosi mbalimbali vya Jeshi vipo katika eneo hilo kuukabili moto huo.
Rombo. Moto uliozuka Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa) katika eneo la Indonet-Rongai, wilayani Rombo umeendelea kudhibitiwa ambapo tayari watu 134 kutoka vikosi mbalimbali vya Jeshi vipo katika eneo hilo kuukabili moto huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 8, 2023 na Ofisa Uhifadhi Mwandamizi kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Catherine Mbena inaeleza moto huo ambao chanzo chake bado hakijajulikana ulizuka Septemba 3, mwaka huu.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, vikosi vya askari na Maofisa wa Jeshi la Uhifadhi (JU), Jeshi la Akiba, na wananchi wa vijiji jirani mpaka sasa wameudhibiti moto huo kwa asilimia kubwa.
"Chanzo cha moto huo bado hakijulikana na uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama," imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa shughuli za utalii katika Mlima Kilimanjaro zinaendelea kama kawaida huku vikosi vingine zaidi vikiendelea kupelekwa kuhakikisha moto huo unadhibitiwa.