Prime
Siku 30 za ACT Wazalendo kujenga msingi wa ushindi

Muktasari:
- Viongozi wake wanasisitiza kushiriki uchaguzi badala ya kususia, wakihimiza umoja wa vyama vya upinzani na kuvutia wanachama wapya kutoka vyama vingine.
Shinyanga/Mbeya. Katika siku saba tangu kuanza kwa Julai 2025, Chama cha ACT Wazalendo kimekuwa kwenye harakati za kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini, kupitia kampeni iliyopewa jina la Operesheni ‘Majimaji linda kura’.
Kampeni hiyo, inayofanyika kwa siku 30 mfululizo, viongozi waandamizi wa chama hicho wapo ziarani mikoani, wakihamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Sambamba na hamasa hiyo, ziara hiyo pia imetumika na chama hicho kujijenga kisiasa, kuimarisha misingi ya chama na kuwasogeza wananchi karibu zaidi na ajenda zake za mabadiliko.
Kwa mtazamo wa haraka, inaweza kuonekana kama ni harakati za kawaida za chama cha siasa, lakini kwa jicho la ndani, operesheni hiyo ni mkakati wa kina unaolenga kuongeza ushawishi wa ACT kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu, huku ukijikita kwenye kujenga miundombinu ya ushindi kuanzia ngazi ya kijiji.

Akizungumzia operesheni hiyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda, amesema pamoja na hoja nzito zinazotolewa na viongozi katika ziara hiyo, wajiepushe na kushambuliana na vyama vingine vya upinzani.
Amesema ni bahati mbaya vyama vya upinzani kwa pamoja vimejikuta vikishambuliana vyenyewe kwa vyenyewe badala ya kusimama dhidi ya watawala.
“Walipaswa kuwa na sauti moja kama vyama vya upinzani ili kuwa na shinikizo kubwa na mwisho wa siku wangepata ripoti moja,” amesema.
Dk Mbunda amesisitiza ilipaswa ama wakubaliane kuingia kwa pamoja au kukataa kuingia kwenye uchaguzi kwa pamoja.
Mchambuzi huyo amesema mkakati wa kushambuliana unafanya washindwe kuvuna idadi ya wanachama kutoka vyama hivyo wanavyovishambulia.
Mchambuzi wa siasa, Ramadhani Manyeko amewataka viongozi wa chama hicho kujikita kutoa elimu ya uraia kwa wananchi na kueleza kwa kina falsafa yao.
"Hatima ya nchi hii ipo mikononi mwa wananchi wenyewe na imeainishwa kwenye Katiba ibara 8 hivyo ACT wawaeleze wananchi namna ya kuihami demokrasia, kwani kwa sasa kura haina thamani tena uamuzi umebaki ni hiari ya msimamizi wa uchaguzi kumtangaza mshindi," amedai Manyeko.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDMS), Dk Aviti Mushi amesema, "kwanza nawapongeze kwa kufanya siasa wakati huu. Wanajijenga na wanajiweka kwenye fikra ya wananchi.
"Hii ni sahihi kabisa. Wao ni chama cha siasa na wanafanya siasa, siku zinavyoendelea wazidi kuimarika kisiasa. Nategemea watavuna wabunge kadhaa kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu," amesema Dk Mushi.
Mizizi ya Majimaji
Jina Majimaji si la bahati mbaya. Linachota kumbukumbu ya harakati za kihistoria za wapambanaji wa uhuru waliopinga ukoloni wa Kijerumani kupitia Vita vya Majimaji vya mwaka 1905–1907.

