Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchengerwa awapa ujumbe Ma-RC, DC, atangaza ‘wiki ya muungano’

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amekagua miradi mbalimbali mkoani Mbeya na kuzungumza na wananchi huku akitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini, pamoja na kutangaza wiki ya Muungano kufanyika kila Aprili kwa shule za msingi na sekondari.

Mbeya. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini kutoruhusu chokochoko za uvunjifu wa amani na badala yake wachukue hatua, huku akionya siasa isiwe chanzo cha migogoro.

Katika hatua nyingine ametaka halmashauri kuwatumia makandarasi wazawa kutekeleza miradi ya maendeleo kutokana na kuonyesha moyo wa kizalendo kusimamia na kuteleza kwa wakati.

Adha, waziri huyo ameagiza shule zote nchini za msingi na sekondari kila ifikapo Aprili kuwe na 'Wiki ya Muungano' ili kutafakari tulipotoka, tulipo na tunapokwenda.

Amesema hatua hiyo itachangia kwa sehemu kubwa kurithisha kizazi kijacho na kutoa uelewa mpana kwa wanafunzi juu ya Muungano.

Mchengerwa ametoa maagizo hayo jana Jumamosi Aprili 26, 2025 katika ziara ya kikazi ya siku moja na kuweka jiwe la msingi katika miradi ikiwamo wa Soko la Matola, kituo cha kisasa cha mabasi ya mikoani kinachojengwa uwanja wa ndege wa zamani itakayogharimu Sh30 bilioni.

Fedha hizo zimetolewa na Serikali kupitia mkopo nafuu wa Benki ya Dunia (WB), ikiwa ni kutekeleza miradi ya uboreshwaji wa miji na majiji (Tactic) ambapo kwa Jiji la Mbeya inatekelezwa na Kampuni ya Sihotech Engineering Company Limited and AMJ Global Mult Contractors Company Limited JV.

Mchengerwa baada ya kukagua miradi hiyo amesema kuridhishwa na utekelezaji wake na kuweka bayana lengo la Serikali ya awamu ya sita kuja na mfuko wa Rais Samia Bond, wenye mikakati ya kuwezesha makandarasi wazawa.

"Awali Serikali tulikuwa na mashaka sana na makandarasi wazawa kuwapa miradi, lakini sasa tunaona namna wanavyotekeleza kwa wakati na natamani miradi yote ya Tamisemi wapewe wazawa," amesema.

Katika hatua nyingine, amezitaka halmashauri kuwatumia makandarasi wa ndani kutekeleza miradi na kumekuwepo na changamoto ya makandarasi wa kigeni kutokamilisha miradi kwa wakati na wengine kukimbia, baada ya kupewa fedha za malipo ya awali.

Pia, amehamasisha makandarasi wa wazawa kufanya kazi kwa ubora ili kuiwezesha Serikali kutotumia makandarasi wa nje kwa masilahi mapana ya Taifa.

Mchengerwa amesema ili kufikia malengo ya Serikali, lazima amani na utulivu wa nchi vilindwe isitokee watu wachache wataka kuivuruga na kusisitiza wakuu wa mikoa  na wakuu wa wilaya  kuchukua hatua pasipo kujalisha ni nani.

Amesema  Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere amelikomboa taifa na kuacha amani na upendo na kwamba siasa isiwe chanzo cha kuchochea migogoro na kusababisha uvunjifu wa amani  na umwagaji wa damu.

"Vijana lindeni amani msiruhusu kudanganywa kwa kuhakikisha mnatimiza ndoto za waasisi wetu kwa kufanya shughuli za kiuchumi kupitia fursa za nchi jirani za Malawi na Zambia," amesema.

Amesisitiza Serikali haitakuwa tayari kuona watoto na vizazi vijavyo vinakimbia kutokana na migogoro ya kisiasa badala ya kutafuta amani.

"Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, umefika wakati vijana wa karne hii tuwaenzi waasisi wetu," amesema.

Katika kusisitiza hilo, Waziri Mchengerwa amesema: “Kila mwezi wa nne unapoingia tutenge wiki ya Muungano, shule zote nchini kuanzia sasa, mwezi wa nne mwakani zitaanza kufanya maonesho ya sanaa, ngojela na mijadala kuhusu muungano.”

“Hii itakwenda sambamba na kutoa elimu ya msingi kuhusu Muungano na hii itakuwa shule zote za msingi na sekondari na nitazungumza na Waziri wa Elimu ili kuona uwezekano maelekezo haya yaende na vyuo vikuu vyote nchini, ili vizazi vya sasa na vijavyo vijue tulipotoka, tulipo na kule baba wa Taifa alitamani twende,” amesema.

Waziri huyo amesema kampeni hiyo itawakumbusha vijana kwamba Muungano si nyaraka bali ni hali ya watu kuheshimiana, kushirikiana na kulijenga Taifa kwa umoja.


Taarifa za miradi

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, John Nchimbi amesema utekelezaji wa mradi wa soko umefikia asilimia 50 ambapo katika mkataba ulipaswa kufikia asilimia 58.4.

Nchimbi amesema changamoto kubwa ni uwepo wa mvua nyingi lakini mkandarasi ameshauriwa kutengeneza mpango kazi kwa kuongeza vifaa na wataalamu ili kufidia muda uliopotea.

"Mradi ukikamilika utachukua wafanyabiashara 513, tofauti na awali walikuwa 450 sambamba na uwepo wa vizimba 204, maduka 207, vyumba vya baba na mama lishe 10, vibanda vya kuuzia kuku 20 na   vyumba 12 vya kuuzia samaki wabichi," amesema Nchimbi.

Kuhusu ujenzi kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, amesema umefikia hatua nzuri na ukikamilika  utakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi ya masafa marefu 113, daladala za ndani ya jiji 150, maegesho ya usafiri wa  bajaji  150, magari binafsi 68 na teksi abiria 68.

"Mbali na maeneo hayo bado kutakuwa na huduma muhimu mbalimbali hususani migahawa, kumbi za mikutano, starehe na maeneo ya kuhifadhi mizigo sambamba na kituo cha Polisi," amesema Nchimbi.

Nchimbi amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa akikagua ujenzi wa soko la Matola jijini hapa ,kabla ya kuweka jiwe la msingi. Picha na Hawa Mathias

Mfanyabiashara wa Soko la Matola, Asha Landa ameishukuru Serikali kwa kuboresha soko hilo kwani litachangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na mapato ya serikali.

Kwa upande wake, mwakilishi wa wabunge, Mbunge viti maalum Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa uwekezaji huo mkubwa na kwamba utaleta tija kubwa kiuchumi hususan kwa kinamama.