Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mmoja auawa na fisi Karatu

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikuyu, Zakaria Luhai amesema kuwa fisi hao wanakuja kwenye makazi ya watu kutokana na kuwa karibu na hifadhi za Taifa.

Karatu. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Posiani Timote (45) amefariki dunia jana katika Hospitali ya Lutheran iliyoko wilayani Karatu baada ya kujeruhiwa na fisi Agosti 29 mwaka huu katika eneo la Rotya mkoani Arusha.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema tukio hilo limetokea Agosti 29 saa nne usiku katika eneo la Kilimatembo, Kata ya Rotya.

"Mtu huyo mkazi wa Kilimatembo alijeruhiwa mita chache wakati akielekea nyumbani kwake usiku wa kuamkia Agosti 29 katika Kitongoji cha Kikuyu, Kata ya Rotya kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Kanisa la Lutheran iliyoko huko huko karatu,"amesema.

Kaka wa Marehemu Benedict Timote amesema kuwa walipokea simu kutoka kwa mmoja wa jirani wa marehemu kuwa ndugu yao aliliwa na fisi sehemu mbalimbali za mwili wake na amepelekwa katika Hospitali ya Kanisa la Lutheran iliyopo mjini Karatu.

"Nilitoka kuwahi hospitalini usiku huo karibu kukucha, Kiukweli ilikuwa ngumu kuamini kumkuta ndugu yangu nyama zote za miguu zililiwa na fisi na kubaki mifupa na sehemu za kifuani na kwenye mbavu, nililia sana nikijua hawezi kuishi kwa mda mrefu lakini tulijipa moyo kabla ya jana ijumaa kupewa taarifa za kifo chake," alisema kwa tabu huku akilia.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa siku ya tukio walisikia kelele za mtu akiomba msaada ambapo waliwahi eneo la husika na kukuta fisi huyo akimshambulia marehemu sehemu mbalimbali za mwili wake hasa miguuni na kifuani.

"Tulisikia kelele na kukimbilia huko ndipo tukakuta fisi ananyofoa nyama za marehemu na kula ambapo amefanikiwa kula sehemu za miguuni na kifuani ndipo tukaanza kumpiga na kumfukuza na kukimbilia porini," amesema Elibariki Sirwa.

Mkazi mwingine, Noeli Julius amesema kuwa matukio ya watu kuliwa na fisi katika eneo hilo ni mengi hivyo kuiomba Serikali kibali cha kuwawinda wanyama hao ikiwemo kuharibu makazi yao yaliyoko kilomita chache karibu na makazi ya watu.

"Kwa mwaka huu tu zaidi ya matukio saba yametokea ya watu kushambuliwa na huyu ni mtu wa tatu kuuliwa na fisi hapa na wengine wamebaki na ulemavu wa kudumu na tukiwaua tunakamatwa na askari wa hifadhi hivyo tunaomba Serikali kibali cha kuwafukuza wanyama hawa kwani wamekuwa na madhara makubwa kwa wakazi wa eneo hili," amesema.

Magdalena Daat amesema kuwa wana hofu kubwa na fisi hao kutokana na imani za kishirikina wakidai kuwa hawaonekani mchana bali ni usiku tu hivyo kuwaomba viongozi wa dini kuweka kambi ya maombi katika kata hiyo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikuyu, Zakaria Luhai amesema kuwa fisi hao wanakuja kwenye makazi ya watu kutokana na kuwa karibu na hifadhi za Taifa.

"Hawa fisi hakuna cha uchawi bali ni mambo tu ya mazingira na ramani ya wilaya yetu kupakana na Hifadhi ya Taifa ya Wanyama ya Tarangire na Ngorongoro ndiyo maana ujirani huo unawaleta lakini kiukweli wamekuwa tatizo kubwa kwa wananchi," amesema.