Mishahara yapaa tena

Muktasari:

Ni kicheko, hivi ndivyo unavyoweza kuelezea furaha waliyonayo wafanyakazi wa sekta binafsi, baada ya Serikali kutangaza kima kipya cha chini cha mshahara, ikiwa imepita miaka tisa tangu ilipopanda mwaka 2013.


Dar/Moshi. Ni kicheko, hivi ndivyo unavyoweza kuelezea furaha waliyonayo wafanyakazi wa sekta binafsi, baada ya Serikali kutangaza kima kipya cha chini cha mshahara, ikiwa imepita miaka tisa tangu ilipopanda mwaka 2013.

Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wamesema viwango hivyo vipya vya kima cha chini cha mshahara, vitakuwa na matokeo chanya na hasi, wakisema ingawa mapato ya Serikali yataongezeka, lakini mfumuko wa bei nao utapanda.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu kuhusu taarifa hiyo, Mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory, alisema inaweza kuwa na matokeo hasi, kwani baadhi ya waajiri wanaweza kupunguza wafanyakazi ili waweze kumudu kulipa mishahara hiyo mipya hivyo kuathiri wigo wa ajira.

Kima hicho cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kimetangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako kupitia tangazo la Serikali (GN) namba 697 la Novemba 25, 2022.

Hata hivyo, amri hiyo ya Serikali itakayojulikana kama amri ya kima cha chini cha mshahara kwa mwaka 2022 itaanza kutumika Januari 1, 2023 na kwamba amri kama hiyo ya kima cha chini kwa sekta binafsi iliyotolewa mwaka 2013 imefutwa.

Kima hicho cha chini kimegusa takribani sekta 12 ambazo ni kilimo, afya, mawasiliano, kazi za majumbani na hotelini, huduma za ulinzi binafsi, nishati, usafirishaji, ujenzi, madini, shule binafsi na sekta ya biashara na viwanda.

Pia mabadiliko hayo yamegusa sekta ya uvuvi na huduma za baharini na sekta nyingine na sheria hiyo imetoa ruhusa kwa mwajiri kumlipa mfanyakazi zaidi ya kima cha chini isipokuwa hatamlipa mfanyakazi chini ya kiwango kilichotangazwa.

Tangazo hilo limekuja miezi mitano kupita, tangu Waziri Ndalichako kutangaza kuwa Serikali ilikuwa katika hatua za mwisho za kutangaza kima cha chini kwa Sekta binafsi, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 63 wa Chama cha Waajiri (ATE).

Kupitia sheria hiyo, pamoja na likizo ya mwaka yenye malipo, mfanyakazi atakuwa na haki ya posho ya likizo mara moja kila miaka miwili ya utumishi na dereva wa lori yeye atastahili posho kwa ajili ya umbali wa safari na kukaa nje ya kituo.


Viwango vya mshahara

Katika viwango hivyo vipya, mfanyakazi anayefanya kazi katika migahawa, nyumba za kulala wageni na baa atalipwa kima cha chini cha Sh150,000 kwa mwezi, hoteli za kati Sh180,000 na hoteli za kitalii atalipwa Sh300,000.

Mfanyakazi wa kazi za ndani ambaye haishi katika kaya ya mwajiri atalipwa chini ya Sh120,000, huku wale wasio katika kundi hilo watalipwa Sh60,000 kwa mwezi, huku wafanyakazi wa kazi za ndani walioajiriwa na Wanadiplomasia na wafanyabiashara wakubwa wakilipwa kima cha chini cha Sh250,000.

Wafanyakazi wanaofanya kazi katika huduma za mawasiliano watalipwa kima cha chini cha Sh500,000, wakati wafanyakazi wa huduma za utangazaji na vyombo vya habari, posta na usafirishaji vifurushi watalipwa kima cha chini Sh225,000.

Katika hoteli kubwa za kitalii, mfanyakazi atalipwa kima cha chini Sh300,000, hoteli za kati Sh180,000, huku katika makampuni makubwa na kimataifa huduma ya ulinzi wakilipwa Sh222,000 huku makampuni madogo wakilipwa Sh148,000.

Hali ikiwa hivyo katika sekta hiyo, katika sekta ya Nishati makampuni ya kimataifa watalipwa Sh592,000 na makampuni madogo Sh225,000, wakati katika sekta ya usafirishaji, wanaofanya katika huduma za usafiri wa anga watalipwa Sh390,000.

Katika sekta hiyo, wafanyakazi wanaofanya kazi za kutoa huduma za utoaji mizigo na usambazaji watalipwa kima cha chini cha mshahara Sh360,000, ilhali wale wanaofanya kazi katika huduma za usafiri nchi kavu ni Sh300,000.

Tangazo hilo halijawaacha nyuma makandarasi ambapo makandarasi wa daraja la pili hadi la nne watalipwa kima cha chini Sh360,000, huku wale wa daraja la tano hadi la saba wakilipwa kima cha chini ya mshahara cha Sh320,000 kwa mwezi.

Katika sekta ya madini, wenye leseni za uchimbaji na utafutaji madini wao kima cha chini cha mshahara kitakuwa Sh500,000, huku wenye leseni za wachimbaji wadogo kikiwa Sh300,000 na wenye leseni za wafanyabiashara kikiwa Sh450,000.

Huduma za shule binafsi kuanzia shule za awali, msingi na sekondari watalipwa kima cha chini Sh207,000, huku katika sekta ya biashara na viwanda wakilipwa Sh150,000 na Taasisi za fedha wakilipwa Sh592,000 kwa mwezi.

Sekta ya uvuvi na huduma za baharini wamepangiwa kima cha chini cha Sh238,000 kwa mwezi na sekta nyingine zote ambazo hazijaainishwa katika tangazo hilo la Serikali, wao watalipwa mshahara wa Sh150,000 kwa mwezi.


TPSF, TUCTA wafunguka

Alipoulizwa kwa simu jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Henry Mkunda alisema hadi Serikali inatangaza kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi, kulikuwa na mchakato uliochukua miaka miaka mitano.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera Taasisi ya Sekta binafsi (TPSF), Zachy Mbena alisema hatua hiyo ni nzuri, kwani kuwepo kwa mfumo unaoratibu viwango vya mishahara huongeza ari, japo zipo sekta binafsi zinazowalipa wafanyakazi zaidi kutokana na utendaji wao.


Wachumi wafunguka

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema “Katika matokeo chanya ni kwamba Serikali itaongeza mapato yake kupitia ile kodi ya PAYE (lipa kadri unavyopata) ambayo hukatwa kwenye mshahara. Kwa hiyo mshahara ukiongezeka na Paye inaongezeka,” alisema mchumi huyo mbobezi.

Mtaalamu wa biashara na mchambuzi wa masuala ya kijamii, Conrad Kabewa alisema ongezeko hilo la kima cha chini linakuwa halina maana sana kama Serikali haitadhibiti mfumuko wa bidhaa.