Kwa kuchukua jina hilo, ACT Wazalendo inajitambulisha kama chama kinachopambana kwa ajili ya ukombozi wa pili wa kisiasa na kiuchumi, kadhalika ukombozi wa wananchi dhidi ya mifumo ya kiimla, ufisadi na udhalimu wa kisiasa.
“Tunarejea Majimaji si kwa sababu ya vita, bali kwa sababu ya ari ya wananchi kuamua hatima ya maisha yao. Tuko hapa kuwaamsha, kuwahamasisha na kuwahimiza kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa usahihi,” amesema Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe, katika moja ya hotuba zake katika ziara hiyo.
Kama ilivyo kwa Zitto, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Issihaka Mchinjita, amesema msingi wa kutumika kwa jina hilo ni historia ya harakati zilizofanywa na wazee wakati wa ukombozi wa Taifa dhidi ya Serikali ya kikoloni.
Kwa mujibu wa Mchinjita, jina hilo linathibitisha hali ya kutokata tamaa na kuthubutu kupigania haki bila woga, kama ilivyofanywa na waasisi wa Taifa walipopambana hata pasi na silaha stahiki.
Msisitizo wa hilo umewekwa pia na kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, aliyesema chama hicho kimejizatiti kushiriki uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu na si kususia.
Uamuzi huo, amesema, unalenga kujenga heshima na hadhi ya kura ya kila mwananchi, lakini wamerejea historia ya athari zilizowahi kupatikana kutokana na kususia uchaguzi.
“Hakuna aliyewahi kufanikiwa kwa kususia uchaguzi. Ukiwaachia watawala wanachukua nafasi zote na wanatumia fursa hiyo kujenga msingi wa kujiimarisha kwenye dola. Hatutasusia, tunaingia kupambana kama walivyopambana wazee wetu enzi za Vita ya Majimaji,” amesema Dorothy.
Majibu dhidi ya washindani
Ziara hiyo, inayohusisha mikoa ya Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam kwa upande wa Dorothy na Mchinjita, haikuishia kujenga hamasa ya wananchi kushiriki uchaguzi, bali imehusisha vijembe dhidi ya washindani.
Pia Zitto, akiwa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), wanaongoza ziara hiyo wakitembelea mikoa ya Tabora, Katavi, Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Lindi, Rufiji, kisha kumaliza jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika Kijiji cha Rungwe Mpya mkoani Kigoma, kada wa chama hicho, Peter Madeleka, amesema historia inaonyesha hakuna chama kilichowahi kufanikiwa kuzuia uchaguzi.

Sio hivyo pekee, amesema hata wanaodai wanataka kuzuia uchaguzi wameshindwa kuweka wazi mkakati utakaofanikisha uratibu wa jambo hilo.
Amesisitiza kauli yake hiyo kwa kuwaita wanasiasa wanaohamasisha kuzuia uchaguzi ni vibaraka wenye nia ya kuacha ushindi kwa watawala na si vinginevyo.
“Achaneni na vibaraka wanaotaka kuwaachia watawala washinde bila upinzani. Sisi tutakwenda kuingia kwenye uchaguzi kwa kuwa ni haki ya msingi ya kila raia na ndiyo mchakato unaokupa nafasi ya kumchagua kiongozi unayemtaka,” amesema Madeleka ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria wa chama hicho.
Hoja hizo za Madeleka zinakuja katikati ya nyakati ambazo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kampeni ya kuzuia uchaguzi iwapo mabadiliko ya kisheria hayatafanyika: ‘No reforms, no election.
Kada mwingine wa chama hicho, aliyeachana na Chadema mapema mwaka huu, Emmanuel Ntobi, amepigia msumari hoja za Madeleka, akisema historia inaonyesha madhara zaidi ya kuacha kushiriki uchaguzi kuliko faida.
Amesema Kwa sababu hiyo, ameihama Chadema na kujiunga na ACT Wazalendo, kwa kuwa ni jukwaa sahihi la kupigania mabadiliko dhidi ya watawala.
Amesisitiza uamuzi wake wa kukihama chama hicho si usaliti, bali ni hatua ya kutumia haki yake ya kikatiba kutafuta jukwaa sahihi la kuendeleza mapambano ya haki za raia.
…Chama kikuu cha upinzani
Akiwa wilayani Busega katika mkutano wa ndani na wanachama, Dorothy aliweka wazi msimamo wa chama hicho kuwa harakati na mikakati inayofanyika hailengi kupambania nafasi ya kuwa chama kikuu cha upinzani nchini, bali kiu ni kushinda uchaguzi na hatimaye kushika dola.
Katika kuijenga hoja hiyo, kiongozi huyo amesema wakati wadau mbalimbali wakidhani chama hicho kinalenga kuwa chama kikuu cha upinzani, hiyo si shabaha yao.
Badala yake, amesema, dhamira ya ACT Wazalendo ni kushinda uchaguzi na hatimaye kushika dola ili kuwaongoza Watanzania kwa misingi ya haki, uwazi na uwajibikaji.
“Tunasikia watu wanasemasema huko mitandaoni eti tunataka kuwa chama kikuu cha upinzani, siyo lengo letu kuwa na nafasi hiyo. Malengo yetu ni kushika dola,” amesema.

