Mgogoro wa biashara ya samaki ulivyosababisha mauaji
Muktasari:
- Mahakama ilieleza kuwa Selemani alikiri kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na vifungu vya 195 na 198(1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023.
Arusha. Mgogoro uliotokana na biashara ya samaki katika Soko la Kilombero jijini Arusha uliosababisha kifo cha mfanyabiashara, Shaaban Mruma baada ya kuchomwa kisu shingoni, umempeleka jela kwa miaka mitatu Selemani Bakari baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Katika shauri hilo, Selemani alikiri kufanya kazi na Shaaban (marehemu) katika soko hilo na kwamba kulikuwa na ugomvi baina yao uliotokana na biashara ya samaki.
Ilidaiwa walipokutana siku moja baada ya ugomvi huo kwa lengo la kutatua tofauti zao, hawakuelewana na walianza kubishana. Shaaban alimsukuma mshtakiwa, ambaye alianguka na alipoinuka alichomoa kisu na kumchoma mwenzake shingoni.
Ilidaiwa mahakamani kuwa, Shaaban alivuja damu nyingi na siku iliyofuata alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.
Hukumu hiyo ilitolewa Julai 3, 2026 na Jaji Aisha Bade, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, huku nakala ya uamuzi huo ikiwekwa kwenye tovuti ya Mahakama.
Jaji amesema pamoja na kuwepo kwa mazingira ya ugomvi wa ghafla, matumizi ya kisu na kumchoma mwathirika katika sehemu hatari ya mwili yalichangia kupotea kwa uhai wa binadamu, jambo ambalo haliwezi kupuuzwa.
Mahakama ilieleza kuwa Selemani alikiri kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na vifungu vya 195 na 198(1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023.
Jaji amesema kosa la kuua bila kukusudia ni kosa zito kwa sababu husababisha kupotea kwa uhai wa binadamu ambao hauwezi kurejeshwa.
Amesema ingawa hakukuwa na ushahidi kwamba mshtakiwa alipanga kumuua marehemu, alipaswa kufahamu kuwa kutumia kisu na kumchoma mtu shingoni kunaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo kifo.
"Haya ni mazingira mazito. Mshtakiwa alitumia kisu na alichoma sehemu ya mwili ambayo ni hatari, yaani shingoni.
"Hata kama kulikuwa na ugomvi au msukosuko wa ghafla kati ya wawili hao, mtu mwenye busara alipaswa kutambua kuwa, kutumia kisu katika sehemu kama hiyo kunaweza kusababisha madhara makubwa sana, ikiwamo kifo, kama ilivyokuwa hapo," amesema Jaji.
Hata hivyo, Mahakama ilizingatia mazingira yaliyopunguza uzito wa adhabu, ikiwamo kwamba Selemani hakuwa na rekodi ya makosa ya jinai, alikiri kosa mapema, hivyo kuokoa muda wa Mahakama pamoja na kuwaepusha mashahidi na familia ya marehemu kupitia upya maumivu ya tukio hilo wakati wa usikilizwaji kamili wa shauri.
"Mazingira ya tukio yanaonesha kulikuwa na ugomvi, msukosuko na msukumo wa ghafla. Hayakuonesha kuwa mshtakiwa alipanga kabla ya kumdhuru marehemu, japokuwa walishagombana siku iliyotangulia."
Jaji Bade amesema pia alizingatia maelezo ya upande wa mashtaka kuwa tukio hilo lilitokea katika mazingira ya kuchokozana na ugomvi, lakini mshtakiwa hakupaswa kutumia nguvu iliyozidi kiwango.
Katika hoja za kupunguza adhabu, wakili wa utetezi aliiambia Mahakama kuwa Selemani ana umri wa miaka 28, ni baba wa watoto watatu wenye umri wa miaka minne, miwili na mtoto mchanga, huku mke wake akiwa mama wa nyumbani anayemtegemea.
Mahakama pia ilielezwa kuwa wazazi wa mshtakiwa ni wazee wanaomtegemea na kwamba tayari alikuwa amekaa rumande kwa takribani miezi 10 tangu alipokamatwa.
Jaji Bade amesema hoja ya kwamba mshtakiwa alikuwa akijihami haiwezi kuondoa hatia kwa kuwa alikiri kosa, lakini mazingira hayo yanaweza kuzingatiwa katika kupunguza adhabu kwa sababu tukio lilitokea wakati wa ugomvi wa ghafla.
Baada ya kupima uzito wa kosa, mazingira ya tukio, kukiri kosa, kutokuwa na rekodi ya uhalifu, umri wa mshtakiwa, majukumu yake ya kifamilia pamoja na muda aliokaa rumande, Mahakama iliamua kuwa adhabu inayostahili ni kifungo cha miaka mitatu jela.
Katika uamuzi wake, Jaji Bade amesema kuwa lengo la adhabu si kulipiza kisasi, bali kutenda haki, kumrekebisha mkosaji na kuikumbusha jamii kuwa migogoro, hasira au msukumo wa ghafla hauwezi kuhalalisha matumizi ya silaha au nguvu zinazoweza kusababisha kifo.
"Ieleweke kuwa Mahakama haitoi adhabu kwa nia ya kulipiza kisasi, bali kwa ajili ya kutenda haki, kutambua thamani ya uhai uliopotea, kumrekebisha mkosaji, lakini pia kuikumbusha jamii kuwa migogoro, hasira au msukumo wa ghafla hauwezi kuwa sababu ya kutumia silaha au nguvu inayoweza kupoteza maisha ya mwenzako.
"Kwa msingi huo, adhabu ya kifungo cha miaka mitatu ninayoitoa ni adhabu yenye kuzingatia huruma na mazingira ya tukio, lakini pia inatoa onyo kwamba uhai wa binadamu ukipotezwa, aliyefanya hivyo atawajibika," amesema Jaji Bade