Mchengerwa akutana na zomeazomea Vunjo, amkingia kifua Dk Kimei

Moshi. Katika hali ambayo haikutarajiwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amejikuta katikati ya zomea zomea katika Jimbo la Vunjo linaloongozwa na Dk Charles Kimei.
Hali hiyo ilijitokeza leo Mei 4,2025 kata ya Kahe wakati waziri huyo akizungumza na wananchi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika jimbo hilo na kupokea taarifa ya kazi alizozifanya Mbunge kutoka kwa Katibu wake, Gulatone Masiga.
Hata hivyo, wakati akijibu maelezo ya Katibu huyo na kuelezea kuwa Mbunge huyo anafanya kazi kubwa, ndipo baadhi ya wananchi walionyesha kutokukubaliana naye na ndipo ilimlazimu kutumia dakika kadhaa kumwelezea Dk Kimei.
“Mbunge wenu anawasaidia sana. Inawezekana asijue kuongea sana. Inawezekana mbunge wenu asijue sana kuongea akawa mtendaji zaidi,” kauli hiyo ilijibiwa na sauti kutoka kwa baadhi ya wananchi kutokubaliana naye na wengine kuzomea.
“Sasa nyie mnafikiri nipo hapa kwa sababu gani. Naomba niwaulize swali. Si ni mbunge kanituma?Mnataka niondoke? Sasa kwanini mnamzomea mbunge?Kwa sababu mbunge kaniomba nije. Mmenisikia, mmenielewa sasa,”alisema Waziri.
“Wakati mwingine unawqeza ukawa na Mbunge asiwe mjanja mjanja sana lakini mkawa na Mbungeambaye anawasemea kero zenu na matatizo yenu. Kwa hiyo msiangalie upande mmoja tu,”alisisitiza Waziri Mchengerwa katika hotuba yake.
“Kwa sabau wazee wetu hawa wamefanya kazi sana kwenye taifa hili. Kwa hiyo endeleeni kuwa na imani na kwa sababu nimeona ninyi ni watu wenye subira. Kwani barabara hii si imedumu miaka mingi?”aliwauliza wananchi hao.
Waziri Mchengerwa alisema changamoto zilizoelezwa na Katibu wa Mbunge zimedumu kwa miaka mingi na wameendelea kuwa na Subira na kwa kuwa amefika hapo mwenyewe, basi changamoto zao zinakwenda kutatuliwa.
“Lakini hata haya tunayoyafanya wawakilishi wenu ndio wanaowasemea ndani ya Bunge na kuhangaika huku na kule kuhakikisha kwamba wameleta yale ambayo mngetamani kuyaona katika maeneo yenu,”alisema Waziri na kuongeza:-
“Msikate tamaa hata kidogo. Msibeze. Nawaambia wazi kabisa. Wakati fulani mnaweza kumtamani mtu fulani lakini yale ambayo mnataka yasifanikiwe. Lakini mkawa na mtu mtaratibu,anafuatilia kidogo kidogo bila kugombana na Serikali”
“Anapita huku waziri atakuja. Kwa hiyo niwaombe sana. Kwa namna ambavyo mmekuwa na subira, endeleeni kuwa na subira na sisi kama Serikali ya wanyonge tutahakikisha zile kero zetu tumezitatua na tumezimaliza,”alieleza Waziri.
Awali akizungumza kwa niaba ya Dk Kimei, Katibu wake alielezea mafanikio katika Jimbo hilo akitaja ujenzi wa kituo cha Afya kilichojengwa kwa Sh520 milioni na wana eneo ambalo wana uhitaji na zahanati katika kijiji cha Mwangaria.
“Kipo kwenye kata hii ambapo tumepewa Sh47 milioni kwa ajili ya kufanya jambo pale lakini kutokana na mgogoro wa Kanisa na wananchi, fedha zile zilirudi Serikalini. Kwa hiyo sasa tunakuomba wananchi wameshatenga eneo,”alisema.
“Pili tuna shule chakavu sana. Tuna shule ya msingi Oria pamoja na hiyo ya Mwangaria. Ni shule chakavu sana. Mheshimiwa waziri, mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba hayo,”alisema Katibu huyo na kuongeza kusema:-
“Kubwa zaidi ambalo limetuweka hapa ni barabara hii ambayo leo tunaitembelea. Barabara ya Mabogini-Kahe na Chekereni. Ni barabara ambayo wananchi wote walioko hapa watapata faraja na watafurahi sana kwa yale ambayo umetuletea”