VIDEO: Moto wazuka mlima Kilimanjaro

Muktasari:
Kamishina wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi Tanzania (Tanapa), William Mwakilema amesema vikosi vinaelekea kuuzima moto huo.
Moshi. Moto ambao chanzo chake bado hakijajulikana, umezuka katika mlima Kilimanjaro, karibu na eneo la Karanga Camp lililopo urefu wa meta 3,963 kutoka usawa wa bahari kupitia njia ya Mweka na jitihada ya kuuzima zinaendelea.
Moto huo ulianza kuonekana jana Ijumaa Oktoba 21, 2022 usiku kutokea Moshi Mjini, ambapo Kamishina wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi Tanzania (Tanapa), William Mwakilema aliyezungumza na Mwananchi leo Oktoba 22, amesema vikosi vinaelekea kuuzima moto huo.
Taarifa zinaeleza moto huo unawaka ukanda wa Moorland, ambao mimea yake ikishika moto huwa ni mkali na tayari Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Hifadhi ya Kilimanjaro (Kinapa) wametuma vikosi kwenda kuukabili.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana Oktoba 21, Kamishina wa Uhifadhi kanda ya Kaskazini, Betrita James amesema baada ya kupata taarifa za kuonekana kwa moto huo, menejimenti ya Kinapa ilianza mara kazi ya kukusanya nguvu kazi na vifaa, na tayari timu zimeelekea eneo hilo.
Mbali na timu hiyo, video ambazo zimesambaa katika makundi mbalimbali ya Whatsapp zinawaonyesha baadhi ya waongoza watalii (Guides) na wapagazi (porters), wakijaribu kuzima moto huo kwa kutumia majani ya miti.
Mmoja wa waongoza watalii mwenye uzoefu na njia hiyo, Geness Shirima, amesema kwa kadri alivyojulishwa, moto huo uko karibu na Karanga Camp na Askari wa Kinapa na wadau wengine walikuwa wakielekea huko kushiriki kazi ya kuuzima.
“Ukitoka kituo cha Mweka ndio unaenda Millennium au High Camp halafu ndio Karanga yaani iko kwenye zone (ukanda) moja. Ni eneo liko juu kama urefu wa karibu meta 4,000 hivi kutoka usawa wa bahari.
“Mfano kama chakula cha wageni kinapandishwa huwa kinapelekwa Karanga camp kwa sababu ndio kituo ambacho ni kabla ya kwenda kituo cha mwisho kwenda Summit (kileleni) pale ndio wageni wanapelekewaga chakula fresh”
Amesema moto huo unaonekana kutokea njia ya Mweka kuelekea ukanda wa Moorland wenye vichaka.
“Ndio maana huu moto unakamata kwa kasi sana ni kama umewasha petrol,” amesitiza.
Oktoba 2020, moto mwingine ulizuka katika mlima huo katika ukanda wa nyasi na vichaka na kuteketeza vibanda 15 vya kulala wageni katika mlima Kilimanjaro pamoja na mifumo ya umeme wa jua na miundombinu ya maji taka.
Endelea kusoma mitandao yetu kwa taarifa zaidi