Kwa sababu malengo yao ni kushika dola, Dorothy amesema tayari wanatambua ili kulifikia lengo hilo, kunahitajika umakini, ujasiri na kujua wanachokitaka, yote hayo wanayo.
“Tumeamua kushiriki uchaguzi na kushinda. Tumejipanga kisayansi kuhakikisha tunashinda. Yale mambo ya unaingia kwenye uchaguzi hujui udhaifu wa mpinzani wako, mwaka huu hayatakuwepo,” amesisitiza.
Kuvuna wanachama wapya
Kwa jicho la haraka haraka unaweza kusema ziara ya viongozi wakuu imelenga kuhamasisha Watanzania kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, lakini ni mkakati wa kuvuna makada wapya.
Ni ziara ambayo kabla ya kufika katika mikutano ya hadhara, viongozi wakuu huanzia katika vikao vya ndani vinavyofanyika katika majimbo mbalimbali, vikihusisha viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya chini.
Katika vikao hivyo, Zitto akiwa na viongozi wenzake wanawajengea uwezo viongozi na makada wa chama hicho ngazi ya chini namna ya kushinda chaguzi, pamoja na kushawishi wanachama wengine kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar.
Wakiwa katika mikutano ya hadhara, viongozi wakuu wa ACT Wazalendo wanatumia majukwaa hayo kuwaomba wananchi na Watanzania kuwaunga mkono katika safari yao ya kuleta mabadiliko ndani ya Taifa.
Akihutubia kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika mikoa ya Tabora, Katavi, Rukwa na Mbeya, Zitto amewaita makada wa vyama mbalimbali kujiunga na chama hicho akisema ndicho jukwaa sahihi la kuleta mabadiliko.
“Njooni mjiunge na ACT Wazalendo, tuunganishe nguvu za kuiondoa CCM madarakani. Kususia uchaguzi si njia sahihi, sisi tumeamua kuingia kwenye mapambano.”
“Katika historia ya Tanzania hakuna uchaguzi ambao wagombea wa upinzani wameshinda ubunge au udiwani kirahisi, ni mapambano. Hivyo ni marufuku kukata tamaa. Twendeni tukashiriki uchaguzi tuiondoe CCM. Njooni katika jukwaa la ACT Wazalendo,” amesema Zitto.
Amesema ziara hiyo imejikita pia kuwaunganisha na kuwahamasisha Watanzania katika kudai haki kupitia sanduku la kura ili kuchagua viongozi wanaowahitaji badala ya kuwachaguliwa.
“Hii ndiyo kazi ambayo chama cha ACT Wazalendo tunaifanya, ya kuwaunganisha na kuwahamasisha Watanzania mkapige kura,” amesema Zitto.
“Tuunge mkono, hata tukipata mbunge mmoja au watatu, tutawatumia hao hao kufikisha bungeni ajenda na changamoto zinazowakabili Watanzania ili zipatiwe ufumbuzi,” amesema.
Zitto pia katika ziara hiyo ameeleza hoja na sababu za Watanzania kuwaunga mkono katika uchaguzi mkuu ujao huku wakibainisha kasoro na changamoto za ajira, umaskini na usimamizi wa rasilimali zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na CCM, iliyotawala Tanzania kwa miaka mingi.
Viongozi wengine walioambatana na Zitto, akiwemo Janeth Rithe, Kiza Mayeye na Ester Thomas, wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa Watanzania kujiunga na ACT Wazalendo ili kuunganisha nguvu za kuiondoa CCM madarakani ifikapo Oktoba.