Meya Temeke aomba barabara mwendokasi Mbagala itumike

Muktasari:
- Tangu mvua hizo zilipoanza wiki tatu zilizopita, zimesababisha kuharibika kwa barabara ndogo za mitaani na kulazimisha magari mengi kuingia barabara hiyo, hivyo kuleta msongamano.
Dar es Salaam. Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, Meya wa Manispaa ya Temeke Abdalla Mtinika ameiomba Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuruhusu kutumika kwa barabara ya mwendokasi ya Kilwa kutoka Mbagala kwenda Kariakoo, ili kupunguza msongamano wa magari.
Tangu mvua hizo zilipoanza wiki tatu zilizopita, zimesababisha kuharibika kwa barabara ndogo za mitaani na kulazimisha magari mengi kuingia barabara hiyo, hivyo kuleta msongamano.
Akizungumza jana Novemba 9 wakati wa kikao cha baraza la madiwani Mtinika amesema kwa kuwa hakuna ujenzi unaoendelea kwenye barabara ya mwendokasi, ingetumika kupunguza adha ya foleni katika kipindi hiki cha mvua.
“Mradi wa mwendokasi kwa ngazi ya ujenzi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90, kwa kuwa mabasi bado hayajaanza ningeomba Tanroads waone haja ya kufungua njia ili itumike katika kipindi hiki cha dharura.
“Tunafahamu barabara nyingi za mitaa haziko vizuri kwa sababu ya mvua kwahiyo watu wote wanalazimika kutemea barabara kuu, msongamano unakuwa mkubwa zaidi nyakati za jioni naomba wafungue njia ili kupunguza hii adha ambayo wanakutana nayo hasa wakazi wa Mbagala,” amesema Mtinika.
Mbali na hilo meya huyo aliwataka wakazi wa Temeke kuendelea kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale yanapotokea madhira yanayosababishwa na mvua.
“Tunamshukuru Mungu hadi sasa hakuna maafa au madhira yoyote makubwa ambayo yametokea, hata hivyo niwasihi watu waendelee kuchukua tahadhari maana tuliambiwa mvua hivi ni kubwa na chochote kinaweza kutoke,” alisema Mtinika.
Hoja ya kuharibika kwa barabara za mitaa ilielezwa na madiwani wa kata kadhaa za manispaa hiyo wakihoji endapo kuna mikakati ya kuzifanyia marekebisho.
Juhudi za kuupata uongozi wa Tanroads hazikufanikiwa baada ya simu ya meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam kuita bila kupokelewa.
Akizungumza kwenye baraza hilo, Mkurugenzi wa manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika robo ya kwanza ya mwaka unakwenda vizuri.
Mabelya ametoa wito kwa madiwani kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi hiyo ili kupata matokeo yenye tija kwa jamii.