Mdhamini jela miezi sita kwa kumtorosha mshtakiwa, atakiwa kulipa Sh5 milioni

Muktasari:
- Mdhamini huyo anadaiwa kumdhamini Khalid Haji tangu Juni 19, 2024, lakini hadi leo, mshtakiwa huyo hajawahi kufika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake ya kujipatia Sh2.4 milioni kwa njia ya udanganyifu pamoja na kujifanya ofisa usalama.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kifungo cha miezi sita jela na kulipa bondi ya Sh5 milioni mdhamini Erick Mwasongwe, baada ya kushindwa kuhakikisha mshtakiwa aliyemdhamini anafika mahakamani kila tarehe ya kesi hiyo inapopangwa.
Mwasongwe, aliyemdhamini Khalid Haji anayekabiliwa na shtaka la kujipatia fedha kwa udanganyifu na kujifanya ofisa usalama, amepewa adhabu hiyo leo, Jumanne, Mei 6, 2025, baada ya kushindwa kumpeleka mshtakiwa mahakamani hapo.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga, baada ya kukubaliana na ombi lililowasilishwa na Serikali la kutaka mdhamini huyo awajibishwe kwa kushindwa kutimiza wajibu wake wa kumpeleka mshtakiwa huyo mahakamani hapo.
Inadaiwa mshtakiwa huyo, baada ya kudhaminiwa Juni 19, 2024, hakuwahi kwenda mahakamani hapo kusikiliza kesi yake.
Leo, Jumanne, Wakili wa Serikali, Eric Davies, amewasilisha maombi hayo mahakamani hapo, akidai kuwa kwa mara ya kwanza mshtakiwa alisomewa mashtaka yake Juni 7, 2024, na kudhaminiwa Juni 19, 2024, na wadhamini wawili ambao walisaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.
"Hata hivyo, kesi hiyo ilipangwa kutajwa Julai 2, 2024, ambapo tangu tarehe hiyo, si mshtakiwa wala mdhamini, akiwemo Mwasongwe, hawakuonekana mahakamani na hakuna taarifa yoyote waliyo wasilisha," amedai Davies.
Wakili Davies ameendelea kudai pia kuwa Mwasongwe anakabiliwa na kesi nyingine ya jinai katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kwa kosa la kutorosha mshtakiwa.
"Tangu mshtakiwa adhaminiwe, takribani mwaka sasa, mdhamini hajaonekana wala mshtakiwa na hakuna taarifa yoyote. Mdhamini ameshindwa kutimiza wajibu wake. Naomba mahakama imwagize alipe bondi ya Sh5 milioni aliyosaini na kifungo cha miezi sita gerezani kama sheria inavyoelekeza," amedai Wakili Davies.
Hata hivyo, kabla ya kutoa uamuzi huo, mahakama ilimpa nafasi mdhamini ajitetee kwa nini asipewe adhabu kali.
Mwasongwe, katika utetezi wake, ameiomba mahakama impe wiki moja akamtafute mshtakiwa na kumfikisha mahakamani.
Amedai hakufahamu kama Haji alikuwa akimdanganya, kwani alikuwa akiwasiliana naye na alimhakikishia kuwa angefika mahakamani.
Akitoa uamuzi, Hakimu Ruboroga amesema kitendo cha mdhamini kutotoa taarifa mahakamani kinaonesha alikuwa na nia ovu ya kumtorosha mshtakiwa.
"Mahakama haiwezi kukuamini tena kwa mara ya pili kutokana na vitendo vyako. Inaonesha wazi ulikuwa na ushirikiano na mshtakiwa kumtorosha," amesema Hakimu Ruboroga, na kuongeza;
"Kutokana na hali hii na ombi lililowasilishwa na upande wa mashtaka, mahakama inakuamuru ulipie bondi Sh5 milioni uliyoisaini kama dhamana siku ulivyomdhamini Haji," amesema.
Mbali na adhabu hiyo, pia mahakama hiyo imemhukumu kifungo cha miezi sita jela ili iwe fundisho kwa wengine.
Katika kesi hiyo, Haji alikuwa anakabiliwa na shtaka la kujipatia fedha kwa udanganyifu kiasi cha Sh2.4 milioni, pamoja na kujifanya ofisa usalama, tukio analodaiwa kulitenda mwaka 2024 jijini Dar es Salaam.